Habari za Punde

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Kassim Majaliwa Akagua Ujenzi wa Daraja la Mto Mbwemkuru Litakalounganisha Wilaya za Rungwa na Liwale.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipata maelezo  kutoka kwa Meneja wa Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini  (TARURA) wa Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa, Mhandisi Mashaka Nalupi kuhusu ujenzi wa daraja la mto Mbwemkuru litakalounganisha wilaya za Ruangwa na Liwale mkoani Lindi.

Muonekano wa ujenzi wa daraja la mto Mbwemkuru linalounganisha wilaya za Ruangwa na Liwale mkoani Lindi. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alikagua maendeleo ya ujenzi huo, Novemba 23, 2021. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)


Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Kassim Majaliwa amesema Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ana nia thabiti ya kuwatumikia Watanzania na kuendelea kuleta maendeleo nchini kote hususani maeneo ya vijijini.

 

Amesema kuwa Serikali inapeleka miradi mbalimbali ya maendeleo kwa ajili ya kuwanufaisha wananchi wote bila ya ubaguzi wa aina yoyote ikiwemo ya ujenzi wa miundombinu ya barabara, maji, elimu na afya.

 

Ameyasema hayo leo (Jumanne, Novemba 23, 2021) wakati akizungumza kwa nyakati tofauti na wananchi wa vijiji vya Lipande, Narungombe, Machang’anja na Namgurugayi akiwa katika ziara ya kikazi wilayani Ruangwa.

 

Akizungumza baada ya kukagua mradi wa ujenzi wa daraja la Mto Mbwemkuru linalounganisha wilaya ya Ruangwa na Liwale wenye thamani ya shilingi bilioni nne amesema mradi huo utapunguza adha ya usafiri katika maeneo hayo.

 

“Awali wananchi wa maeneo hayo walikuwa wanapata adha kubwa hasa kipindi cha masika ambapo walitumia mitumbwi na madumu kuvuka kutoka upande mmoja kwenda mwingine.”

 

Naye, Meneja wa TARURA wilaya ya Ruangwa Mhandisi Mashaka Nalupi amesema mradi huo ulianza kujengwa Januari 31, 2020 na unatarajiwa kukamilika Desemba 31, 2021 ambapo kwa sasa umefikia asilimia 54.

 

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amezengumza na wananchi wa kata Narungombe baada ya kukagua ujenzi wa kituo cha Afya cha kata hiyo, ambapo amesema ameridhishwa na ubora wake kwani umeendana na thamani ya fedha iliyoyolewa.

 

“Msisitizo wa Mheshimiwa Rais Samia kwenye ujenzi wa miradi ya Serikali ni ubora, kamati zote zilizopewa mamlaka ya kusimamia miradi hii ni lazima wajiridhishe na viwango vya ubora wake ili iendane na thamani ya fedha zilizotoka”

 

Aidha, Waziri Mkuu amesema kuwa Mheshimiwa Rais Samia ametoa fedha nyingi kwa ajili ya sekta ya elimu hivyo wazazi kote nchini wahakikishe watoto wote wenye umri wa kuanzia miaka minne wanakwenda shule. “Mzazi usikubali mtoto wako amefika miaka minne hadi mitano halafu anakaa nyumbani, msiwatumikishe watoto kwenye biashara wapelekeni shule.”

 

Pia, Mheshimiwa Majaliwa ametoa wito kwa Watanzania kutofanya shughuli za kibinadamu kwenye vyanzo vya maji. “Lindeni vyanzo vyetu vya maji, msiruhusu watu walime kwenye vyanzo kuweni walinzi wa maeneo hayo.”

 

IMETOLEWA NA:

OFISI YA WAZIRI MKUU,                                

JUMANNE, NOVEMBA 23, 2021

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.