Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi Ameshuhudia Utiaji wa Saini Uendeshaji Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume Zanzibar.

 

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akishuhudia utiaji wa saini wa mkataba wa Ushirikiano wa Uendeshaji wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume Zanzibar, hafla hiyo imefanyika katika ukumbi wa Ikulu Jijini Zanzibar. 

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Mwinyi amesema uamuzi wa Serikali wa kushirikiana na Kampuni za National Air Travel Agency (DNATA) pamoja na EGIS  katika uendeshaji wa Huduma za Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume Terminal III, unalenga kuimarisha uchumi kwa mtazamo mpana ili kuvutia mashirika ya ndege zaidi kufanya safari  zake hapa Zanzibar.

Dk. Mwinyi amesema hayo leo katika shughuli ya utiaji saini wa mkataba wa Mashirikiano ya Uendeshaji wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume (terminal 111), baina ya Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi na Dubai National Air Travel Agency (DNATA), pamoja na Kamuni ya EGIS, hafla iliofanyika Ikulu Jijini Zanzibar.

Alieleza kuwa ongezeko la ndege utaongeza idadi ya watalii wanaokuja kuitembelea Zanzibar, wageni, mizigo na ukuaji wa biashara pamoja na  soko la ajira.

Alisema ujio wa watalii utaambatana na ukuaji wa sekta mbali mbali muhimu katika ukuaji wa uchumi , akibainisha uamuzi huo wa Serikali umelenga kuleta manufaa mapana ya kiuchumi katika sekta zote.

Rais Dk. Mwinyi alizitaka taasisi zote zinazofanyakazi katika uwanja huo wa ndege ikiwemo za Serikali na binafsi kufanya kazi kwa ushirikiano ili kuleta ufanisi .

Alizitaja taasisi hizo ikiwemo Idara ya Uhamiaji, ZRB, Watendaji wa Wizara Afya pamoja na vyombo vya Ulinzi na Usalama kushirikiana na Kampuni hizo na   kuboresha utendaji wao  na kutoa huduma bora kwa wageni, vinginevyo mafanikio yanayotarajiwa kamwe hayawezi kufikiwa.

Aidha, aliishukuru wajumbe wa Kamati ya majadiliano ya Serikali kwa kazi nzuri waliyofanya mpaka kufikia makubaliano hayo yenye maslahi na Taifa, huku akibainisha kuwa zoezi hilo lilikuwa zito , gumu na lililochukua muda mrefu kukamilika.

“Nimeridhika sana kwamba mikataba hii  tuliotiliana saini imezingatia maslahi mapana ya nchi yetu”, alisema.

Rais Dk. Mwinyi alisema Serikali imeamua kutafuta Kampuni zenye sifa Duniani ili kuja kusaidiana katika uendeshaji wa Huduma za Kiwanja hicho cha Ndege kwa lengo la kuwa huduma zenye kiwango cha kimataifa.

Alisema Serikali imewekeza fedha nyingi zipatazo Dola za Kimarekani Milioni 128 kwa ajili ya ujenzi wa Terminal  111, pamoja na kuimarisha miundombnu ya barabara nje ya kiwanja, ujenzi wa uzio pamoja na maegesho ya magari, hivyo imelazimika kutafuta kmapuni zenye uwezo wa kimataifa ili kuwa na huduma zinazofanana na hadhi ya Terminal 111.

Alisema Kamapuni hizo zilizopatikana katika mchakato wa kuendesha huduma katika uwanja huo zina uwezo mkubwa na kutambulika kimataifa.

Aliongeza kuwa Kampuni hizo zimekuwa zikiendesha  shughuli katika nchi mbali mbali Duniani, ambazo zinafanana na zile zilizokabidhiwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar,  na kubainisha matumaini yake ya kupata huduma zinazohitajiwa.

Dk. Mwinyi alisema Kamapuni ya DNATA inatambulika  kwa uwezo wake mkubwa katika uendeshaji wa Viwanja vya Ndege vipatavyo 126 Dunini kote,ikiwa imeanzishwa tangu mwaka 1959.

Aidha, alisema kampuni hiyo ina uwezo mkubwa katika ushughulikiaji wa huduma za abiria, ushughulikia mizigo, kuweka taratibu nzuri na mwenendo wa ndege,  pamoja na masuala mbali mbali  ya Usalama wa  Abiri na  miziigo katika viwanja vya ndege.

Mapema, Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi Rahma Kassim Ali aliipongeza Kampuni ya DNATA  kwa kuteuliwa kuendesha huduma za  Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume Terminal 111, hivyo akaiomba kufanya shughuli zake kwa ufanisi, sambamba na kuwarithisha uzoefu wafanyakazi wazalendo ili kuwa bora na endelevu.

Alisema utiaji saini wa mikataba  minne juu ya Uendeshaji wa huduma katika Uwanja huo , ni miongoni mwa juhudi za serikali katika uimarishaji wa miundombinu ya anga pamoja na kurahisisha shughuli za usafiri na usafirishaji.

Alisema  Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi iliona ipo haja ya kushirkiana na  Kampuni za DNATA na EGIS kwa kuzingatia uzoefu na kutambulika kwao Kimataifa.

Nae, Makamo Mwenyekiti wa Kampuni ya DNATA ambae pia ni Mwenyekiti wa Kampuni ya Emirates Leisure, Steve Allen alisema  kupitia ushirikiano  uliotiwa saini hivi leo Kampuni hiyo itaweza kuzalisha ajira zisizo rasmi  zipatazo 400 kwa wazawa, sambamba na kuimarisha huduma katika uwanja huo wa ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume (terminal 111).

Aidha, Mkurugenzi wa Biashara wa Kampuni ya EGIS Christian Laugier alisema Kampuni hiyo inatoa huduma katika viwanja vya ndege 17 Barani Afrika, Zanzibar ikiwa cha tano miongoni mwao.

Jengo la Terminal 111 ambalo limefikia asilimia 90 ya ujenzi wake na linalotarajiwa kukabidhiwa Serikalini hivi karibuni, limejengwa  na Kampuni ya Beijing Contract Engineering Group (BCEG) kutoka nchini China, likiwa na urefu  wa mita za mraba 25,000 na uwezo wa kuhudumia Abiria 1,600,000 kwa mwaka.

Katika hafla hiyo jumla ya mikataba  minne imetiwa saini, ikiwemo Mkataba wa Huduma za Abiria na mizigo, mkataba wa huduma za  Uendeshaji, mkataba wa kumbi za wageni pamoja na mkataba wa uendeshaji wa huduma za Maduka na Migahawa.

Kitengo cha habari,

Ikulu Zanzibar. 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.