Habari za Punde

Maonesho ya Sita ya Viwanda Vya Tanzania Kufungwa Viwanja vya Maisara Suleiman Zanzibar.

Na Khadija Khamis –Maelezo Zanzibar 10/12/2021.

Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda Mhe.Omar Said Shaaban amesema Serikali itaendelea kuviwezesha viwanda vidogo vidogo na vya kati ili kufanya kazi zao kwa ufanisi.


Amesema kufanya hivyo kutasaidia sekta binafsi kuingia katika ushindani wa masoko ya kikanda na kimataifa .


 Akiyasema hayo huko Maisara wakati wa kufunga Maonyesho ya sita ya Viwanda vya Tanzania alisema  soko imara la ndani litajenga msingi bora  wa ushindani katika soko la kikanda na kimataifa 

.

Aidha alizitaka Benki na Taasisi za kifedha kufikiria kutoa mikopo rafiki kwa sekta ya viwanda na biashara nchini kwa kuimarisha viwanda vidogo na vya kati ili  

viweze kuzalisha bidhaa na kutoa huduma bora kwa wananchi .


Alisema nchi tayari imeridhia mikataba mbali mbali ya kikanda na kimataifa ili wafanyabiashara kupata fursa za masoko kwa uzalishaji wa bidhaa ili kujenga hamasa ya uzalishaji nchini .


Aidha alisema kwa upande wa Zanzibar iko fursa hiyo kwa takwimu zilizopo jumla ya viwanda elfu 2200, na vikubwa vitano ambavyo vimetoa ajira elfu 7100 na kuifanya jumla ya ajira kwa viwanda vyote 11,000 .


“Katika mwaka 2021 zaidi ya vijana 4000  wamejipatia fursa ya ajira kutokana na viwanda vinane vipya vilivyofunguliwa”alisema Waziri.


Nae Katibu Mkuu wa Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda Dkt . Islamu Seif Salum amesema changamoto za wazalishaji na wawekezaji zinaendelea kutatuliwa na serikali zote mbili ili kuhakikisha wanapata tija katika kazi zao


Akitoa wito kwa wenye viwanda na wafanya biashara  aliwataka kutii sheria kanuni na taratibu zinazotolewa na serikali pamoja na miongozo mbali mbali ili kuhakikisha changamoto zilizopo zinaondoka 

  

Kwa upande wa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maendeleo ya Viwanda Tanzania (TANTRADE ) Latifa Mohamed Khamis  aliwashukuru washiriki wote  wa maonyesho hayo pamoja na  watembeleaji mbali mbali, waliofika katika maonyesho hayo ya  kitaifa yalioshirikisha ushiriki wa viwanda katika maeneo yote ya Tanzania .


Alisema lengo la maonyesho hayo ni kuihamasisha jamii kufahamu bidhaa zilizopo nchini pamoja na kutumia rasilimali  zilizopo na jumla ya Kampuni 113 zilishiriki katika maonyesho hayo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.