Habari za Punde

Wanamipango Watakiwa Kutatua Changamoto za Ajira na Umasikini Nchini.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Adolf Nduguru, akiwataka wanamipango nchini kufanya kazi kwa bidii ili kutatua changamoto ya ajira kwa vijana, wakati akifungua Kongamano la Wanamipango kwa mwaka 2021, katika Ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango, jijini Dodoma.
Meza Kuu ikiongozwa na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Adolf Nduguru (katikati), wakisikiliza kwa makini maelezo ya baadhi ya wajumbe wa Kongamano la Wanamipango kwa mwaka 2021, katika Ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango, jijini Dodoma, kulia ni Kamishna wa Fedha za Nje, Bi. Sauda Msemo na aliyeko kushoto ni Kaimu Kamishna wa Idara ya Mipango ya Kitaifa wa Wizara hiyo, Bw. Ekingo Magembe.
Baadhi ya viongozi wa Wizara ya Fedha na Mipango na wajumbe wa Kongamano la Wanamipango kwa mwaka 2021 wakisikiliza hotuba ya Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Adolf Nduguru wakati akifungua Kongamano la Wanamipango kwa mwaka 2021, katika Ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango, jijini Dodoma.

Na. Farida Ramadhani, WFM, Dodoma

Wanamipango nchini wametakiwa kuhakikisha wanapanga na kusimamia vema utekelezaji wa Mipango ya maendeleo kwa kuweka na kutekeleza vipaumbele vya kutatua changamoto ya ukosefu wa ajira kwa vijana, athari za mabadiliko ya tabianchi, umaskini na maradhi mapya hususan UVIKO-19.

Rai hiyo imetolewa jijini Dodoma na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Adolf Ndunguru  kwa niaba ya Katibu wa Wizara hiyo, Bw. Emmanuel Tutuba, wakati akifungua Kongamano la Wanamipango la mwaka 2021 linalowashirikisha wanamipango zaidi ya 220.

Alisema kuwa changamoto hizo zimekuwa zikilikabili Taifa kwa muda mrefu na kubainisha kuwa wanamipango hao wanajukumu kubwa la kuzitatua.

Akizungumzia kongamano hilo ambalo dhima yake ni Mwanamipango Imara, kwa Ustawi wa Taifa, Bw. Ndunguru alisema dhima hiyo imezingatia jukumu la Wanamipango la kuibua, kupanga, kutekeleza, kufuatilia, kutathmini na kutoa taarifa za utekelezaji wa mipango ya maendeleo.

“Tunakaribishwa kujifunza, kuwa na majadiliano mazuri ya kujenga, kutoa maoni na ushauri. Wizara ya Fedha na Mipango inaahidi kuyafanyia kazi Maazimio yote yatakayotolewa katika Kongamano hili”, alisema Bw. Ndunguru.

Aliwataka wanamipango kuendelea kushauri na kutoa mapendekezo kwa Serikali kwa lengo la kuboresha utekelezaji wa majukumu yao ya msingi na kuendeleza kada hiyo.

“Mada zilizoandaliwa katika Kongamano la mwaka huu zimezingatia mafanikio yaliyopatikana katika utekelezaji wa maazimio ya kongamano la mwaka jana, ambayo ni pamoja na Kada za Wanamipango kuendelea kupewa umuhimu na kipaumbele kwa kuendeleza na kuimarisha malezi ya kitaasisi kwa wanamipango”, alibainisha.

Aidha, Bw. Ndunguru aliwapongeza waandaaji wa Kongamano hilo kwa kutekeleza maazimio ya Makongamano yaliyotangulia ikiwemo kuanzishwa kwa Mfumo wa Kitaifa wa Kusimamia Miradi ya Maendeleo na kuanza maandalizi ya Kanzidata ya Wanamipango kwa lengo la kuwatambua na kuwa na mikakati madhubuti ya kuilea kada hiyo.

Kwa upande wake, Kaimu Kamishna Msaidizi wa Idara ya Mipango ya Kitaifa, Bw. Ekingo Magembe, alisema nchi ipo katika hatua za kukamilisha utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo mwaka 2025 na kuanza maandalizi ya Dira mpya, ambapo Serikali imeona ni muhimu kuhakikisha waandaaji na watekelezaji wa Mipango wanajengewa uwezo katika kutekeleza dira.

Alisema kongamano hilo litawajengea uwezo washiriki kuhusu masuala ya uibuaji na uandaaji wa Maandiko ya Miradi ya Maendeleo pamoja na uchambuzi wa Sera.

Kongamano la Wanamipango nchini hufanyika kila mwaka ambapo huwakutanisha wachumi, maafisa mipango, watakwimu na wanademografia kutoka Wizara, Taasisi na Mashirika ya Umma, Wakala wa Serikali, Idara zinazojitegemea, Sekretarieti za mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.