Habari za Punde

Wanavyuo Waaswa Kuiepusha na Ukatili Mitandaoni.

Mkurugenzi wa Maendeleo ya Jinsia, Mwajuma Magwiza akikabidhi nakala ya mwongozo wa uanzishwaji na uendeshaji wa dawati la Jinsia kwenye vyuo ya kati na juu kwa mmoja wa mwanafunzi wa chuo Mkoani Kigoma.

Na Mwandishi Wetu Kigoma

Wanavyuo nchini wameaswa kuwa na matumizi sahihi ya mitandao ya kijamii na kujiepusha na matumizi mabaya ya mitandao hiyo inayoweza kusababisha vitendo vya ukatili.

 

Wito huo umetolewa Mkoani Kigoma na Mkurugenzi wa Maendeleo ya Jinsia, kutoka Wizara ya Afya, Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii Mwajuma Magwiza wakati akizungumza na wanavyuo mbalimbali Mkoani hapa kuhusu muongozo wa uanzishwaji wa madawati ya jinsia Vyuoni. 

 

Mwajuma amesema wanafunzi wengi wanaingia kwenye matatizo ya kudhalilishwa kutokana na kutumia vibaya mitandao ya kijamii ambapo wengi wao imewapeleka kupata matatizo ya kisakolojia na hata wengine kukatisha uhai wao.

 

"Wizara tumeona tuje na mifumo mbalimbali ikiwemo kuanzisha madawati haya na tunatendelea kuweka mifumo hii maeneo mengi ikiwemo vituo vya mabasi, sokoni na maeneo yote ya wazi ili kupambana na vitendo hivi vya ukatili" alisema Mwajuma

 

Ameongeza kuwa jukumu la kulinda watoto, kujilinda wenyewe na kuhakikisha Amani ya nchi yetu ni jukumu letu zote, sababu za ukatili tulizoziainisha tunaweza kuzisimamia na kuzuia madhara ikiwemo Mila na Desturi zilizopitwa na wakati.

 

Awali akiwasilisha mwongozo wa kuanzisha na kuendesha dawati la Jinsia katika vyuo vya elimu ya juu na ya kati kwa wanafunzi hao, Afisa kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Alex Shayo amesema lengo ni kutekeleza kwa pamoja jitihada za kuondokana na vitendo vya ukatili vyuoni kwa kutoa taarifa katika dawati hilo ili hatua ziweze kuchukuliwa dhidi ya wanaofanya vitendo hivyo. 

 

 Baadhi ya wanachuo wamesema mwongozo huo utawasaidia kujua namna ya kupata na kutoa taarifa za ukatili na hivyo kuleta suluhisho la ukatili vyuoni ambapo wanafunzi walio wengi walikuwa wanakosa sehemu sahihi ya kutoa taarifa za vitendo hivyo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.