Habari za Punde

Waziri wa Ujenzi Mawasiliano na Uchukuzi Zanzibar Mhe.Rahma Kassim Ali Amefanya Ziara ya Kushtukiza Bandarini leo.Atakaezidisha abiria kuchukuliwa hatua za kisheria

WAZIRI wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Rahma Kassim Ali akizungumza na Waandishi wa habari baada ya kufanya ziara ya kushtukiza katika bandari ya Malindi Jijini Zanzibar,
kuangalia upakiaji wa abiria katika meli zinazofanya safari zake kati ya Unguja na Pemba.

WAZIRI wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Rahma Kassim Ali akiangalia utaratibu wa uchukuaji tiketi kabla ya abiria kuingia katika meli ya Sealink iliyokua inakwenda Pemba wakati wa ziara yake ya kushtukiza katika bandari ya Malindi Jijini Zanzibar, kuangalia upakiaji wa abiria katika meli zinazofanya safari zake kati ya Unguja na Pemba.

BAADHI ya Abiria wakiwa wamekaa chini katika Meli ya Ikraam Sealine I ilikua inatoka Unguja kwenda Pemba na kuacha viti vikiwa vitupu.

Na.Haroub Hussein -Zanzibar.

WAMILIKI wa vyombo vya usafiri wa baharini wametakiwa kuhakikisha wanafuata taratibu za upakiaji abiria kwa mujibu wa uwezo wa chombo husika.

Kauli hiyo imetolewa leo na Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Rahma Kassim Ali wakati alipofanya ziara ya kushtukiza katika bandari ya malindi Jijini Zanzibar.

Waziri Rahma alisema ni vyema kwa wamiliki wa vyombo hivyo kufuata utaratibu wa kupakia abiria na mizigo kwa mujibu wa uwezo wa chombo na sio kupakia kwa kuzidisha idadi inayoruhusiwa jambo linaloweza kusababisha ajali zisizokua za lazima.

‘‘Nimeamua kuja mwenyewe bila ya taarifa ili kujionea namna utaratibu unavyokwenda , kipindi hiki cha disemba abiria huwa wengi sana, hatutaki meli zipakie kupita idadi iliyoruhusiwa na mamlaka kutokana na uwezo wa meli husika‘‘ alisema waziri Rahma.

Aidha alisema wizara yake haitasita kuchukua hatua za kisheria ikiwemo kuipiga faini kampuni yoyote itakayokwenda kinyume na taratibu ziliopo.

Alisema katika kuhakikisha abiria na mizigo yao wanasafiri salama ni lazima kwa taasisi zote zinazofanya kazi katika bandari nchini zihakikishe zinafanya kazi zao ipasavyo.

‘‘Kabla ya ziara yangu hii mnamo tarehe tano mwezi huu tuliwaita wamiliki wa vyombo hivi na tukawaeleza kuwa disemba ni mwezi unaokua na abiria wengi kutokana na kufungwa kwa skuli na sikukuu ziliopo mwisho wa mwaka, hivyo wawe makini katika kupakia abiria kwa utaratibu ulio mzuri na sio kupakia tuu kwa vile abiria wapo wengi, ziara yangu hii ni kuja kujionea kuwa tulichokubaliana kinafuatwa au laa?.‘‘ alisikika waziri huyo.

Aidha waziri Rahma alisema kutokana na idadi kubwa iliopo katika mwezi wa disemba wamewataka wamiliki wa vyombo vya moto nchini kuongeza idadi ya safari zao kwa wiki ili kuondosha adha ya usafi  huku kukiwa na usafiri unaofuata taratibu zote zilizowekwa.

Waziri Rahma aliitaka Mamlaka ya usafiri baharini Zanzibar (ZMA)kufanya kazi zao ipasavyo bila ya kumuonea muhali mmiliki yoyote na kuhakikisha wanachukua hatua zinazofaa kwa yoyote atakaekiuka taratibu ziliopo.

Nae Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya usafiri baharini Zanzibar (ZMA),Sheikha Ahmed Mohammed alisema kuwa mamlaka hiyo inafanya kazi zake kuhakikisha taratibu ziliopo zinafuatwa kama inavyotakiwa na ikitokea vyenginevyo hatua za kisheria huchukuliwa dhidi ya aliekiuka taratibu hizo.

Sheikha alisema wamekua wakifanya ukaguzi wa kila siku na ule ukaguzi mkubwa mara kwa mara ili kuhakikisha usalama wa abiria na mizigo unakua wa uhakika pale wanapokua katika vyombo hivyo.

Tumekua tukihakikisha vyombo vyote vinapakia kwa mujibu wa idadi inayotakiwa na kila abiria ana tiketi yake pamoja na taratibu nyengine za kiusalama zinafuatwa kama ilivyoelekezwa na sheria zetu.

‘‘Mbali na kufuatilia taratibu zote hizo kumekua na changamoto ya uchukuaji wa watoto kwa kiasi kikubwa jambo linaloweza kuhatarisha usalama wao, utaona mtu mmoja ana watoto zaidi ya watano hii ni hatari kwa usalama wa abiria na watoto husika tunaomba jamii ibadike katika suala hilo’ alisema mkurugenzi mkuu zma.

Kwa upande wake ofisa mkuu wa meli ya Ikraam sea line I , Boniface Tumbi Silube  alisema wamekua  na utaratibu wa kupakia abiria na mizigo kwa mujibu wa uwezo wa meli yao lakini kumekua na changamoto kwa abiria wao ya kukaa chini na kuacha viti vikiwa vitupu.

Amesema abiria walio wengi hawataki kukaa katika viti hivyo hufanya meli ionekane kuwa imejaa wakati halisi halisi haiku hivyo.

Aidha alisema changamoto nyengine ni kuwa na idadi kubwa ya watoto kutokana na abiria mmoja huchukua watoto wengi jambo linalowapa wakati mgumu katika safari.

Alisema meli yao ina uwezo wa kubeba abiria 1,156 na tani 350 za mizigo lakini katika safari ya leo kutoka Unguja kwenda Pemba wamebeba abiria 1,094 na watoto 190 huku wakiwa wamepakia mizigo ya tano 50 tuu.

Nae ofisa zamu wa kituo cha zimamoto na uokozi (KZU) bandari ya malindi, ispekta Mohammed Salum Ali alisema ni vyema kwa serikali ikaweka utaratibu maalum ya kila abiria kusafiri na idadi isiyozidi watoto wawili ili kuhakikisha usalama wao pale itakapotokea dharura, tofauti na ilivyo sasa abiria mmoja huwa na zaidi ya watoto wanne.

Alisema kwa sasa kumekua na wimbi kubwa la watoto walio chini ya umri wa kukatiwa tiketi kuchukuliwa na abiria mmoja jambo linalowafanya watoto hao kuwa katika hatari kubwa ikitokea dharura kwa kukosa mtu wa kuwashughulikia.

Nao baadhi ya abiria waliokua wakisafiri na meli ya sealink na Ikraam sealine I walimpongeza waziri rahma kwa kufika bandarini hapo kuangalia hali ya usalama katika vyombo hivyo.

Walisema ni jambo jema kwa serikali kuona wanasimamia taratibu zilizowekwa ili usalama wa abiria na mali zake uweze kupatikana.

Abiria hao walisema ufuatiliwaji wa  karibu wa wafanyabiashara hao utasaidia kuondokana na ujanja unaoweza kufanywa kwa kukwepwa taratibu endapo kutakua hakuna ufuatiliaji wa namna hiyo.



No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.