Habari za Punde

Wizara ya Biashara yakemea upandishaji wa bidhaa za chakula

 Na Khadija Khamis – Maelezo . 02 /12/2021.

Wizara ya  Biashara, Maendeleo na Viwanda imesema itawachukulia hatua Wafanyabiashara watakaopandisha bei za bidhaa kinyume na taratibu zilizowekwa na Taasisi husika .

Akizungumza katika kikao na Waandishi wa Habari, katika ukumbi wa leseni malindi , Waziri wa Biashara  Maendeleo na Viwanda Mhe.Omar Said Shaaban amesema kwa mujibu wa sheria na bei elekezi ya ushindani halali ya kumlinda mlaji imeeleza bei zitakazotumika ni zile zilizoelekezwa kisheria  .

Alisema Tume ya Ushindani Halali wa Biashara na Kumlinda Mlaji na Idara ya Biashara  wamefanya uchunguzi kwa wafanyabiashara na kubaini  wanaoengeza bei kinyume na zile zilizoelekezwa.

 Alifahamisha kuwa tayari kwa sasa wameshafutiwa leseni zao wafanyabiashara sita kutokana na kwenda kinyume na bei elekezi kwa kupandisha bidhaa za chakula ikiwemo Sukari, Mchele na Unga wa Ngano.

“Maeneo tuliofanyia ufuatiliaji wa bei hizo ni Konde, Wete, Micheweni na Chake Chake kwa upande wa Pemba na kwa Unguja ni Darajani, Mwanakwerekwe na Mombasa shimoni,”alisema Waziri .  

Aidha alisema Wizara yake inaendelea kukusanya taarifa na kufuatilia kwa karibu mwenendo wa biashara ya ndani na nje ya nchi  kwa lengo la kuhakikisha kuna ushindani halali wa biashara na kumlinda mlaji.

Waziri huyo aliwataka wafanyabiashara waingizaji wa bidhaa za chakula nchini kutopandisha bei ya chakula kabla ya kuwasiliana na mamlaka husika ili kupata idhini na uhalali wa kufanya hivyo .

Akitoa wito kwa wananchi kuwataka  wasisite kutoa taarifa za wafanyabiashara wanaokiuka maagizo ya serikali kuhusu bei ya bidhaa hizo muhimu kupitia Tume ya Kumlinda Mlaji au Idara ya Biashara .

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.