Balozi wa China
nchini Tanzania, Zhang Zhisheng amesema msaada wa Vyerahani uliotolewa na Ubalozi huo kwa Jumuiya ya “Zanzibar Maisha
Bora Foundation”, unalenga kuwawezesha wanawake wa Zanzibar ili kuondokana na
umasikini.
Balozi Zhang amesema hayo wakati alipokabidhi Vyerahani vinane kwa Uongozi wa Jumuiya ya Zanzibar Maisha Bora Foundation, hafla iliofanyika katika Ubalozi huo, uliopo Mazizini Jijini Zanzibar.
Amesema msaada wa Vyerahani hivyo vinane, ni mwanzo wa misaada mbali mbali inayolengwa kutolewa na Ubalozi huo kwa Jumuiya hiyo ili kuwawezesha wanawake wa Zanzibar kuinua maisha yao.
Nae, Mtendaji Mkuu wa Jumuiya hiyo Mwanaidi Mohamed Ali, kwa niaba ya Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo Mama Mariam Mwinyi aliushukuru Ubalozi wa China nchini Tanzania kwa msaada huo, na kusema hatua hiyo inaonyesha dhamira ya Ubalozi huo katika kushirikiana na Jumuiya hiyo, ili kuwawezesha wanawake Zanzibar.
Alisema Jumuiya ya Zanzibar Maisha Bora Foundation inathamini msaada huo na itaendelea kushirikiana na Ubalozi huo, huku akiahidi kutumika vyema kwa malengo yaliokusudia.
Msaada wa Vyerahani vinane uliotolewa na Ubalozi wa China nchini Tanzania, unatokana na mkutano wa Wadau uliofanyika Januari 26, mwaka katika Hoteli ya Golden Tulip, Zanzibar – Airport, uliolenga kuwahamaisha wadau mbali mbali kushirikiana na Jumuiya hiyo ili kufanikisha malengo yaliokusudiwa.
Jumuiya ya Zanzibar Maisha Bora Foundation, ambapo malengo yake makuu ni kuinua maisha ya wanakake wa Zanzibar kuondokana na umasikini, inatarajiwa kuzinduliwa rasmi mwezi ujao.
Imetayarishwa na Kitengo cha Habari,
Ikulu Zanzibar
No comments:
Post a Comment