Habari za Punde

Wizara ya afya yapokea msaada wa chanjo ya UVIKO 19 - Sinopharm kutoka China

Kaimu Waziri wa Afya , Ustawi wa Jamii,Wazee Jinsia na Watoto Mhe. Simai Mohammed Said, akipokea Chanjo ya UVIKO – 19 aina ya SINOPHARM kutoka kwa Balozi Mdogo wa China Nchini, Zhang Zhi Sheng, huko Uwanja wa Ndege wa Abeid Amani Karume Mjini ZaNZIBAR.
Katibu Mkuu Wizara ya Afya , Ustawi wa Jamii,Wazee Jinsia na Watoto Dkt. Fatma Mrisho akitowa shukurani kwa Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China kwa kuwapatia Msaada wa Chanjo ya UVIKO – 19 aina ya SINOPHARM. 

 Mkurugenzi Kinga na Elimu ya Afya Dkt. Ali Said Nyanga, akisisitiza Jamii kuchukua tahadhari ya UVIKO – 19, baada ya makabidhiano ya Chanjo ya UVIKO – 19 aina ya SINOPHARM kutoka kwa Balozi Mdogo wa China Nchini, Zhang Zhi Sheng, huko Uwanja wa Ndege wa Abeid Amani Karume Mjini ZaNZIBAR.

Kaimu Waziri wa Afya , Ustawi wa Jamii,Wazee Jinsia na Watoto Mhe. Simai Mohammed Said, wakiagana na Balozi Mdogo wa China Nchini, Zhang Zhi Sheng, huko Uwanja wa Ndege wa Abeid Amani Karume Mjini Zanzibar.        (PICHA NA MARYAM KIDIKO – MAELEZO)

Na Kijakazi Abdalla           Maelezo   2

Wizara ya Afya, Ustawi wa Jamii,Wazee, Jinsia na Watoto Zanzibar imepokea msaada wa chanjo ya Uviko 19 aina ya Sinopham kutoka Serikali ya Jamuhuri ya watu wa China

Hafla hiyo ya Makabidhiano ilifanyika huko Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume Mjini Zanzibar,Kaimu Waziri wa Afya ,Ustawi wa Jamii,Wazee,Jinsia na Watoto Simai Mohammed Said amesema jumla ya chanjo ya dozi 200,000  zimepokelewa ambazo zitatumika kuchanja wananchi wapatao 100.000.

Amesema hii ni awamu ya pili kwa chanjo ya aina hiyo kutoka Serikali ya China kuipatia Zanzibar  ambapo awamu ya kwanza ilipokea dozi 110,000 za chanjo  ambazo zilitumika kuchanja wananchi 52,000.

Aidha amesema mapokezi hayo yanafanya kuwa na jumla ya chanjo zilizopokelewa nchini tangu kutolewa chanjo dhidi ya uviko19 hadi sasa kuwa dozi 422,520.

Vilevile Kaimu Waziri wa Afya amesema jumla ya watu 1,39,431 wamepata chanjo kamili hapa Zanzibar kati ya watu waliopata chanjo za uviko 19 na mpaka sasa hakuna taarifa yoyote ya kupata madhara na kuthibitika kuengeza kinga mwilini na kupunguza makali kwa wale waliopata maambukizi ya virusi vya korona.

Hata hivyo amesema kwa sasa takwimu zinaonesha kuwa Mkoa  unaofanya vizuri katika kutekeleza utoaji wa chanjo ya uviko 19 ni Mkoa Mjini Magharibi ambapo jitihada zaidi zinahitajika kwa mikoa mengine.

Nae Balozi Mdogo wa China nchini Zhang  Zhi Sheng amesema Serikali yake itaendeleza mashirikiano zaidi  na  Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika kuchukua jitihada  za kupambana na uviko 19 nchini.

Aidha amemshukuru Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk Hussein Ali Mwinyi kwa kuwa pamoja na mapambano dhidi ya Uviko 19 kwa kuyadhibiti na kupatiwa chanjo wananchi.

Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dk Fatma Mrisho ameishukuru Serikali ya Jamuhuri ya Watu wa China kwa msaada wake kwa vile Zanzibar inahitaji msaada huo.

Aidha amewataka wananchi kuchukua hatua mbalimbali za kujikinga na uviko 19 ikiwa pamoja na uvaaji wa barakoa,kunawa mikono kwa maji na sabuni kwa kutumia vitakasa mikono na kupunguza mikusanyiko isiyokuwa na lazima.

Hata hivyo amewaomba Wakuu wa Mikoa kuongeza juhudi za kuhamasisha jamii ili kiwango cha utoji chanjo uongezeke na wapate chanjo kama walivyoshauriwa na wataalamu.

 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.