Habari za Punde

Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Zanzibar Aapishwa leo Ikulu.

 

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi  akimuapisha Kanali Burhan Zuberi Nassor kuwa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Zanzibar, hafla hiyo iliyofanyika katika Ukumbi wa Ikulu Jijini Zanzibar leo 25-2-2022

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Hussein Ali Hassan Mwinyi leo amemuapisha Kanali Burhani Zuberi Nassor kuwa Kamishna  Mkuu  wa Mamlaka  ya Kudhibiti  na Kupambana  na Dawa za Kulevya Zanzibar.

Hafla ya kuapishwa kiongozi huyo ilifanyika Ikulu Jijini  Zanzibar ambayo ilihudhuriwa na viongozi mbali mbali wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar akiwemo Makamo wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Othman Masoud Othman, Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Hemed Suleiman Abdullah, Spika wa Baraza la Wawakilishi Zubeir Ali Maulid.

Wengine ni Kaimu Jaji Mkuu wa Zanzibar  Khamis Ramadhan Abdallah, Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi  Idrissa Kitwana Mustafa, Mawaziri, Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar Dk. Mwinyi Talib Haji,  Makatibu Wakuu, Viongozi wa Dini, Viongozi wa Vyama vya siasa, Wakuu wa Vikosi vya Ulinzi na Usalama pamoja na wanafamilia.

Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kula kiapo  hicho Ikulu Jijini Zanzibar, Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Kuthibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Zanzibar, Kanali Burhani Zubeiri Nassor alisema kuwa kupambana na dawa za kulevya ni jambo linalohitaji ushirikiano ya kina.

Alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imechukua sura mpya kulingana na nchi nyengine duniani  ambazo zimeweka sheria kali na zinazodhibiti dawa za kulevya.

Aliongeza kuwa sheria iliyopo hivi sasa ni mpya  hivyo, inahitaji ushirikiano mkubwa kutoka kwa wananchi pamoja na viongozi kwani uhalifu bao uko katika jamii pamoja na mitaani hasa ikizingatiwa kwamba Zanzibar ni kisiwa na ina bandari bubu zipatazo 371  hivyo, ushirikiano wa kina unahitajika kuanzia Shehia hadi Taifa.

“Hii dhima ni kubwa lakini kwa pamoja tutahakikisha kwamba Zanzibar bila ya Dawa za kulevya inawezekana na dira ya Mamlaka ni kuhakikisha kwamba Zanzibar inakuwa huru kutokana na dawa za kulevya ifikapo mwaka 2050”, alisema Kanal Nassor.

“ ”Kwa  sheria hii mpya hakuna mtu anayeitwa papa na kila mtu yuko chini ya sheria na nitahakikisha hata akiwa mke wangu anashiriki dawa za kulevya anakamatwa na kufikishwa katika vyombo vya sheria, sitokuwa na muhali wala sitomuonea mtu isipokuwa nitatimiza wajibu wangu na matakwa ya sheria hii”, aliongeza Kanali Nassor.

Pamoja na hayo, Kanali Nassor alimshukuru Rais Dk. Mwinyi kwa kujiandaa kumpa ushirikiano mkubwa kwa kumpatia vifaa vya kutosha katika mapambano hayo sambamba na ahadi iliyotolewa na Serikali ya Uingereza baada ya kusaini makubaliano ambapo imeahidi kuleta vifaa  kwa kuunga mkono juhudi hizo ambapo hivi sasa wako katika mchakato wa kuangalia vifaa vinavyohitajika.

Imetayarishwa na Kitengo cha Mawasiliano

Ikulu Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.