Afisa Habari kutoka mfuko wa Hifadhi ya Jamii (ZSSF) Mussa Yussuf akizungumza katika mkutano wa Maafisa Habari na Mawasiliano wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar huko Ukumbiwa Sheikh Idrisa Badul-wakil Kikwajuni.
PICHA NA FAUZIA MUSSA- MAELEZO ZANZIBAR.
Na Mwashungi Tahir Maelezo
Maafisa Habari nchini wametakiwa kutumia ujuzi walionao ili kuwapatia taarifa wananchi juu ya utekelezaji wa mipango ya serikali, mafanikio pamoja na changamoto zake.
Wito huo umetolewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya habari, vijana,utamaduni na Michezo Fatma Hamad Rajab kwa niaba ya Waziri wa habari wakati alipokuwa akizungumza katika mkutano wa Maafisa wa Habari na mawasiliano wa Serikali huko Ukumbi wa Sheikh Idriss Abdul Wakil, Kikwajuni.
Amesema ana matarajio makubwa baada ya mkutano huo kuwa, utoaji wa taarifa juu ya shughuli za serikali ya awamu ya nane utaimarika ili kila mwananchi ajue yanayofanywa na serikali.
Katibu huyo amesema Rais wa Zanzibar Dk. Mwinyi amekuwa akihimiza kila siku wananchi kupatiwa taarifa zinazofanywa na Serikali kutokana na umuhimu wa habari katika maendeleo ya nchi.
Kutokana na hali hiyo Katibu huyo amesema kwa Wizara yake kupitia Idara ya habari Maelezo itafanya uhakiki wa maafisa hao jinsi wanavyofanya kazi katika taasisi zao.
Amefahamisha kuwa Afisa husika atakaeshindwa kutekeleza vyema majukumu yake bila ya kujali taasisi anayofanyia kazi Wizara ya habari itapendekeza kwa Idara ya Utumishi kupatiwa kazi nyengine.
“Kuanzia sasa tutaendelea kuwafuatilia Maafisa habari wote kuhusu utendaji kazi zao, afisa yeyote atakayeshindwa kutekeleza vyema majuku tutaiomba Utumishi impatie kazi nyingine” Alisema Katibu huyo kwa niaba ya Waziri.
Awali akimkaribisha mgeni Rasmi, Mkurugenzi wa Habari Maelezo Zanzibar Hassan Khatib amesema tayari Wizara kupitia Idara ya Habari Maelezo imeshakamilisha muundo wa Utumishi wa Kada ambapo baada ya kuupitia utawasilishwa utumishi kwa ajili ya hatua muafaka.
Amesema Serikali imeamua kuitambua rasmin kada ya habari na mawasiliano ambapo muongozo umetolewa kwa Idara ya Habari Maelezo kuwaratibu maafisa wa habari na mawasiliano wote wa Serikali ili kuwatambua na kuwafanyia tathmini ya utendaji wao.
No comments:
Post a Comment