Habari za Punde

Zanzibar imekuwa ni nchi ya kwanza Afrika kutumia teknolojia ya mashine ya kupimia UVIKO 19 (EDE Covid Scanners)

 

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akizungumza na Waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali vya Kitaifa na Kimataifa, mazungumzo hayo yamefanyika katika ukumbi wa Ikulu Jijini Zanzibar, wakiwa Zanzibar kutembelea Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume Zanzibar kushuhudia uzinduzi wa matumizi ya  Mashine ya (EDE) ya kupimia UVIKO-19, pamoja na kuwasili kwa Ndege ya “Fly Dubai” kutoka (UAE).

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema kuwa Zanzibar imekuwa ni nchi ya kwanza Afrika kutumia teknolojia ya mashine ya kupimia UVIKO 19 (EDE Covid Scanners) kutokana na azma yake ya kuimarisha sekta ya utalii ambayo ndio tegemeo kubwa la uchumi wa Zanzibar.

Rais Dk. Mwinyi aliyasema hayo leo wakati akifanya mahojiano na waandishi wa habari wa Kitaifa na Kimataifa kufuatia matukio mawili makubwa yaliyotokea leo hapa nchini katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume likiwemo kuanza tena kwa safari za ndege ya ‘Fly Dubai’ kutoka Umoja wa Nchi za Kiarabu (UAE), pamoja na uzinduzi wa matumizi ya mashine ya (EDE Covid Scanners) ya kupimia UVIKO 19.

Alisem kuwa hatua hiyo itapunguza matatizo ambayo wasafiri wanayapata na kusisitiza kwamba ni muhimu Serikali kufanya kila juhudia katika kurudisha watalii hapa Zanzibar ambapo ndege ya ‘Fly Dubai’ itakuwa inakuja mara mbili kwa siku na sio muda mrefu ndege za Shirika la ndege la ETIHAD itaanza safari zake hapa Zanzibar.

Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeona umuhimu wa kutumia teknolojia hiyo ya mashine ya (EDE Covid Scanners) kutokana na utegemezi mkubwa wa sekta ya utalii katika uchumi wake ambapo inakisiwa kwamba asilimia 30 ya pato la taifa linategemea sekta hiyo.

Aliongeza kuwa huduma ya kupima UVIKO 19 kwa kutumia teknolojia ya mashine ya (EDE Covid Scanners) italeta unafuu mkubwa kwa wageni wanaotumia uwanja wa ndenge wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume Zanzibar wakiwemo wale wanaotumia mashirika hayo ya ndege kutoka (UAE) kwa lengo la kurahisisha safari zao.

Alieleza kwamba mashine hiyo ambayo ni msada kutoka Abu Dhabi itasaidia kwa kiasi kikubwa kufikia lengo lililokusudiwa sambamba na matumizi yake kutokuwa na ulazimu wa kupimwa kupitia puani ama mdomoni na badala yake kutatumika teknolojia hiyo ya kutumia mashine hiyo ambayo itakuwepo katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume Zanzibar.

Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa Upimaji wa UVIKO 19 umerahishwa ambapo mgeni anaweza kupima katika hoteli aliyofikia, anaweza akaenda mwenye katika kituo na kupima na kupata matokeo kwa wakati ambapo pia, anaweza kupata huduma hiyo katika uwanja wa ndege hata masaa mawili kabla ya kusafiri.

Alisema kuwa ni matumaini ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwamba hatua hiyo itarahisisha usafiri na kuendelea kuleta watalii wengi hapa Zanzibar ambapo tayari ukurasa mpya umeanza kwa ndege za ‘Fly Dubai’ kutua hapa Zanzibar na si muda mrefu ndege za Shirika la ndege la ETIHAD nazo zitaanza kutua.

Alisema kuwa Zanzibar inahitaji watalii na itafanya kila linalowezekana katika kuhakikisha juhudi za makusudi zinachukuliwa ili idadi ya watalii iweze kuongezeka kwa azma ile ile ya kuongeza pato la taifa.

Imetayarishwa na Kitengo cha Mawasiliano

Ikulu Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.