Habari za Punde

Mchezo wa Soka Unafursa Kubwa katika Ujenzi wa Uchumi wa Taifa

Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Mhe. Lela Mohamed Mussa (kulia) akizindua Kongamano la Mpira wa Miguu Tanzania (TFS) litakalofanyika Juni 25-26, 2022 Zanzibar. Kushoto ni Katibu wa Kamati ya Maalum ya Maandalizi ya kongamano hilo ambaye pia Afisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Afrisoccer inajishughulisha na shunghuli za Michezo Bw. Peter Simon.

Na Eleuteri Mangi-WUSM, Zanzibar

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo Bw. Saidi Yakubu amesema mchezo wa soka unafursa kubwa katika ujenzi wa uchumi wa taifa ambao unamchango mkubwa kwenye mapato ya Serikali kupitia kupitia ligi mbalimbali zinazoendeshwa nchini.

Naibu Katibu Mkuu Yakubu amesema hayo Februari 27, 2022 wakati wa uzinduzi wa Kongamano la Mpira wa Miguu Tanzania (TFS) ambapo Mgeni rasmi alikuwa Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Mhe. Lela Mohamed Mussa.

Akipokea taarifa ya kongamano la mwaka 2021, Naibu Katibu Mkuu Yakubu amesema wataifanyia kazi taarifa hiyo na kuahidi kuyafanyia kazi maazimio ya mwaka jana na kuwapongeza waandaji wa kongamano kwa kuendelea kuunga mkono juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya Rais Dkt. Hussein Ali Mwinyi inayojali michezo katika kujenga uchumi na kuwapongeza Kamati maalumu ya inayoandaa kongamano la mwezi Juni 2022 ambapo tayari mada zake zimeandaliwa kwa wakati.

Akitolea mfano namna michezo inavyochangia kukuza uchumi wa nchi, Naibu Katibu Mkuu Yakubu amesema ligi ya mpira wa miguu ya Uingereza imekuwa mfano wa kuigwa kwa kutoa mchango mkubwa kwenye uchumi wa nchi hiyo kwa Paundi bilioni 7.6 na kuchangia kodi kutoka kwa wanamichezo takribani Paundi bilioni 3.6 ambazo ni sawa kiasi cha Sh. trilioni 18 za Tanzania.

Ameongeza kuwa utalii wa kimichezo umekuwa kiungo muhimu katika nchi ambayo inalenga kuendesha michezo kisayansi na kusema Zanzibar maeneo mazuri ya kuwekeza kwenye sekta ya michezo yapo ikiwemo fukwe na bahari ambazo ni chanzo cha vivutio vya watalii na kutolea mfano nchi ya Uingereza ambayo imekuwa na jumla ya watalii wa kimichezo wapatao 1,180,000 ambapo watalii wa ndani ya nchi hiyo ni 652,000 na watalii 528,000 kutoka nje ya nchi hiyo..

Akizindua kongamano la mwaka 2022 ambalo linatarajiwa kufanyika Juni 25-26, 2022 visiwani Zanzibar, Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Mhe. Lela Mohamed Mussa amesema lengo la Serikali zote mbili ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ni kuboresha michezo na kutumia watu maarufu duniani ili kutangaza nchi kimataifa.

“Kufanyika kwa kongamano hili mwezi Juni hapa Zanzibar, tunatarajia kutatumia watu mbalimbali maarufu duniani ambao watakuwa chachu ya kutangaza utalii wa kimichezo nchini. Huu ni wakati mwafaka wa kutangaza vyakula vyetu vya hapa, nataka wakati wa kongamano wageni wetu wale vyakula vyetu vinavyotokana na bahari, wale samaki wa hapa kwetu” amesema Waziri Mhe. Lela.

Waziri Mhe. Lela ameongeza kuwa kongamano la TFS limekuja muda mwafaka likiongozwa na kaulimbiu ya mwaka huu inayosema “Maendeleo ya Mpira wa Miguu kwa Uchumi wa Buluu” kuwa ni hatua ya kuunga mkono sera ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ya Awamu wa Nane chini ya Rais wa Zanzibar Dkt. Hussein Ali Mwinyi inayolenga katika matumizi endelevu ya rasimali za bahari katika kuleta maendeleo kwa wananchi wa Zanzibar.

Kwa upande wake Katibu wa Kamati ya Maalum ya Maandalizi ya kongamano hilo ambaye pia Afisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Afrisoccer inajishughulisha na shunghuli za Michezo Bw. Peter Simon amesema walengwa wakuu wa kongamano hilo ni wadau mbalimbali wa mpira ikiwemo Serikali, wasimamizi wa mpira wa Miguu ikiwemo Shirikisho la Mpira, vilabu, Makocha, wachezaji wa zamani, wawekezaji, makampuni binafsi, mawakala, waandishi wa habari na wapenzi na mashabiki wa mpira wa miguu.

Kongamano la mwaka huu linatarajiwa kuwa na mada sita ambazo zitajadiliwa ikiwemo Nafasi za Uwekezaji katika Mpira wa Miguu, Uongozi na Usimamizi wa Mpira wa Miguu, Utalii wa Michezo, Sheria za Michezo, Mpira wa Miguu katika janga la Uviko 19, Matumizi ya Mpira wa Miguu katika kutatua changamoto mbalimbali za Kijamii. na kusistiza maazimio yatakayotokana na majadiliano hayo yatawasilishwa katika ngazi mbalimbali za maamuzi ili kusaidia katika kutunga wa sera na miongozo mbalimbali.

Kongamano la kwanza lililofanyika mwaka jana jijini Dar es Salaam huku washiriki wake wakitoka mataifa zaidi ya kumi ikiwemo Ufaransa, Ubeligiji, Ujerumani, Afrika Kusini, Uganda, Misri, Israeli, Senegali na Cameroon na kutibu kiu na matarajio ya malengo ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ambapo Uchumi wa Buluu umejikita kuwatumia pia watu maarufu duniani kutangaza fursa za kiuchumi zilizopo Visiwani humo.

Katika kongamano la mwaka huu linatarajiwa kuhudhuriwa kuwa na washiriki zaidi ya 500 kutoka ndani na nje ya nchi wakati mwaka 2021 kongamano hilo lilihudhuriwa na washiriki zaidi ya 150 na kuwavutia wachezaji magwiji wa soka waliotamba barani Afrika na duniani ambao pia wanatarajiwa kushiriki kongamano la mwaka huu ambao ni Khalilou Fadiga, mchezaji wa zamani wa timu ya taifa ya Senegal na vilabu mbalimbali vikiwemo PSG na Bolton Wanderers pamoja na nyota wa zamani wa timu ya taifa ya Cameroon Patrick Mboma ambaye pia alicheza katika vilabu kama vile PSG na Parma.

Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Mhe. Lela Mohamed Mussa (kulia) akizindua Kongamano la Mpira wa Miguu Tanzania (TFS) litakalofanyika Juni 25-26, 2022 Zanzibar. Kushoto ni Katibu wa Kamati ya Maalum ya Maandalizi ya kongamano hilo ambaye pia Afisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Afrisoccer inajishughulisha na shunghuli za Michezo Bw. Peter Simon.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo Bw. Saidi Yakubu (kushoto) akipokea taarifa ya kongamano la mwaka 2021 wakati wa uzinduzi wa Kongamano la Mpira wa Miguu Tanzania (TFS)  Februari 27, 2022 Zanzibar. Kulia nia Mkurugenzi wa Uratibu na Maendeleo ya Uchumi wa Buluu Kapteni Hamad Bakar Hamad.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo Bw. Saidi Yakubu akiongea na wajumbe pamoja na waandishi wa habari (hawapo pichani) wakati wa uzinduzi wa Kongamano la Mpira wa Miguu Tanzania (TFS) Februari 27, 2022 Zanzibar.

Mwenyekiti wa bodi Ushauri ya Kongamano la Mpira wa Miguu Tanzania (TFS) Bi. Nassra Juma Mohamed ambaye pia ni Naibu Kamishna wa Uhamiaji Zanzibar akiongea na wajumbe bodi hiyo pamoja na waandishi wa habari (hawapo pichani) wakati wa uzinduzi wa wa kongamano la TFS
Katibu wa Kamati ya Maalum ya Maandalizi ya kongamano hilo ambaye pia Afisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Afrisoccer inajishughulisha na shunghuli za Michezo Bw. Peter Simon akitoa taarifa kuhusu Kongamano la Mpira wa Miguu Tanzania (TFS) kwa wajumbe bodi hiyo pamoja na waandishi wa habari (hawapo pichani) wakati wa uzinduzi wa kongamano la TFS 

Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Mhe. Lela Mohamed Mussa (wa tatu kulia mstari wa mbele) akiwa katika picha ya pamoja na Kamati maalumu ya kuandaa Kongamano la Mpira wa Miguu Tanzania (TFS) litakalofanyika Juni 25-26, 2022 Zanzibar.  Wa tatu kulia mstari wa mbele ni Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo Bw. Saidi Yakubu.

 (Picha na Eleuteri Mangi-WUSM, Zanzibar)

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.