Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais-Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dkt. Lauren Ndumbaro akifungua kikao cha wadau cha kujumisha anuai za jamii katika TEHAMA kilichofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Uwanja wa Ndege leo tarehe 03 Machi, 2022 jijini Dodoma
Na Mwandishi Wetu, WHMTH, Dodoma
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imejipanga kiuhakikisha kuwa anuai za jamii zinajumuishwa kwenye TEHAMA ili kufikia Tanzania ya Kidijitali
Hayo yameelezwa na Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dkt. Laurian Ndumbaro wakati akifungua kikao cha wadau wa taasisi za Serikali na anuai za jamii ikiwemo watu wenye ulemavu, vijana, wazee na wanawake ili kuhakikisha kuwa anuai hizo za jamii zinajumuishwa kwenye TEHAMA (Teknolojia ya Habari na Mawasiliano) kupitia mradi wa Tanzania ya Kidijitali ili makundi hayo maalum yaweze kutumia na kunufaika na TEHAMA nchini. Kikao hicho kimefanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Uwanja wa Ndege, Dodoma.
Dkt. Ndumbaro amesema kutokana na mabadiliko ya TEHAMA duniani ambapo imepelekea huduma nyingi kutolewa kupitia TEHAMA, Serikali kupitia Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari itahakikisha kuwa huduma hizi zinatolewa na kumfikia kila mwanachi kwa wakati ili kutekeleza Sera ya Taifa ya TEHAMA ya mwaka 2016 kwa kutambua na kukusanya mahitaji ya anuai za jamii ili yajumuishwe kwenye TEHAMA.
Ameongeza kuwa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kwa kushikiana na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora inatekeleza mradi wa Tanzania ya Kidijitali kwa kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka 2021 hadi mwaka 2026 kwa lengo la kuboresha na kukuza maunganisho ya ndani na ya kimataifa ili kuweza kufikisha huduma za mawasiliano pamoja na utoaji wa huduma mbali mbali za Serikali kwa wananchi kidijitali.
“Lengo la Mradi huu ni kuboresha na kukuza maunganisho ya ndani na
ya kimataifa ili kuweza kufikisha huduma za mawasiliano pamoja na utoaji wa
huduma mbalimbali za Serikali kwa wananchi kwa kujenga vituo vya ubunifu vya TEHAMA
ili kuboresha ubunifu kwa kupitia na kuhuisha sera na sheria mbalimbali ili
kuweka mazingira wezeshi ya utekelezaji na uendelezaji wa Sekta ya Mawasiliano
pamoja na kuwajengea uwezo wataalam wa TEHAMA nchini” amesema Dkt. Ndumbaro.
Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Watu Wenye Walemavu Tanzania
(SHIVYAWATA), Ernest Kimaya ameishukuru Serikali kwa kuwaalika na ameiomba
Serikali iangalie uwezekano wa kuongeza vifaa rafiki vya TEHAMA na matumizi
yake kwa wananchi hususani kwa anuai za jamii ikiwa ni pamoja na kushirikisha watendaji
wa anuai za jamii katika ngazi za kata hadi taifa na Ofisi ya Rais - TAMISEMI
itumike kufikisha na kutekeleza hili
Akizungumza kuwakilisha kundi la wajasiriamali nchini, Mwenyekiti wa Wamachinga
wa Mkoa wa Dodoma, Bruno Mponzi amesema kuwa mradi wa Tanzania ya Kidijitali ni
chachu kwao kwa kuwa utarahisisha shughuli zao na kuwawezesha kufanya biashara
mtandao kwa kuwa wana umoja unaowaunganisha wamachinga wote na kusajiliwa
kwenye kanzi data ambayo inarahisisha mawasiliano baina yao na Serikali.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari,
Dkt. Jim Yonazi wakati akifunga kikao hicho amesema kuwa mabadiliko ya
teknolojia yanagusa maisha yetu ya kila siku katika nyanja za kiuchumi na
kijamii ambapo Serikali kwa kutambua hili imeweka sera, sheria, kanuni pamoja
na kujenga miundombinu ya TEHAMA, kutoa huduma za mawasiliano ili kuhakikisha
kuwa wananchi wote pamoja na anuai za jamii zinajumuishwa na kushirikishwa
katika TEHAMA ili kufikia Tanzania ya Kidijitali
“Kila mmoja wetu atekeleze maazimio mliyokubaliana kwa kuwa taifa hili
halina mtu mwingine wa kuliendeleza ila sisi ili taifa letu liweze kuwa mbele
na kunufaika na TEHAMA,” amesisitiza Dkt. Yonazi
Naye Mwenyekiti wa Wazee Mkoa wa Dodoma, Mchungaji Petro Mpolo ameishukuru
Serikali kwa kuwakumbuka wazee na kuwajumuisha kwa kuwa wakizungumza katika
jamii sauti zao zinasikika kwa kuwa wapo wazee wenye nguvu, utaalamu na
hawawezi kuwa nje ya mabadiliko ya teknolojia
Akitoa wasilisho kuhusu mradi wa Tanzania ya Kidijitali, Jumanne
Makumbato amesema kuwa mradi huu umejikita katika maeneo matatu ambayo ni
ikolojia ya kidijitali itakayohusisha kuweka mazingira wezeshaji na kuendeleza
ujenzi wa miundombinu ya TEHAMA; maunganisho ya kidijitali ambayo itajikita
kwenye upatikanaji wa mawasiliano ndani ya Serikali na kufikisha mawasiliano
yenye kasi vijijini kwa maendeleo ya wananchi; pamoja na jukwaa la huduma za
kidijitali ambapo eneo hili litahusika na mifumo, huduma, miundombinu ya
kuhifadhi data, kujenga uelewa na uwezo wa wananchi katika masuala ya
kidijitali
Imetolewa na
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini,
Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari.
Katibu Mkuu wa
Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt Jim Yonazi
akizungumza wakati akifunga kikao cha wadau cha kujumjuisha anuai za jamaii
katika TEHAMA kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Uwanja wa Ndege leo
tarehe 03 Machi, 2022 jijini Dodoma.
Mkurugenzi wa
Rasilimali Watu na Utawala wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya
Habari, Teddy Njau (kushoto) akimuelekeza jambo Mkurugenzi Msaidizi wa
Miundombinu ya TEHAMA wa Wizara hiyo, Mhandisi Nikusubila Maiko (kulia) wakati
wa kikao cha kujumjuisha anuai za jamii katika TEHAMA kilichofanyika kwenye ukumbi
wa mikutano wa Uwanja wa Ndege leo tarehe 03 Machi, 2022 jijini Dodoma.
Katibu Mkuu wa
Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dkt. Lauren Ndumbaro
(kushoto) akisikiliza uwasilishaji wa mada kuhusu mradi wa Tanzania ya
Kidijitali kwenye kikao cha wadau cha kujumuisha anuai za jamii kilichofanyika kwenye
ukumbi wa mikutano wa Uwanja wa Ndege leo tarehe 03 Machi, 2022 jijini Dodoma.
Kulia ni Mkurugenzi Idara ya Uendelezaji wa Ofisi hiyo, Agnes Meena.
Mwakilishi wa
Wanawake wa Mkoa wa Dodoma, Mwajuma Nyambo akizungumza katika kikao cha wadau
cha kujumisha anuai za jamii katika TEHAMA kilichofanyika kwenye ukumbi wa
mikutano wa Uwanja wa Ndege leo tarehe 03 Machi, 2022 jijini Dodoma. Wa kwanza kulia
ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt
Jim Yonazi.
Mwenyekiti wa
Wamachinga Mkoa wa Dodoma, Bruno Mponzi akizungumza katika kikao cha wadau cha kujumuisha
anuai za jamii kwenye TEHAMA kilichofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Uwanja
wa Ngege leo tarehe 03 Machi, 2022 jijini Dodoma. Wa kwanza kulia ni Katibu
Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Jim Yonazi.
No comments:
Post a Comment