Habari za Punde

Makamu wa Rais Mhe.Dkt.Philip Mpango Akizungumza na Mkurugenzi wa UNEP

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango akifanya mazungumzo na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mazingira (UNEP) Bi.Inger Anderson. Mazungumzo yaliofanyika makao makuu ya UNEP Nairobi nchini Kenya. Machi 3,2022.


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango akiwa katika picha ya pamoja  na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mazingira (UNEP) Bi.Inger Anderson mara baada ya kumalizika kwa  Mazungumzo yao yaliofanyika makao makuu ya UNEP Nairobi nchini Kenya. Machi 3,2022.

 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango leo tarehe 3 Machi, 2022 ameshiriki katika mkutano maalum wa kuadhimisha miaka hamsini ya Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP) uliofanyika katika makao makuu yake Jijini Nairobi nchini Kenya.

Akiwasilisha salamu za Mheshimiwa Rais, Samia Suluhu Hassan, Dkt. Mpango amesema kuwa Tanzania inayofuraha kushiriki maadhimisho hayo na kwamba Tanzania inawahakikishia utekelezaji pamoja na  kuiunga mkono UNEP majukumu yake katika kuifanya dunia kuwa salama kwa wote.

Makamu wa Rais amesema kuwa Tanzania inathamini juhudi ya Shirika la Mazingira Duniani kuwa mstari wa mbele katika kutetea mabadiliko ya tabia nchi, kupotea kwa bioanuai, pamoja na uchafuzi wa mazingira. Amesema kuwa Shirika la Mazingira Duniani UNEP, limeonesha uongozi madhubuti kwa kushirikisha wajumbe katika kukabiliana na masuala ya mazingira.

Amesema unahitajika  ushirikiano wa pamoja hususan katika sekta ya teknolojia ili kupunguza gharama za nishati mbadala pamoja na kulinda vyanzo vya maji. Makamu wa Rais amesisitiza kwamba suala la utunzaji mazingira linapaswa kupewa kipaumbele ili kuwa na dunia salama kwa vizazi vya sasa na vijavyo.

Aidha Makamu wa Rais amesema Tanzania imekua ikifanya jitihada za kukabiliana na uchafuzi wa mazingira unaotokana na taka za plastiki na tayari ilifanikiwa kupiga marufuku matumizi ya plastiki zinazotumika mara moja tangu 2019. Amesema juhudi za pamoja zinahitajika katika kukabiliana na  taka ngumu, taka uoevu  na uchafuzi wa mazingira wa mazingira kwa ujumla hususani kupitia taka za plastiki.

Aidha, Dkt. Mpango amesema kuwa Tanzania ipo mstari wa mbele katika uhifadhi wa mazingira ikiwemo kuanzisha kampeni ya kupanda miti nchi nzima, utunzaji wa bioanuai, kuhamasisha matumizi ya nishati mbadala, pamoja na utunzaji wa vyanzo vya maji.

Katika hatua nyingine Makamu wa Rais amekutana na kufanya mazungumzo na mkurugenzi mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mazingira Inger Anderson. Makamu wa Rais amelishukuru shirika hilo kwa kuendelea kufadhili miradi mbalimbali nchini Tanzania yenye lengo la kupambana na uharibifu wa mazingira.

Makamu wa Rais amesema kutokana na changamoto za mazingira bado Tanzania inahitaji msaada wa shirika hilo hasa katika kuwezesha tafiti zitakazotoa njia za kukabiliana na uharibifu wa vyanzo vya maji. Aidha amesema kutoka na ukataji miti kwaajili ya nishati, Tanzania inakaribisha teknolojia rafiki pamoja na nishati mbadala nafuu kwa manufaa ya wananchi wa Tanzania pamoja na kulinda mazingira.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa UNEP Bi. Inger Anderson ameipongeza Tanzania katika jitihada zake za uhifadhi wa mazingira pamoja na ushiriki wa ujumbe wa Tanzania katika mkutano wa baraza la kimataifa la mazingira uliofanyika Nairobi. Amesema UNEP imefurahishwa na uwepo wa sera ya taifa ya mazingira ambayo inalenga kupambana na changamoto za uharibifu wa mazingira.

Bi Inger ameongza kwamba UNEP itaendelea kuunga mkono Tanzania katika juhudi hizo za uhifadhi wa mazingira ikiwemo kupambana na taka za plastiki ambazo zimekua tishio la mazingira duniani.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.