Na Meleka Kulwa -Dodoma
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amemteua Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kwa mujibu wa hati iliyowasilishwa leo tarehe 13 Novemba 2025 Bungeni Jijini Dodoma na Mpambe na Mshauri wa Masuala ya Kijeshi wa Rais, Brigedia Jenerali Nyamburi Mashauri, jina la Dkt. Mwigulu Nchemba lilikuwa ndani ya bahasha maalum iliyofunguliwa na Spika wa Bunge, Mhe. Mussa Azzan Zungu. Spika alilisoma jina hilo mbele ya wabunge na kueleza kuwa Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, Mbunge wa Jimbo la Iramba Magharibi, ndiye aliyependekezwa na Rais kushika wadhifa huo.
Dkt. Mwigulu Nchemba ambaye alikuwa Waziri wa Fedha katika awamu iliyopita, anatarajiwa kupigiwa kura na wabunge kwa Azimio litakalopitishwa na Bunge ili kuthibitishwa rasmi kuwa Waziri Mkuu.
Iwapo atapigiwa kura za ndiyo, Dkt. Mwigulu Nchemba atamrithi Mhe. Kassim Majaliwa, ambaye muda wake wa miaka 10 kuhudumu katika nafasi hiyo umemalizika.


No comments:
Post a Comment