Habari za Punde

SERIKALI KUPONGEZA HATUA ZA MAPAMBANO DHIDI YA UKIMWI

 

Waziri wa Nchi Ofisi ya waziri Mkuu, (Sera Bunge na Uratibu) Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana akizungumza na WAVIU Mkoani  Njombe.

Na Mwandishi wetu- Dodoma

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera Bunge na Uratibu ) Mhe. Balozi  Pindi Chana amepongeza Mkoa wa Njombe kwa jitihada za kupunguza viwango vya maambukizi ya Virusi vya Ukimwi.

Waziri Pindi amesema hayo katika ziara yake Mkoani Njombe alipopokea taarifa ya Mkoa  kuhusu utekelezaji wa shughuli za UKIMWI na baadaye kutembelea vikundi vya wajasiriamali vya WAVIU, pamoja na kukagua ujenzi wa Kituo cha Care Treatment Centre (CTC), katika  Halmashauri ya Mji wa Makambako mkoani hapo..

Mhe. Pindi alisema licha ya kupungua kwa maambukizi hayo bado ipo haja ya kuendelea kutoa elimu kwa wananchi ili kudhibiti maambukizi mapya na wananchi kuwa katika hali ya usalama na afya bora.

“Nipongeze hatua hii kubwa mliyopiga kama Mkoa lakini tuna jukumu la kuendelea kupunguza viwango hivi na kama Serikali tumefanikiwa kupunguza maambukizi ya virusi vya ukimwi kwa kina mama pia maambukizi ya virusi vya UKIMWI kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto,” alisema Mhe. Pindi.

Vile vile alibainisha kwamba katika kuhakikisha vikundi vya ujasiriamali vya WAVIU vinaimarika kiuchumi kupitia shughuli mbalimbali wanazozifanya kuendesha maisha na kupata huduma muhimu serikali imetenga 10% kwa ajili ya Vijana, wanawake na watu wenye ulemavu kupata mikopo itakayowawezesha kuboresha shughul zao.

“Mashirikiano ya Serikali za mitaa na vikundi vya wajasiriamali  ni imara sana na niwasisitize mtumie fursa hii ya mikopo ambayo inatolewa na serikali yetu lengo ni kuhakikisha hakuna mwananchi anayeachwa nyuma katika maendeleo na mtapata na elimu ya matumizi sahihi ya hiyo mikopo na ujasirimali,” alieleza Mhe. Pindi.

Aidha alihimiza ushirikiano baina ya vikundi vya ujasirimali kushirkiana na serikali za mitaa katika maneo yao  ili  kupata taarifa za fursa mbalimbali pindi zinapojitokeza  katika maeneo yao huku akisisitiza WAVIU kujiunga katika  vikundi na kuendelea kuchapa kazi kwa manufaa yao na kuinua pato la Taifa.

Katika hatua nyingine  Balozi  Pindi alitoa wito kwa wananchi kutumia kituo kinachotoa huduma za afya cha  Care Treatment Centre (CTC) kujua hali ya afya zao akisema kuwa suala la  kujua hali  ya kiafya hususani  VVU ni jambo la msingi.

Naye Mkurugenzi wa Tume ya kudhibiti UKIMWI Tanzania ( TACAIDS), Dkt. Leonard Maboko alisema mradi wa Southern Afrika Trade and Transportation Facilitation Project umehusisha ujenzi na ukarabati wa kituo hicho, maabara ya kupima virusi vya ukimwi, kutoa mashine za kupima virusi vya ukimwi na vichomea taka.

“Ujenzi huu pia umehusisha  ujenzi wa vituo 20 katika barabara kuu kutoka  Dar es salaam kuelekea mpaka wa Tunduma na Kasumulu  kwa ufadhili wa World Bank kwa sababu ndio mwingiliano wa Tanzania na Nchi za Jangwa la Sahara ambazo kiwango cha maambukizi kiko juu  na vituo hivi vimejengwa katika vituo vya afya na vitakuwa chini ya Halmashauri. ,”alifafanua Dkt. Maboko.

Akitaja mikoa mingine ambayo vituo hivyo vinajengwa ni pamoja na Mkoa wa Pwani wenye vituo vitano vya CTC, Mkoa wa Morogoro  vituo vitatu ,Mkoa wa Iringa vituo vinne, Mkoa wa Njombe  wenye  kituo kimoj pamoja na  Mkoa wa Mbeya wenye  vituo vitano na Mkoa wa Songwe  vituo viwili.

Akitoa neno la shukrani Mwenyekiti wa Jukwaa la Watu Wanaoishi na Virusi vya UKIMWI Bi, Joseline Mtono ameishukuru Serikali na wadau mbalimbali wa maendeleo kwa kuendelea kushirikiana na kuwajali watu wanaoishi na virusi vya UKIMWI hali inayowafanya kujisikia nao ni sehemu ya jamii.

Mkurugenzi wa Tume ya kudhibiti UKIMWI  Dkt. Leonard Maboko akitoa Salamu katika Mkutano wa Nchi WAVIU Mkoani Njombe.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera Bunge na Uratibu) Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana akipata maelezo ya bidhaa zinazozalishwa na vikundi vya WAVIU Mkoani Njombe.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera Bunge na Uratibu) Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana akiangalia Mradi wa kuku wa mayai alipotembelea kikundi cha WAVIU cha Juhudi Mkoani Njombe.

 PICHA KUTOKA OFISI YA WAZIRI MKUU.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.