Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe.Othman Masoud Othman akizungumza wakati wa mkutano wa Maadhimisho ya Siku ya Magonjwa Adimu Duniani, akimuwakilisha Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dk.Hussein Ali Mwinyi amesema Serikali itahakikisha kuwepo sera na sheria madhubuti zitakazorahisisha utekelezaji wa mipango ya nchi kwa ufanisi na kukidhi matarajio, ili kuongeza kasi katika kuzikabili athari za magonjwa adimu.
Rais Dk. Mwinyi ameyasema hayo leo, kupitia Hotuba yake iliyosomwa na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Othman Masoud, katika Maadhimisho ya Siku ya Magonjwa Adimu Duniani, iliyofanyika katika Hoteli ya Golden Tulip, Uwanja wa Ndege, Jijini hapa.
Mheshimiwa Rais amewahakikishia wananchi kwamba, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya Awamu ya Nane, itahakikisha inaweka kipaumbele na umuhimu unaostahiki katika kupambana na kuyashughulikia Magonjwa adimu, pamoja na kuwapatia huduma bora wagonjwa wanasumbuliwa na maradhi hayo.
Amesema kuwa Serikali itaendelea kutafuta rasilimali fedha na nyenzo nyengine muhimu kwa ajili ya kuyashughulikia magonjwa adimu yanayowasibu wananchi, huku akihamasisha umuhimu wa kutoa elimu na mafunzo kwa wafanyakazi na kununua vifaa tiba vinavyohitajika, ili kuongeza ufahamu wa maradhi hayo kwa jamii.
“Ili tuweze kupiga hatua za haraka katika juhudi zetu za kutafuta maendeleo, lazima kuwepo na ushirikiano mzuri baina ya Serikali, sekta binafsi, asasi za kiraia pamoja na wananchi wenyewe; maandalizi ya maadhimisho haya ni mfano mzuri wa ushirikiano ambao nimekuwa nikiuhimiza katika ujenzi wa nchi yetu; ni matumaini yangu kuwa asasi nyengine za kiraia zitajifunza kutokana na mfano huu”, amesema Mheshimiwa Dk.Mwinyi.
Akisisitiza juu ya utoaji wa huduma bora za afya kwa wananchi, Mheshimiwa Rais ameeleza kuwa kunahitajika uwepo wa watendaji walio tayari kufanyakazi, miundombinu imara pamoja na vifaa tiba vya kisasa, akitamka kwamba msingi wa yote hayo ni uimara na utayari wa watendaji, huku akiwahimiza madaktari, wauguzi, wataalamu, viongozi na wafanyakazi wote katika sekta ya afya kufanya-kazi kwa bidii, moyo wa uzalendo na kwa kuzingatia maadili ya kazi, na kwamba waendelee kuzingatia misingi ya uadilifu na huruma kwa wagonjwa, wakati ambapo anaendelea kukumbuka ahadi yake ya kuyatizama upya na kuyaimarisha maslahi yao.
Naye Waziri wa Afya, Ustawi wa Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto, Mheshimiwa Nassor Ahmed Mazrui amesema kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu watahakikisha hatua za pamoja zinachukuliwa, zikiwemo za sensa, tafiti na kuwatambua, ili kuweka mazingira bora kwa watu wanaoishi na magonjwa adimu, pamoja na kujenga Shule na vituo maalum vitakavyowapatia huduma zote muhimu zinazojumuisha makaazi.
Mheshimiwa Mazrui amebainisha kwamba uamuzi wa kuungana na wadau kutoka nchi mbali mbali kwa ajili ya kufanya maadhimisho haya kila mwaka ambapo mwaka huu ni mara ya tano kwa hapa Tanzania, tangu yalipoanza mwaka 2016, ni muhimu ikieleweka kwamba hatua hiyo ina mchango mkubwa katika kuongeza uelewa kwa jamii juu ya uwepo wa Magonjwa Adimu, sambamba na jitihada za kupambana nayo, kuondosha unyanyapaa, pamoja na kuondoa dhana na imani potofu zinazohusu matatizo hayo.
Kwa niaba ya watabibu, wahudumu na watu wanaosumbuliwa na magonjwa adimu, Mhadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA), Mwanzilishi wa Taasisi ya Magonjwa Adimu ya Ali Kimara (Ali Kimara Rare Diseases Foundation); na Rais wa Jumuiya ya Vinasaba vya Binaadamu Tanzania, Dr. Sanaa Said Suleiman; Bi Sharifa Mbarak; na Dokta Siana Nkya, wameeleza changamoto mbali mbali katika kuhudumia sekta hiyo ambazo ni pamoja na kukosekana kwa elimu ya kutosha, ukosefu wa wataalamu, vifaa tiba, gharama kubwa na ughali wa vipimo, na jamii kuhusisha baadhi ya maradhi hayo na masuala ya itikadi za mila potofu, hali inayodhoofisha na kuzorotesha juhudi za kutafuta tiba wakati muafaka na kwa kutumia njia sahihi.
Wameeleza kuwa baadhi ya magonjwa hayo, hasa kwa watoto, yanapelekea maisha yao kuwa hatarini kutokana na kukosa miongozo na maelekezo sahihi ya kitaalamu, huku wakiwanasihi wananchi, pale wanaposumbuliwa na maradhi yasiyo ya kawaida wasisite kutafuta ushauri kwa madaktari ili kuweza kujua chanzo na sababu halisi.
Viongozi mbali mbali, Watendaji, Wakurugenzi, Madaktari Bingwa, sambamba na Mkuu wa Wilaya ya Mjini, Ndugu Simai Msaraka, Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Bw. Ali Khamis Juma, Viongozi kutoka Taasisi ya Vinasaba vya Binaadamu Tanzania, Wanafunzi walioimba Wimbo Maalum kutoka Skuli ya Sekondari ya Ukongoroni, Wafadhili wa Huduma za Afya na Matibabu, kutoka ndani na nje ya Nchi, na baadhi ya watu wanaoishi na magonjwa adimu.
Kauli-mbiu ya Maadhimisho ya Mwaka huu, ambayo huadhimishwa kila ifikapo tarehe 28 Februari ni, USAWA KWA WAISHIO NA MAGONJWA ADIMU, “Equity for people living with a rare disease”.
Kwa mujibu wa takwimu za wataalamu, magonjwa adimu ni zaidi ya elfu sita (6000) duniani kote; yakiathiri takriban watu milioni 300 wenye umri na viwango tofauti, ambapo imeripotiwa kwamba takriban asilimia 70 ya maradhi hayo yanasababishwa na kasoro katika vinasaba, jambo mbalo linapelekea kwa baadhi yao kuwa ni vigumu kugundulika au kuyapatia tiba muafaka kwa njia za kawaida, na wakati unaostahiki, ikielezwa kuwa kundi lao kubwa ni watoto, ambao zaidi ya asilimia 30 hufariki dunia kabla ya kutimu umri wa miaka mitano (5), na ambapo pia athari zake ni kubwa zaidi katika nchi zinazoendelea ikiwa ni pamoja na Tanzania, ikiwemo Zanzibar.
No comments:
Post a Comment