Habari za Punde

Watendaji OMKR watakiwa kuwa wabunifu

Aliekuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais ambae kwa sasa ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Fedha na Mipango Mhe Dkt Saada Mkuya Salum na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Mhe Harusi Said Suleiman wakiweka saini hati za makabidhiano huku wakishuhudiwa na Katibu Mkuu Dkt Omar D. Shajak, hafla iliyofanyika  kwenye ukumbi wa mkutano Migombani

Aliekuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais ambae kwa sasa ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Fedha na Mipango Mhe Dkt Saada Mkuya Salum akimkabidhi vitendea kazi muhimu Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Mhe Harusi Said Suleiman huku wakishuhudiwa na Katibu Mkuu Dkt Omar D. Shajak na watendaji wengine, kwenye ukumbi wa mkutano Migombani
 
Na Raya Hamad, OMKR

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango Mhe. Dk. Saada Mkuya Salum, amewataka Watendaji  wa Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, Zanzibar kuendelea kuwa wabunifu ili kwenda sambamba na maono ya Serikali ya awamu ya nane ya kutimiza matarajio ya kuwatumikia vyema wananchi.

Dkt. Mkuya ameyasema hayo wakati wa makabidhiano ya ofisi baina yake na Waziri mpya wa Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Mhe, Harous Said Suleiman kufuatia mabadiliko ya Mawaziri  yaliyofanywa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Mwinyi hivi karibuni.

Amesema kwamba wananchi wanamatarajio makubwa ya Serikali ya awamu ya nane katika utekelezaji wa sera na mipango mbali mbali ya maendeleo na kwamba ni vyema wafanyakazi kujitahidi kwenda sambamba na matarajio hayo.

Hata hivyo, Dkt Saada amewakumbusha watendaji hao pia kujitahidi kuenda na muda kwa kuzingatia  wakati katika utekelezaji wa shughuli za kazi mbali mbali ili kumsaidia waziri Harusi kutimiza vyema majukumu yake.

Amehimiza wafanyakazi hao kumpa mashirikiano Waziri Harusi kama walivyompa yeye ili aweze kutumiza majukumu yake kwa wepesi na kuweza kupata mafanikio katika sekta zote mtambuka anazoziongoza ndani ya wizara hiyo.

Naye waziri mpya wa Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Mhe. Harusi Said Suleiman, amewaomba wafanyakazi hao kumpa mashirikiano katika kufanikisha utekelezaji wa shughuli za Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais na ujenzi wa nchi kwa jumla.

Aidha amewakumbusha watendaji hao umuhimu wa kuendelea kufanyakazi kwa mashirikiano na kuheshimu sheria na taratibu za kazi kama msingi wa mafanikio   kazini.

Bi Harusi amezitaka taasisi zote za ndani kuhakikisha kwamba zinatayarisha na kutekeleza mpango mkakati katika utekelezaji wa malengo ya taasizi husika.

Naye Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Dk. Omar D. Shajak, amemshukuru waziri aliyeondoka Mhe. Dkt Saada Mkuya kwa usimamizi bora kwa kipindi chote alichokuwepo kwa kutumia umahiri na maono mapana katika kusimamia sekta zilizopo ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais.

Dkt Shajak amesema kwamba katika kipindi kifupi alichoiingoza Ofisi hiyo usimamizi wake umeleta ufanisi kwa kutekeleza mambo mengi  likiwemo suala la mabadiliko ya sheria ya kupambana na dawa za kulevya Zanzibar. 

Makabidhiano hayo yamefanyika kwenye ukumbi wa mkutano wa Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Migombani


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.