Habari za Punde

Fursa ya Kujifunza Historia,Hekima na Uzalendo wa Mwasisi Huyo wa Mapinduzi

 

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk,.Hussein Ali Mwinyi akihutubia na kulifungua Kongamano la Nne la Kumbukizi ya Rais wa Kwanza na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Zanzibar Hayati Sheikh.Abeid Amani Karume, lililofanyika katika ukumbi wa Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere Kampasi ya Karume Zanzibar Bububu lililofanyika leo 5-4-2022.

UTARATIBU wa kuandaa Kongamano la kumkumbuka Rais wa Kwanza wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Hayati Sheikh Abeid Amani Karume ni fursa ya kujifunza historia, hekima na uzalendo wa mwasisi huyo wa Mapinduzi ili kizazi cha sasa kiweze kuhamasika kujitolea katika kuleta maendeleo ya nchi kama alivyofanya yeye.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi ameyasema hayo leo  katika hotuba yake ya uzinduzi wa Kongamano la nne la kumbukumbu ya Rais wa Kwanza wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Hayati Sheikh Abeid Amani Karume lililofanyika katika Chuo cha Mwalimu Nyerere, Kampasi ya Karume Bububu, Zanzibar.

Katika maelezo yake Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa imepita miaka 50 tokea kiongozi huyo aondoke duniani lakini kwa kuzingatia mchango wake mkubwa kwa maendeleo ya Zanzibar na Tanzania kwa ujumla ataendelea kuenziwa na kukumbukwa milele sambamba na kuyaenzi maono na fikra zake ili kuzidi kupiga hatua za maendeleo kama alivyodhamiria katika uhai wake.

“Tumamuombea dua, Mwenyezi Mungu ampe malazi mema peponi na waasisi wote wa Mapinduzi matukfu ya tarehe 12 Januari, 1964 ambayo ndiyo yaliyoleta uhuru wa Wazanzibari na mwanzo wa safari yetu ya maendeleo katika sekta zote hapa nchini”,alisema Dk. Mwinyi.

Aidha, Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa Sheikh Abeid Karume ataendelea kukumbukwa kutokana na jitihada zake, falsafa yake na kuenzi dhamira yake ya ukombozi kwa vitendo ili kuacha urithi bora wa uzalendo hasa kwa vijana ambao ndio walinzi na wajenzi wa Taifa hili.

Rais Dk. Mwinyi alitumia fursa hiyo kutoa pongezi kwa uongozi, wafanyakazi na wanachuo wa Chuo hicho cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere kwa kuona umuhimu wa kuandaa Kongamano hilo la kila mwaka kwa lengo la kuenzi mchango wa mwasisi huyo.

Pamoja na hayo, Rais Dk. Mwinyi alitoa wito kwa washiriki wote kuwa makini kusikiliza na hatimae kuweza kuchangia mada na kuwataka kutumia fursa hiyo kuwa jukwa muhimu la kujifunza mambo muhimu ya maendeleo ya nchi na kuhamasisha umoja wa Taifa hili.

Sambamba na hayo, Rais Dk. Mwinyi alikipongeza Chuo hicho kwa  kuona umuhimu wa kuwashirikisha wanafunzi katika jambo hilo ikiwemo uandishi wa Insha zinazomhusu Marehemu Mzee Karume.

Alisisitiza kwamba hatua ya kukutana katika kongamano hilo ni muhimu kwa lengo la kuenzi fikra za Jemedari wa Mapinduzi Mzee Abeid Karume hasa katika mwezi huu ambao Taifa linaadhimisha miaka 50 tokea kufariki kwa mwasisi huyo.

Pia, kongamano hilo ni muhimu katika kukumbusha wajibu wa kuwa wazalendo na kuwa tayari kuitumikia nchi na kufanya kazi mbali mbali za kujitolea alivyokuwa akifanya Marehemu Mzee Karume.

“Kupitia Kongamano hili tunapata wasaa wa kujikumbusha falsafa na hekima za Mzee wetu na kurithisha kwa vijana wetu ambao ndio tegemeo la nguvu kazi ya Taifa letu”,alisisitiza Rais Dk. Mwinyi.

Nae Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Ikulu, Jamal Kassim Ali kwa niaba ya Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali alieleza kwamba wakati umefika wa kuwepo kwa makavani ya Mzee Abeid Amani Karume ambayo yataweza kutoa tafsiri pana ya maisha ya kiongozi huyo na hatimae kuwasaidia vijana waliopo na watakaokuja hapo baadae.

Mapema Mwenyekiti wa Bodi ya Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, Stephen Wasira alisema kuwa chuo hicho kinakusudia kuwandaa vijana kwua viongozi ambapo shabaha yake kuu ni kutoa elimu huku akitumia fursa hiyo kumueleza Mzee Karume na umhimu wake ndani ya nchi hiii.

“Huwezi kuandika historia ya Zanzibar na Tanzania bila ya kumtaja Mzee Abeid Amani Karume”,alisema Wasira.

Aidha, Wasira alieleza kuwa Mapinduzi ni maendeleo na Mapinduzi ya Zanzibar ya Januari 12.1964 yamefanyika kwa ajili ya kuondoa dhulma na kusisistiza kwamba awamu zote zimetekeleza mawazo ya Mapinduzi na Awamu hii ya Nane nayo inaendeleza.

Mkuu wa Chuo Professa Shadrack Mwakalila alitumia fursa hiyo kutoa historia ya Chuo hicho tokea kuanzishwa kwakwe mnamo Julai 29.1961 na hatimae kurejeshwa Serikalini na kuwa Chuo cha Serikali ambacho kwa upande wa Zanzibar kilianza na wanafunzi 25 mnamo mwaka 2015 lakini hivi sasa kina wanafunzi zaidi ya 2300 ambacho kinatoa elimu katika program mbali mbali.

Alieleza azma yao ya kujenga Kampasi ya Chuo hicho huko Pemba ambapo tayari wameshakabidhiwa kiwanja huku wakiendelea na ujenzi wa mabweni katika Kampasi ya Bububu Unguja.

Profesa Mwakalila alieleza umuhimu wa Kongamano hilo ambalo lina kaulimbiu ya “Mchango wa Hayati Sheikh Abeid Amani Karume katika maendeleo ya elimu na uchumi wa Zanzibar”.

Katika uzinduzi huo wa Kongamano hilo, Rais Dk. Mwinyi alitunuku zawadi kwa washindi wa Insha Bora ambao ni wanafunzi sita watatu kutoka skuli za Msingi na watatu kutoka skuli za Sekondari za Unguja na Pemba.

Mapema baada ya kuwasili chuoni hapo Rais Dk. Mwinyi alipata fursa ya kukagua Bunifu mbali mbali za Wanafunzi wa chuo hicho hapo katika viwanja vya jengo la chuo hicho Bububu Zanzibar.

Mada ambazo zinatarajiwa kutolewakatika Kongamano hilo ni “Mchango wa Hayati Sheikh Abeid Amani Karume katika Maendeleo ya Elimu ya Zanzibar ya Leo” pamoja na mada isemayo “Mchango wa Hayati Sheikh Abeid Amani Karume katika Utekelezaji wa Uchumi wa Buluu Zanzibar”.

Imetayarishwa na Kitengo cha Habari

Ikulu Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.