Habari za Punde

Waziri Dkt.Khalid Ameridhishwa na Hatua Zinazochukuliwa na Watendaji wa Mamlaka ya Viwanja Vya Ndege.

Na.Kassim Abdi.

Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi Mhe.Dkt.Khalid Salum ameridhishwa na hatua zinazochukuliwa na watendaji wa Mamlaka ya viwanja vya ndege katika kuimarisha mazingira bora ya uwanja pamoja na mazingira ya utoaji wa huduma.

Waziri Dk. Khalid ameeleza hayo wakati akiwa katika muendelezo wa ziara zake pamoja na Naibu Waziri wa wizara hiyo ya kukagua na kutembelea maeneo mbali mbali kwa lengo la kuzitambua taasisi zinazounda Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi.

Amesema ameridhishwa na jitihada zinazochukuliwa na watendaji wa Mamlaka hasa katika harakati za Ujenzi katika kuipatia ufumbuzi changamoto ya kuondosha maji katika uwanja huo.

Waziri Dk. Khalid ameeleza kwamba pamoja na jitihada nzuri zinazochukuliwa na watendaji wa Mamlaka ya viwanja vya ndege lakini pia ameshauri kuchukuliwa kwa hatua za makusudi za kuhamishia shughuli za ushushaji wa abiria kwenye Jengo namba 3 la abiria  ili kuondosha changamoto ya msongamano kwenye Jengo nambari 2.

Pia, Katika ziara hiyo, viongozi hao walipata fursa ya kutembelea maeneo yalioanishwa kutumiwa na mamlaka ya viwanja vya ndege ambayo kwa sasa baadhi ya maeneo hayo yanakaliwa na wananchi.

Akizungumzia juu ya maeneo hayo Waziri Dk. Khalid ameleza kuwa, lengo la kufanya ziara katika maeneo hayo ni kuangalia hatua zinazoendelea ambapo amewataka wananchi kutokuwa na taharuki kwani Serikali inaendelea na mchakato wa mipango yake juu ya maeneo hayo na mara ya kukamilika kwa mipango hiyo wananchi watapewa taarifa kamili.

"Nawaomba wananchi wanaoishi katika maeneo ya karibu ambayo yamewekwa alama wasiwe na khofu kupitia ziara hii, kwani ziara hii hailengi kuchukua hatua yoyote". Alifafanunua Waziri Dk. Khalid

Katika hatua nyengine Mhe. Waziri amewashauri viongozi na watendaji wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege kuwa na mikakati ya muda mrefu inayofafanua dhamira na Dira ya mamlaka ili kutoa urahisi katika utekelezaji wake.

Nae, Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya viwanja vya Ndege Zanzibar Ndugu Seif Abdalla Juma amesema kupitia ziara ya viongozi hao wa Wizara Mamlaka hiyo itayafanyia kazi mapendekezo na maoni yote yaliotolewa ili kuufanya Uwanja wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume kuendelea kutoa huduma bora kitaifa na Kimataifa.

Ziara hizo za viongozi wa Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi zinalenga kuimarisha utendaji kazi wa Taasisi na Idara tofauti zilizomo ndani ya Wizara hiyo.

Kassim Abdi
Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi Zanzibar. 
05/04/2022.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.