Habari za Punde

Dk.Hussein Ameipongeza Azma ya Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) Kujenga Kampasi ya Chuo Zanzibar.

 

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akizungumza na Ujumbe wa Bodi ya Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) ukiongozwa na Mwenyekiti wa Bodi Prof.Wineaster Saria Anderson (kulia kwa Rais) walipofika Ikulu Jijini Zanzibar kwa mazungumzo yaliofanyika katika ukumbi wa Ikulu
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akizungumza na Mwenyekiti wa Bodi ya Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) Prof.Wineaster Saria Anderson alipofika Ikulu Jijini Zanzibar kwa mazungumzo yaliofanyika katika ukumbi wa Ikulu leo 6-4-2022

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi ameipongeza azma ya Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) ya kujenga Kampasi ya Chuo hicho hapa Zanzibar.

Rais Dk. Mwinyi aliyasema hayo leo Ikulu Zanzibar wakati alipofanya mazungumzo na uongozi wa Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) ulioongozwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Uongozi wa Chuo hicho Profesa Wineaster Sania Anderson.

Katika maelezo yake Rais Dk. Mwinyi aliueleza uongozi huo kwamba uwamuzi huo wa kujenga chuo cha elimu ya Biashra hapa Zanzibar utawasaidia kwa kiasi kikubwa wanafunzi wa Zanzibar ambao walikuwa wakifuata elimu hiyo huko Tanzania Bara.

Rais Dk. Mwinyi alieleza kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iko tayari kutoa ushirikiano mkubwa katika kuhakikisha chuo hicho kinajenga Kampasi yake hapa Zanzibar kwani uwamuzi huo ni mzuri na unahitaji ushirikiano.

Aidha, Rais Dk. Mwinyi alipongeza azma ya chuo hicho ya kutoa mafunzo hata kwa vijana walioishia Kidato cha Pili ambao wameshindwa kuendelea na elimu ya juu.

Aliongeza kuwa hatua hiyo ya kuwasomesha vijana walioishia Kidato cha Pili na kushindwa kuendelea na elimu ya juu ni miongoni mwa malengo na mikakati iliyowekwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Alieleza kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaendeleza mikakati yake ya kuimarisha elimu ya Vyuo vya Amali ili kuhakikisha vijana walioshindwa kuendelea na elimu ya juu nao wanapata elimu za stadi za maisha katika vyuo hivyo hapa Zanzibar.

Mapema Mwenyekiti wa Bodi ya Uongozi wa Chuo hicho Profesa Wineaster Sania Anderson alimueleza Rais Dk. Mwinyi azma ya chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) ya kujenga Kampasi yake hapa Zanzibar.

Katika maelezo yake Profesa Anderson alimueleza Rais Dk. Mwinyi kwamba tayari mchakato wa kupata eneo kwa ajili ya ujenzi wa chuo hicho umeshafanyika na kupongeza mashirikiano mazuri waliyoyapata kutoka Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Sambamba na hayo, Mwenyekiti huyo wa Bodi ya Uongozi wa Chuo cha CBE Professa Anderson alieleza hatua zitakazochukuliwa na uongozi huo kupitia Serikali kuu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika bajeti yake juu ya utaratibu wa kuanza ujenzi huo ambao utakuwa kwa awamu tatu na kutarajiwa kugharibu TZS Bilioni 10.12.

Pamoja na hayo, Mwenyekiti huyo wa Bodi ya CBE alieleza matarajio yake kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuunga mkono juhudi zao hizo kwa kutambua kwamba kumekuwa na mashirikiano mazuri kati ya Chuo hicho na Serikali kupitia Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali ya Zanzibar.

Aliongeza kuwa miongoni mwa wanafunzi watakao wachukua kwa ajili ya kujiunga na chuo hicho kitakapokuwa tayari kuanza mafunzo ni wale walioishia Kidato cha Pili na kushindwa kuendelea na elimu ya Juu ambao watawaanzisha elimu ya Cheti mpaka Digirii katika kada hiyo ya elimu ya Biashara.

Imetayarishwa na Kitengo cha Habari

Ikulu Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.