Habari za Punde

Ili Taifa Liwe na Amani ni Lazima Kuhakikisha kila Mwananchi Anapata Kaki zake za msingi.

 

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akihutubia katika hafla ya sherehe ya Jubilei ya Miaka 25 ya Uaskofu wa Muhashamu wa Jimbo Katoliki Zanzibar Askofu Agustino Mweleli Shao, iliyofanyika katika Uwanja wa Amaan Unguja Jijini Zanzibar leo 10-5-2022. 

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi  Dk. Hussein Ali Mwinyi alisema ili Taifa liwe na amani, ni lazima kuhakikisha kila mwananchi anapata haki zake za msingi.

Dk. Mwinyi amesema hayo katika sherehe za Jubilee ya miaka 25 ya Askofu Mhashamu Augustine Shao, iliofanyika katika Uwanja wa Amani, Jijini Zanzibar.

Amesema ili Taifa liwe na amani, ni vyema  likahakikisha kila mwananchi anapata haki zake za msingi, hivyo akaahidi kuzipatia ufumbuzi wa haraka  changamoto mbali mbali  zinazolikabili Kanisa.

Aliwataka viongozi wote wa Dini katika madhehebu tofauti  kuwa waadilifu kwa kigezo kuwa hatua hiyo itawaletea sifa, sambamba na kuwajengea imani waumini wao.

Akitoa ufafanuzi  juu ya sera ya Uchumi wa Buluu na utekelezaji wake,  Dk. Mwinyi alisema Serikali  imegawa dhana hiyo katika sekta kuu tano , ambazo ni utalii, Bandari, Biashara na Usafirishaji, Uvuvi/mwani pamoja na Mafuta na Gesi.

Alisema utalii ni mhimili wa Uchumi wa Taifa, ambapo asilimia 30 ya Pato la Taifa linategmea Utalii, hivyo akabainisha malengo ya serikali kuwa ni kutumia vyema rasilimali za bahari katika kuwaletea maendeleo wananchi.

Alieleza kilimo cha mwani pamoja na uvuvi ni eneo linalochukua thuluthi mbili ya watu, hivyo serikali imeweka mkazo katika uimarishaji wa zana za uvuvi, ili kuimarisha uzalishaji na kuwaondolea wananchi umasikini.

Aidha, alisema Serikali ya Awamu ya nane imeanzisha ujenzi wa Bandari kubwa ya kisasa katika eneo la Mangapwani,itakayohusisha Bandari tofauti, kwa lengo la kuongeza pato la Taifa.

Dk. Mwinyi alisema eneo jengine lilioko katika sekta hiyo ni Mafuta na Gesi  na kubainsiha kiwango kikubwa cha Gesi kilichokwisha kugunduliwa na wataalamu hadi sasa.

               

Alisema biashara na usafirishaji Baharini ni neo ambalo bado halijafanyiwa biashara ya kutosha na kusema Serikali ina azma ya kuimarisha biashara baharini ili kuchochea uchumi wake.   

Rais Dk. Mwinyi akatumia fursa hiyo kuwahimiza wananchi kuendelea kudumisha amani iliopo nchini, ikiwa ni utamaduni uliozoeleka wa kuishi kwa amani na kuvumiliana miongoni mwa watu wenye imani tofauti za kidini.

Alisema Zanzibar ina historia ya muda mrefu ya wananchi wake kuishi kwa kuvumiliana kidini, jambo linaloiletea sifa kubwa nchi, sambamba na kuliwekea Taifa msingi muhimu wa Umoja.

Aidha, alipongeza uamuzi wa Kaanisa  Katoliki Zanzibar kwa mashirikiano  na viongozi wengine wa Dini katika Kamati ya kitaifa ya Amani inayojumuisha madhehebu tofauti ya Dini, na kusema mashirikiano hayo yanatoa nafasi kubwa ya kuimarisha umoja wa taifa katika kushajiisha maendeleo na Ustawi wa Jamii.

Alieleza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inathamani mchangao wa Viongozi wa Kidini katika utekelezaji wa mipango mbali mbali ya Maendeleo, na kubainisha azma ya kuzitafutia ufumbuzi changamoto zote zinazohusu masuala ya ajira, usafirishaji wa binadamu, ukwepaji kodi pamoja  na uimarishaji wa huduma za wagonjwa wanaoishi Kituo cha wazee Welezo.

Rais Dk. Mwinyi alisema anatambua mchango mkubwa wa taasisi za kidini katika kuwahimiza waumini juu ya utii wa sheria na kujiepusha na vitendo vya uvunjifu wa amani, ikiwemo matumizi ya dawa za kulevya, vitendo vya udhalilishaji, huku akipongeza taasisi za kidini kwa kuwa mstari wa mbele katika kusimamia maadili na ustawi wa jamii.

Sambamba na hilo alipongeza taasisi za kidini katika uimarishaji wa huduma za kijamii,ikiwemo uanzishaji wa skuli  zilizo chini ya madhehbu ya dini, ujenzi wa vituo vya afya na kutoa huduma bila ya ubaguzi.

“Tunathamini na kutambua mchango wa taasisi za kidini katika uimarishaji wa huduma za kijamii..............., napenda niwaahidi Serikali itaendelea kutoa ushirikiano kwa taasisi za Dini ili ziweze kutoa huduma mbali mbali kwa ufanisi zaidi”, alisema.

Dk. Mwinyi alitumia fursa hiyo kutoa shukrani kwa wuamini wa Jimbo la Zanzibar, huku akimuombea kheri Mhashamu Askofu Shao ili aweze kufanikisha vyema majukumu yake katika kipindi kijacho.

Aidha, Dk. Mwinyi alimkabidhi zawadi Mhashamu Askafu Shao kwa kuadhimisha miaka 25 ya Utumishi wake.

Nae, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamo wa Pili wa Rais, Sera, Uratibu na Baraza la Wawakilishi Hamza Hassan aliahidi kuzifanyia kazi changamoto zote zilizowasilishwa na Viongozi mbali mbali sambamba na kuahidi kuendeleza mashirikiano na viongozi na waumini wa Dini hiyo bila ubaguzi.

Aidha, Mkuu wa Mkoa wa  Mjini Magharibi Idrissa Kitwana Mustafa  alisema Serikali itaendelea kusimamia na kudumisha amani na utulivu uliopo nchini, hususan katika suala la imani na kuabudu.

Mapema, Askofu wa Jimbo Katoliki Zanzibar Mhashamu Askofu Augustino Mweleli Shao pamoja na mambo mengine aligusia uwepo wa changmoto mbali mbali zinazolikabili Kanisa na waumini wake.

Alisema Katiba ya Zanzibar inawapa  haki ya kumiliki ardhi wananchi wote bila ya ubaguzi wa dini au eneo mtu anatoka, jambo ambalo limekuwa kinyume chake kwa waumini wa dini hiyo.

Alisema pia Kanisa linakabiliwa na changamoto katika suala la upatikanaji wa vibali vya utoaji huduma na kusema Wamishonari hawawezi kutekeleza kazi za maendeleo ya jamii bila ushirikiano na  kubainisha kuwa jamii ya Wanzibari ni watu wapole, hivyo akaomba hali hiyo iende sambamba na upatikanaji wa fursa ili watu wengi wafanye kazi.

“Kanisa lipo tayri kulipa Vibali vya ukaazi, ni muhimu kwa Serikali kutambua  idadi ya watu kutoka nje.......naomba Serikali iangalie ili baadhi ya wakati tuondokane na  udanganyifu”, alisema.

Katika hatua nyengien, Naibu Mufti wa Zanzibar Sheikh Mahamoud Mussa alimsifia Askofu Shao kuwa  mtu mpole , mwenye tabia njema  pamoja na busara, hali inayomuwezesha kumudu kutekeleza majukumu yake kikamilifu.

Aidha, Mwakilishi wa Baba Mtakatifu kutoka Vitican  Monsignori Richard Gyhra akitoa salam kutoka kwa Papa, alitoa pongezi  kwa Askofu Shao kwa kazi ya utume uliotukuka kwa kondoo wake kiatika kipindi hicho cha miaka 25.

Imetayarishwa na Idaya ya Mawasiliano

Ikulu Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.