Na Muandishi Wetu.
Kamishna wa Bodi ya
Mapato Zanzibar (ZRB) Ndg. Yusuph Juma Mwenda amewataka wamiliki na wasimamizi
wa vyombo vya usafiri Baharini Zanzibar kuhakikisha kuwa kabla ya Juni 2022
wawe wameunganisha mifumo yao ya kibiashara na Mfumo wa kutolea Risiti za
Kielektroniki (VFMS) ZRB ili kuleta ufanisi katika ukusanyaji wa mapato nchini.
Agizo hilo amelitoa
leo katika kikao cha pamoja na wamiliki na wasimamizi wa kampunzi za
usafirishaji baharini katika kikao cha pamoja kilichofanyika katika ukumbi wa
mkutano wa Ofisi za Bodi ya Mapato Mazizini Zanzibar.
Kamishna Mwenda
amesema kuwa, wamiliki na wasimamizi hao wanatakiwa kuwasilisha ritani na
malipo kulingana na idadi sahihi ya abiria na mizigo wanayosafirisha kama
itakavyosomeka katika mfumo wa kutolea Risiti za Kielektroniki ili kuendana na
uhalisia wa biashara wanayoifanya sambamba na kupunguza malalamiko ambayo
wamekuwa wakihusishwa nayo.
Hivyo, Kamishna
Mwenda amewasisitiza kuwa sheria inamtaka kila anayefanya shughuli za kiuchumi,
na ambaye anapokea malipo ni lazima atoe risiti za kielektroniki. Na
amewatanabahisha kuwa Vyombo vya usafiri Baharini kama ilivyo kwa biashara
nyengine wanalazimika kuunganisha mifumo yao na mfumo wa VFMS ili Serikali ikusanye
kodi stahiki kulingana na biashara inayofanywa.
Kwa upande wa
wamiliki na wasimamizi wa vyombo hivyo vya usafiri Baharini wamesema kuwa, kupanda
kwa gharama za mafuta na kutokubadilika kwa bei za usafirishaji, miundombinu ya
hali ya Bandari ni miongoni mwa changamoto
zinazowapelekea kutokulipa kodi sahihi na kwa wakati.
Kikao hicho
kilihusisha wamiliki na wasimamizi wa vyombo vya baharini kutoka kampuni ya Zanfast
Ferries, Azam Marine, Ikram Sea Line na Flying Horse.
No comments:
Post a Comment