Habari za Punde

Filamu ya Royal Tour Kuitangaza Tanzania Kiutalii Duniani -Dk.Mwinyi.

 

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akihutubia wakati akizindua Filamu ya Tanzania Royal Tour, uzinduzi huo umefanyika katika ukumbi wa Hoteli ya Golden Tulip Uwanja wa Ndege Kiembesamaki Jijini Zanzibar leo 7-5-2022.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi  Dk. Hussein Ali Mwinyi amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mama Samia Suluhu Hassan kwa kuja na wazo la kutayarisha Filamu ya ‘The Royal Tours’ yenye lengo la kuitangaza Tanzania kiutalii Duniani.

Dk. Mwinyi ametoa shukurani hizo katika uzinduzi wa Filamu hiyo hapa Zanzibar, hafla iliofanyika katika Hoteli ya Golden Tulip iliopo karibu na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume.

Alisema madhumuhi ya kutayarisha filamu hiyo ni kuitangaza Tanzania katika nyanja za Utalii, Uwekezaji pamoja na Utamaduni, huku akibainisha Tanznaia kuwa na  utajiri mkubwa wa rasilimali ikiwemo maeneo ya fukwe, mbuga za wanyama, maeneo ya urithi (mji mkongwe)  na mengineyo na  hivyo kutoa fursa ya kuvutia Wawekezaji.

Aidha, aliwataka watendaji Serikalini na sekta binafsi, wadau wa Utalii pamoja na wananchi kwa ujumla kujipanga na kutoa huduma bora ili kukidhi mahitaji kutokana na wimbi kubwa la watalii linalotarajiwa kuzuru hapa nchini kutokana na utayarishaji wa filamu hiyo.

Nae,   Mwenyekti wa Kamati ya Maandalizi ya Filamu hiyo Dk. Abass alisema filamu hiyo imeandaliwa na kusimamiwa na mabingwa katika usimamizi wa filamu Duniani.

Mapema, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Kukuza  Uwekezaji Zanzibar (ZIPA) Sharrif Ali Sharrif alisema utayrishaji wa filamu hiyo ni jambo linalotoa taswira ya kuimarika kwa Muungano wa Tanzania, huku akibainisha jinsi itakavyofanikiwa kuitangaza Tanzania.

Katika hafla hiyo iliohudhuriwa na Viongozi mbali mbali wa Serikali, akiwemo Makamo wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Mohamed Gharib Bilali, Makamo wa Pili wa Rais Hemed Sleiman Abdalla pamoja na viongozi mbali mbali, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Mwinyi alikabidhiwa Tuzo ya uigizaji Bora wa Filamu    Tanzania.  

Imetayarishwa na Idaya ya Mawasiliano

Ikulu Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.