Habari za Punde

Makamu  wa  Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe.Hemed Suleiman Abdulla akizungumza baada ya kumaliza mazoezi ya viungo na matembezi yalioazia katika viwanja vya Afiso za ZRB Mazizini na kumalizia katika viwanja vya Baraza la Wawakilichi Chukwani. 

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imewataka Wananchi kufahamu umuhimu wa kukusanya kodi kwa kutumia Mashine za Kielektroniki ili kukuza mapato ya Nchi.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla ametoa kauli hiyo katika matembezi ya kuhamasisha zoezi la kudai  risiti  za Kielektroniki yaliyoambatana na mazoezi ya vingo yaliyoanzia Afisi za Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB) na kumalizia Uwanja wa Baraza la Wawakilishi Chukwani Zanzibar.

Amesema ni vyema Wananchi kwa Ujumla kudai na kutoa risiti kwa wanaofanya miamala ya kibiashara ili kudhibiti ukusanyaji wa Mapato yasiweze kupotea kiholela.

Mhe. Hemed ameeleza kuwa jukumu la msingi kwa Serikali ni kuweka mipango madhubuti ya ukusanyaji wa mapato ambayo yatatumika katika ujenzi wa Miradi mbali mbali ya maendeleo ili kuijenga Zanzibar mpya.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amewataka Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kufikisha Elimu ya kudai na kupokea risiti  kwa Wananchi wao katika majimbo yao  ili  iwafikie Wananchi wote.

Pamoja na hayo Mhe. Hemed ametoa wito kwa Wananchi kuunga mkono suala hilo kwa kutoa  taarifa kwa wasiodai na wasiotoa risiti ili kuwadhibiti wanaokiuka sheria hiyo na wanaouhujumu chumi wa nchi.

Sambamba na hayo Mhe. Hemed ameagiza Serikali za Mikoa kufatilia kuona utumiaji wa mashine za Kielektroniki katika maeneo yao na kuwachukulia hatua wote wasiotumia mashine hizo.

Kwa upande wake Spika wa Baraza la Wawakilishi la Zanzibar Mhe. Zubeir Ali Maulid ameeleza kuwa ni vyema kwa Wauzaji na wafanyabiashara kuweka matangazo katika maeneo yao ya Biashara ambayo yataonesha umuhimu wa kudai risiti kwa anaenunua bidhaa katika maeneo yao ya kazi.

Aidha Mhe. Zubeir ameeleza kwa kuwa wanamichezo wanaushawishi mkubwa katika jamii hivyo Baraza la Wawakilishi limeamua kuandaa matemebezi hayo pamoja na mazoeai ya viungo ili kuamsha ari ya uelewa kwa jamii.

Nae Waziri wa Nchi Afisi ya Rais Fedha na Mipango Mhe. Dkt Sada Mkuya Salum ameeleza kuwa Wizara imejipanga kukusanya mapato katika maeneo mbali mbali ikiwemo kwa wafanyabiashara na kuwaomba Wananchi kuendelea kuunga mkono juhudi hizo kwa kudai risiti kwa anaefanya miamala.

Kwa upande wake Kamishna wa Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB) Ndugu Yussuf Juma Mwenda  ameeleza kuwa suala la kulipa Kodi ni la kila mmoja ambapo Serikali imejipanga kuongeza Mapato yake kwa njia ya kisasa ili kuweka kumbukumbu kwa wanaofanya biashara.

Aidha Kamishna Mwenda ameitaka jamii kukanusha taarifa zinazoenea katika jamii ya kuwa matumizi ya mashine hizo kunaongeza Kodi  na kueleza kuwa mashine zipo kwa udhibiti wa Kodi Sahihi ili kuongeza Pato la Taifa.

Matembezi hayo yaliyoanzia Afisi za Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB) Mazizini yamejumuisha vikundi mbali mbali vya mazoezi vya Zanzibar, Taasisi binafsi na Mashirika mbali mbali ya Serikali ambayo  yamesimamiwa na Afisi ya Baraza la Wawakilishi kwa mashirikiano ya Jumuiya ya Vikundi vya mazoezi Zanzibar (ZABESA)

ABDULRAHIM KHAMIS
AFISI YA MAKAMU WA PILI WA RAIS WA ZANZIBAR
19 Juni 2022

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.