Habari za Punde

Serikali Yapokea Gawio la Shs. Bilioni 36.1 Kutoka Benki ya CRDB.

Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), akiwa akipokea mfano wa hundi kifani yenye thamani ya Sh. bilioni 19.7 ikiwa ni sehemu ya gawio la shilingi bilioni 36.1 ambazo Benki ya CRDB imetoa, katika hafla iliyofanyika jijini Dodoma.

Na. Peter Haule na Saidina Msangi, WFM, Dodoma.                                                                      Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba,  amepokea gawio la shilingi bilioni 36.1 kutoka Benki ya CRDB na kuahidi kutumia fedha hizo katika kutekeleza miradi ya maendeleo ikiwemo sekta ya elimu, afya na miundombinu.                                                                                                               

Dkt. Nchemba aliyasema hayo jijini Dodoma wakati akipokea gawio la jumla ya shilingi bilioni 36.1 kutoka Benki ya CRDB, ikiwa ni gawio kwa mwaka 2021 linatokana na uwekezaji ambao Serikali imefanya ndani ya Benki kwa kushirikiana na mfuko wa Uwekezaji wa pamoja na Serikali ya Denmark (DANIDA) pamoja na Taasisi na Mashirika mbalimbali ya umma.

 

Fedha hizo zimekuja kwa wakati mwafaka baada ya Bunge kupitisha Bajeti Kuu ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2022/23 na kwamba fedha hizo zitasaidia kutekeleza bajeti hiyo.

 

Aidha alisema  kuwa Serikali ya Awamu ya Sita itaendelea kuimarisha na kuweka mazingira rafiki na endelevu ya kufanya biashara katika sekta ya fedha ili kuiwezesha sekta hiyo kutoa mikopo kwa sekta za uzalishaji kwa lengo la kuwezesha taasisi hizo kutoa mikopo yenye riba nafuu itakayowezesha kuongeza uzalishaji na ajira kwa wananchi.  

 

Vilevile amewataka watu wote wanaokopa katika taasisi za fedha kuhakikisha wanalipa, kwa kuwa utaratibu wa kukwepa kulipa ni jambo ambalo halikubaliki kwa kuwa utapeli unachafua taswira ya nchi.

 

“Utapeli unasababisha vikwazo kwa watu wengine ambao nao wanahaki ya kupata mikopo ambayo ingewasaidia kupata mitaji na kujishughulisha katika shughuli mbalimbali za kiuchumi ambazo zingechochea maendeleo na kuimarisha uchumi wa nchi”, alisema Dkt. Nchemba.

Pia ameipongeza Benki hiyo kwa kupunguza riba katika mikopo ya kilimo kutoka asilimia 20 hadi asilimia 9, kupunguza riba katika mikopo ya wafanyakazi na wastaafu kutoka asilimia 16 hadi asilimia 13.

 

Vilevile kuingia mkataba na Mfuko wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Hali ya Hewa (UNGCF) wa jumla ya dola za Marekani milioni 200 kuwezesha wakulima nchini kufanya kilimo stahimilivu kupitia Programu ya Matumizi ya Teknolojia Endelevu za Kilimo Tanzania (TACADTP).

 

Kwa upande wao Manaibu Mawaziri wa TAMISEMI, Mhe. David Silinde na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Vijana, Mhe. Patrobas Katambi, wamezipongeza Halmahauri ambazo zimeongeza ubunifu kwa kuwekeza Hisa katika Benki ya CRDB kwa kuwa wameongeza wigo wa mapato.

Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Mhe. Lawrance Mafuru, alisema kuwa miongoni mwa viashiria vya kukua kwa uchumi ni ongezeko la mikopo katika Sekta binafsi. Sekta ya Benki mpaka Aprili mwaka huu imekua kwa asilimia 13 na benki tano za juu ambazo zinafanya vizuri ni za watanzania hivyo kuwa na uhakikia na matokeo chanya ya uchumi wa nchi.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela, alisema kuwa  Benki hiyo inatoa  gawio la Sh. bilioni 36.1 kwa Serikali na Taasisi zake ambapo Mfuko wa Ushirikiano wa Serikali na DANIDA umepata shilingi bilioni 19.7Mfuko wa Hifadhi kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) shilingi bilioni 11.8 Mfuko wa Hifadhi ya Taifa (NSSF) – shilingi milioni  501.9 na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar (ZSSF) shilingi milioni   827.2.

Aidha Uwekezaji kupitia Serikali za Mitaa ni pamoja na Mfuko wa Maendeleo wa Lindi shilingi milioni 535.5Halmashauri ya Manispaa ya Mbinga shilingi milioni 5.8, Manispaa ya Shinyanga milioni 60.2 na Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi shilingi milioni 3.2.

Halmashauri zingine zilizopata mgao ni pamoja na Wilaya ya Chunya na Rungwe pia Local Government Loans BoardMfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), Umoja Fund Unit Trust Scheme na Chama cha Ushirika cha Wakulima wa Tumbaku Kanda ya Magharibi na kufanya jumla ya gawio lililotolewa Serikalini kufikia shilingi bilioni 36.1

Benki ya CRDB imeendelea kuimarika na kuongeza faida kila mwaka na kusababisha kuongezeka kwa gawio la wanahisa kutoka Shilingi 22 kwa hisa moja kwa mwaka 2020 hadi Shilingi 36 kwa mwaka 2022 ikiwa ni ongezeko la asilimia 64%.

Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), akiteta jambo na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela (kulia) baada ya Benki hiyo kukabidhi gawio la Sh. bilioni 36.1, kwa Serikali na Taasisi zake kwa mwaka 2021, katika hafla iliyofanyika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango, jijini Dodoma.

Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), akizungumza wakati wa hafla ya Benki ya CRDB kukabidhi gawio la Sh. bilioni 36.1, kwa Serikali na Taasisi zake kwa mwaka 2021, iliyofanyika katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango, jijini Dodoma.
Naibu Katibu Mkuu Wizara Fedha na Mipango, Bw. Lawrence Mafuru, akizungumza wakati wa hafla ya Benki ya CRDB kukabidhi gawio la Sh. bilioni 36.1, kwa Serikali na Taasisi zake kwa mwaka 2021, iliyofanyika katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango, jijini Dodoma.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela, akizungumza katika hafla ya kutoa gawio la Sh. bilioni 36.1kwa Serikali na Taasisi zake, katika hafla iliyofanyika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango, jijini Dodoma.
Naibu Waziri Ofisi ya Rais TAMISEMI. Mhe. David Silinde (Mb) na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Vijana, Mhe. Patrobas Katambi (kulia) wakifuatilia hotuba ya Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba(Mb) (hayumo pichani), wakati wa hafla ya Benki ya CRDB kukabidhi gawio la Sh. bilioni 36.1, kwa Serikali na Taasisi zake kwa mwaka 2021, iliyofanyika katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango, jijini Dodoma.

Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), (wa pili kushoto walioketi) akiwa katika picha ya pamoja na Menejimenti ya Benki ya CRDB baada ya benki hiyo kukabidhi gawio la Sh. bilioni 36.1, kwa Serikali na Taasisi zake kwa mwaka 2021, katika hafla iliyofanyika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango, jijini Dodoma.

(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, WFM, Dodoma)


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.