Habari za Punde

SMZ Itafanya Bidii Kuhakikisha Inautengeneza Mfuko wa Hijja ili Kuwasaidia Wale Wasio na Uwezo.

 

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk.Hussein Ali Mwinyi akiitikia dua ikisomwa na Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh.Saleh Omar Kabi (kushoto kwa Rais) baada ya kumaliza kuzungumza na kuwaaga Mahujaji Wataraji wanaojiendaa kuelekea Nchini Saudi Arabia (Makka) kwa ajili ya Hija, hafla hiyo iliyofanyika katika Masjid Jamiu Zinjibar Mazizini Unguja leo 18-6-2022 na (kulia kwa Rais) Waziri wa Katiba Sheria,Utumishi na Utawala Bora Zanzibar Mhe. Haroun Ali Suleiman.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya itafanya bidii katika kuhakikisha inautengeneza Mfuko wa Hijja ili kuwasaidia wale wote wasio na uwezo wa kwenda kufanya ibada ya Hijja wapate fursa hiyo.

Alhaj Dk. Mwinyi ameeleza hayo leo wakati alipokuwa akiwaaga Mahujaji watarajiwa wa Zanzibar wanaokwenda kutekeleza ibada ya Hijja huko Makka, Saud Arabia mwaka huu, hafla iliyofanyika huko Masjid  Jamii Zanjibar, Mazizini Mkoa wa Mjini Magharibi.

Akitoa nasaha zake, Alhaj Dk. Mwinyi alieleza kwamba mfuko wa Hijja utawasadia kwa kiasi kikubwa wale ambao hawana uwezo wa kwenda kutekeleza ibada hiyo huko Makka sambamba na kufikia lengo na madhumuni ya kupata watu wengi kwenda Hijja.

Alhaj Dk. Mwinyi aliwaomba waumini kuwa na subira kutokana na kuwepo kwa masharti ya umri katika ibada ya Hijja ya mwaka huu huku akipongeza idadi ya Mahujaji waliojitokeza mwaka huu kwenda kutekeleza ibada hiyo licha ya changamoto kadaa zilizojitokeza.

Akitoa ufafanuzi kuhusu maombi ya Mahujaji kwa Serikali, alisema kuwa kwa upande wa huduma ya vipimo vya “PCR test” hivi sasa huduma hiyo inatolewa na sekta binabsi kwa dola 80 ambapo katika makubaliano na Serikali dola 50 inakwenda kwa Serikali na dola 30 inakwenda kwa sekta binafsi na kueleza utayari wa Serikali kuondoa dola 50 na kubakisha ya watoa vipimo hao huku akiahidi kuwaomba ili kinachotolewa na Mahujaji kiwe kidogo zaidi.

Alieleza kuwa Serikali itatizama uwezekano wa kuondosha cheti cha afya kama ilivyo kwa Tanzania Bara huku akieleza kwamba amelipokea suala la akauti maalum ya Zanzibar kwa ajili ya Hijja na kueleza kwamba suala hilo litafikishwa katika ngazi husika ili kuweza kuondoshwa kwani limefikia pazuri.

Aidha, alieleza kwamba kuna kazi ya ziada ya kufanywa na Serikali, Taasisi pamoja na wananchi kwa ujumla ya kujifunza hasa kwa nchi zenye Waislamu wengi kama vile Malaysia na Indonesia ambapo huanza mipango ya kwenda Hijja mapema.

Alieleza kwamba miongoni mwa mipango inayofanywa na nchi hizo pamoja na utaratibu mzuri wa kukukusanya fedha za Hijja kwani kuna wazazi wanaaza kuwawekeza watoto wao akauti za Hijja mara tu anapozaliwa mtoto mpaka pale anapofikia umri wa kwenda kuhiji fedha zinakuwa tayari zimeshakamilika.

Alhaj Dk. Mwinyi alisisitiza suala la umoja na kueleza haja ya kuuendeleza umoja wao hasa kwa Mahujaji hao wakati wakiwa katika Ibada hiyo ya Hijja huko Makka nchini Saud Arabia.

Alieleza kwamba kwa wale wanaokwenda kwa mara ya kwanza wana kila sababu ya kuhakikisha wanaifanya ibada ya Hijja kwa uzuri zaidi kwani inawezekana ikawa ndio ibada yako ya mwisho ya Hijja na hawatopata nafasi nyengine tena.

Alieleza kwamba mafunzo ya Hijja waliyopewa yatawasaidia na kuwataka kuzingatia suala zima la Ikhlas, kufanya ibada inavyotakiwa, suala la subira pamoja na kuutumia vizuri wakati wa ibada ya Hijja.

Aliwasisitiza Mahujaji hao watarajiwa kuiombea dua nchi, ili Mwenyezi Mungu ajaalie kuendelea kuwa na amani pamoja kuiondolea nchi mambo mazito yote yaliopo duniani huku akiwaombea safari njema sanjari na kukubaliwa ibada zao.

Nae Waziri wa Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora Haroun Ali Suleiman kwa upande wake alimpongeza Alhaj Dk. Mwinyi kwa kufuatilia kwa karibu safari ya Hijja ya Mahujaji wa Zanzibar.

Alisisitiza haja ya kuiombea dua nchi pamoja na kumuombea dua Rais Dk. Mwinyi ili azidi kuiletea maendeleo Zanzibar huku akisisitiza suala zima la Hijja kwa Mahujaji na kufuata maelekezo ya viongozi.

Akieleza suala zima la akauti inayojitegemea ya Hijja kwa Zanzibar, Waziri Haroun alisisitiza haja ya kuwepo kwa akaunti hiyo ili kuepuka changamoto zinazojitokeza.

Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Saleh Omar Kabi aliwaeleza Mahujaji hao umuhimu wa Hijja na kuwaombea kwa Mwenyezi Mungu kukubaliwa Hijja zao.

Nae Katibu Mtendaji wa Kamisheni ya Wakfu na Mali ya Amana Sheikh Abdalla Talib kwa upande wake alitoa pongezi kwa Rais Dk. Mwinyi kwa kwenda kuwaunga mkono kwa kuwaaga Mahujaji na kueleza kuwa huo ni utamaduni wa muda mrefu uliowekwa.

Alisema kuwa maandalizi ya Hijja yakikamilika hukutana na usiku wa siku ya pili viongozi wa taasisi za Hijja huwenda Saudia Arabia na kwa mwaka huu tarehe 22 mwezi huu kundi la kwanza linatarajiwa kuondoka kuelekea nchini Saud Arabia.

Alisema kuwa Zanzibar imeanza utaratibu wa kuratibu shughuli za Hijja tokea mwaka 1923 ambapo wakati huo ilikuwa ikiratibu kanda yote ya Afrika Mashariki ambapo pia, mnamo mwaka 1945 ndio mara ya kwanza watu kutakiwa wachukue pasi za kusafiria pamoja na Mahujaji kuanza kwenda kwa usafiri wa ndege ambapo kundi la kwanza kusafiri kwa Afrika Mashiriki lilitokea Zanzibar.

Pia, alieleza azma ya Alhaj Dk. Mwinyi ya kuhakikisha Mahujaji wanaongezeka kutokana na juhudi kubwa za maendeleo anazozichukua hapa nchini.

Akitoa historia fupi Katibu Huyo Mtendaji wa Wakfu na Mali ya Amana alisema kuwa Hijja kila baada ya miaka kunatokea mabadiliko kwani

Nae Mwenyekiti wa Kamati ya Hijja Yussuf Salim Yussuf akisoma risala ya Umoja wa Taasisi za Hijja Zanzibar (UTAWAZA), alisema kuwa kwa mwaka huu (UTAWAZA), unaziratibu taasisi 23 zinazotegemea kusafirisha Mahujaji 1,600 huku akieleza lengo la taasisi hiyo ni kuimarisha huduma za Hijja na kuzifanya ziwe na ufanisi zaidi.

Alisema kuwa ongezeko la idadi ya mahujaji haliridhishi kwani bado kuna idadi ndogo ya Mahujaji wanaokwenda kutekeleza ibada hiyo ikilinganishwa na Waislamu waliopo nchini.

Aliongeza kuwa Serikali ya Saud Arabia kwa mwaka huu imetoa nafasi za Hijja kwa Mahujaji 11,467 kwa Tanzania lakini kutokana na sababu mbali mbali imeshindikana kufikisha hata robo ya idadi hiyo kwani kwa mwaka huu Zanzibar inatarajia kusafirisha Mahujaji 1,600 na Tanzania Bara Mahujaji 1,100.

Alieleza kwamba ongezeko la gharama za utekelezaji wa Hijja, zuio la umri unaozidi miaka 65 pamoja na hali za maisha ya watu zimesababisha kutokwenda kutekeleza ibada hiyo muhimu.

Pia, Mwenyekiti huyo alitoa ombi kwa Serikali kutumia taasisi zake na vyombo vya habari kuwashajiisha wenye uwezo kwenda kutekeleza ibada hiyo, kuwahamsisha wenye uwezo kuwasaidia wasio na uwezo kwenda kuhiji, serikali kusimamia na kuhakikisha Mfuko wa Hijja unaanza rasmi, kuangalia namna bora ya upatikanaji wa vipimo vya UVIKO-19, bila ya malipo kwa Mahujaji pamoja na kuondoa cheti cha afya ya msafiri.

Imetayarishwa na Idara ya Mawasiliano,

Ikulu Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.