Habari za Punde

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe.Hemed Suleiman Abdulla Amefunga Mafunzo ya Wakufunzi wa Sensa ya Watu na Makazi Ngazi ya Taifa.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ambae pia ni Mwenyekiti Mwenza wa Kamati Kuu ya Sensa ya Watu na Makaazi Tanzania Mhe. Hemed Suleiman Abdulla, akihutubia na kuyafunga mafunzo ya Wakufunzi wa Sensa Tanzania yaliofanyika katika ukumbi wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu cha Mkwawa Iringa.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla akimkabidhi cheti Ndg. Devota Meta mmoja kati ya Wanafunzi bora wa Mafunzo ya Wakufunzi wa Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022 hafla iliyofanyika katika Ukumbi wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Mkwawa Mkoani Iringa.

Na.Abdulrahim Khamis

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla amewataka wakufunzi wa Sensa kutoa Taaluma ipasavyo ili kufanikisha zoezi la Sensa linalotarajiwa kufanyika Tarehe 23 Agosti mwaka huu.

Mhe. Hemed ambae pia ni Mwenyekiti Mwenza wa Kamati Kuu ya Sensa ya Watu na Makaazi 2022 ametoa kauli hiyo wakati akifunga mafunzo ya Wakufunzi wa Sensa ya watu na Makazi ngazi ya Taifa iliyofanyika ukumbi wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Mkwawa Mkoani Iringa.

Amesema kuwa ni dhahiri Elimu waliyoipata wataitumia ipasavyo katika ngazi zinazofuata akitolea mfano Mikoa, Wilaya, Tarafa na Shehia ili kupata takwimu sahihi na zinazokidhi vigezi na kanuni za Umoja wa Mataifa.

Aidha Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ameeleza kuwa kwa mujibu wa kanuni za Umoja wa Mataifa za kufanya Tafiti na Sensa ya Watu na Makazi ni lazima wenye uzoefu katika sekta mbali mbali kushiriki katika mafunzo kwa lengo la kujenga uelewa mpana kuhusu namna ya kukusanya taarifa kwa kutumia kanuni zilizopo

Ameeleza kuwa zoezi la  Sensa ya watu na makazi ni zoezi litakalowezesha kupata takwimu muhimu katika kupanga mipango ya Nchi pamoja na kutekeleza matakwa ya Umoja wa Mataifa.

"Zoezi hili linatuwezesha kupata takwimu muhimu katika kupanga mipango yetu ya Maendeleo na pia kuweza kutekeleza Matakwa ya Umoja wa Mataifa ambapo Tanzania ni Nchi Mwanachama" Mhe. Hemed

Aidha Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amezitaka Kamati zote za Sensa za Mikoa, Wilaya  Tarafa na Shehia kuhakikisha Makarani na wasimamizi watakaopatiwia mafunzo wawe ni wakazi wa maeneo husika ambao wanajua maeneo hayo jambo ambalo litasaidia wanakaya kuwa na Imani zaidi wakati wa kuchukua Taarifa.

Sambamba na hayo Mhe. Hemed amewataka wananchi kutoa ushirikiano kwa Makarani wa sensa watakapopita katika maeneo yao ili kurahisisha zoezi hilo kukamilika kama lilivyopangwa.

Aidha Mwenyekiti huyo mwenza wa Kamati Kuu ya Taifa ya Sensa ya Watu na Makazi ametumia fursa hiyo kuwapongeza viongozi wakuu wa Nchi Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan pamoja na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi kwa maelekezo yao katika kuhakikisha Operesheni ya anwani za Makazi inakamilika kwa mafanikio.

Aidha ameeleza kuwa juhudi za viongozi hao imefanikisha kufikia asilimka Thamanini na Saba (87%) maandalizi ya Sensa ya watu na makazi ambapo amewataka wananchi kuendelea kuunga mkono Serikali katika kuhakikisha zoezi hilo linafanikiwa kwa Asilimia Mia moja (100%)

"Hadi sasa maandalizi ya Sensa ya Watu na Makazi yamefikia asilimia Thamanini na Saba (87%) kuelekea Tarehe 23 Agosti, 2022. Hii ni hatua nzuri ambayo Wananchi hatuna budi kuiunga Mkono Serikali katika kuhakikisha zoezi hilo linafanikiwa. Hii ni pamoja na kutoa ushirikiano wa kutosha kwa Makarani na Wasimamizi wa Sensa watakapozitembelea Kaya zetu" amesema

Kwa upande wake Waziri Afisi ya Waziri Mkuu Sera, Uratibu na Bunge Mhe. George Simbachawine ameeleza kuwa Sensa ya Mwaka huu itakuwa ni ya mfano na kueleza kuwa Serikali imeiandaa kwa ufanisi mkubwa ili kufikia malengo.

Aidha Mhe. Simbachawine ameeleza kuwa miongoni mwa upekee wa Sensa hiyo ni ushiriki mzuri wa Taasisi na makundi mbali mbali ikiwemo Vyama vya Siasa, Wajasiriamali, Asasi za Kiraia,Vijana na wengine.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Hamad Chande ameeleza kuwa kukamilika kwa mafunzo hayo ni hatua moja wapo ya kufanikisha Sensa ya Mwaka huu na kuwataka wahitimu hao kumtanguliza Mungu mbele ili kupata baraka zake katika kukamilisha zoezi hilo.

Mtakwimu Mkuu wa Serikali Dkt. Albina Chuwa pamoja na Mtakwimu Mkuu wa Serikali ya Mapiduzi Zanzibar Bw. Salum Kassim Ali Wameeleza kuwa mafunzo hayo yamejumuisha Washiriki Mia Nne na Kumi (410) ambapo Wakufunzi walioendesha ni wabobezi wa Sensa zilizopita.

Aidha wameeleza kuwa watawajibika vyema kusimamia zoezi hilo liweze kukamilika kwa maslahi ya Taifa.

Afisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

01/07/2022

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.