Habari za Punde

Mhe.Majaliwa Akagua Mashamba Yalioharibiwa na Tembe Wilayani Nachingwea na Kutoa Pole kwa Waathirika.

 

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Mzee Athumani Mohamed Nkabuye  wakati alipokagua shamba la mtama la mzee huyo ambalo limeharibiwa na tembo waliokula zao hilo  katika kijiji cha Namapuya wilayani Nachingwe, Julai 6, 2022. Kushoto ni Mkuu wa Mkoa Lindi, Zainab Telack. 
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Mzee Athumani Mohamed Nkabuye  wakati alipokagua shamba la mtama la mzee huyo ambalo limeharibiwa na tembo waliokula zao hilo katika kijiji cha Namapuya wilayani Nachingwe, Julai 6, 2022. Kushoto ni Mkuu wa Mkoa Lindi, Zainab Telack na kula ni  Mkuu wa wilaya ya Nachingwea, Hashim Abdallah Komba.                                                      

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na wananchi wa kijiji cha Mwandila wilayani Nachingwea wakati alipotoa pole  kwa wananchi hao ambao   vijiji vyao vilivamiwa na tembo waliosababisha kifo cha mtu mmoja, Riziki Rashid Issa  na kuharibu mashamba ya mazao ya chakula katika baadhi ya vijiji wilayani humo.

(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

RAIS Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ametoa pole kwa wananchi kutokana na athari walizozipata baada ya tembo kuvamia katika vijiji vyao na kusababisha maafa kikiwemo kifo.

 

Salamu hizo zimetolewa leo (Jumatano, Julai 6, 2022) na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kwa niaba ya Rais Mheshimiwa Samia, wakati akizungumza na wananchi katika kijiji cha Nditi.

 

Waziri Mkuu amefanya ziara wilayani Nachingwea kwa ajili ya kukagua athari zilizosababishwa na uvamizi wa tembo katika mashamba ya wananchi kwenye kijiji cha Namapwiya na kuwapa pole wananchi hao.

 

Amesema Rais Mheshimiwa Samia anawapa pole kutokana na athari hizo na kwamba Serikali itahakikisha hakuna mwananchi atakayekosa chakula.

 

Amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Nachingwea kupitia kamati ya maafa ya wilaya ahakikishe wanaandaa utaratibu wa kupatikana chakula kwa wananchi wote ambao mashamba yao yameathiriwa na wanyamapori.

 

Waziri Mkuu amesema tatizo hilo limechangiwa na wafugaji kuvamia maeneo ya hifadhi kwa kuingiza mifugo ikiwemo mbuzi, ng’ombe na kondoo katika hifadhi na kusababisha wanyamapori kukimbia na kwenda kwenye makazi ya wananchi.

 

Kufuatia hali hiyo Waziri Mkuu amemwagiza Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki kukutana na wafugaji na kuwataka kutopeleka ng’ombe na mbuzi kwenye maeneo ya hifadhi.

 

Pia, Mheshimiwa Majaliwa ametoa wito kwa wananchi kutoingia na kuendesha shughuli za kilimo katika maeneo ya hifadhi ili kuepuka mazao yao kuharibiwa na wanyamapori.

 

Amesema katika kuhakikisha wanyamapori wanadhibitiwa, Mheshimiwa Rais Samia ameridhia zaidi ya shilingi bilioni 1.2 zitumike kwa ajili ya ujenzi wa vituo 19 vya askari wa wanyamapori karibu na maeneo ya hifadhi.

 

Waziri Mkuu amesema kati ya vituo hivyo vitatu vitajengwa katika wilaya tatu za mkoa wa Lindi ambazo ni Nachingwea (Nditi), Liwale (Liwale) na Milola (Ruangwa)

 

Waziri Mkuu amesema Mheshimiwa Rais Samia ameridhia kibali cha ajira 6,000 za askari wa wanyamapori ambao watasambazwa katika maeneo yete yanayopakana na hifadhi.

 

Amesema ajira hizo zinalenga kuendelea kuimarisha ulinzi na kudhibiti wanyamapori kuingia kwenye maeneo makazi ya wananchi. “Tuanataka wananchi  waendelee kuishi kwa amani.”

 

Mheshimiwa Majaliwa amesema Serikali imetoa namba ya bure ya mawasiliano ambayo ni 0800110067 ili kuwawezesha wananchi kutoa taarifa mara wanyamapori wanapovamia kwenye makazi yao.

 

Akiwa katika kata ya Nditi kijiji cha Namanja kabla ya kuzungumza na wananchi Waziri Mkuu alikwenda kuifariji familia ya marehemu Riziki Issa ambaye aliuawa na tembo.

 

Akizungumza kwa niaba ya familia hiyo Mussa Nambole amesema wamefarijika kwa namna ambavyo viongozi mbalimbali wa Serikali walivyoshirikiana nao katika kipindi cha msiba huo.

 

Naye, Mbunge wa Nachingwea Dkt. Amandus Chingwile ameishukuru Serikaki kwa kuweka mikakati mbalimbali inayolenga kuzuia uvamizi wa wanyamapori kwenye makazi ya wananchi

IMETOLEWA NA:

OFISI YA WAZIRI MKUU,

JUMATANO, JULAI 06, 2022.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.