Habari za Punde

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe Hemed Suleiman Abdulla Amekutana na Kuzungumza na Balozi wa Tanzania Nchi Indonesia.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla akisalimiana na Balozi wa Tanzania Nchini Indonesia Mhe.Macocha Yembele alipofika katika Ofisi ya Makamu kwa ajili ya mazungumzo na kujitambulisha. 
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla akizungumza na Balozi wa Tanzania Nchi Indonesia Mhe. Macocha Yembele, alipofika Ofisini kwake Vuga kwa ajili ya mazungumzo na kujitambulisha na kumuaga akielekea Kituo chake cha Kazi.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla akiwa katika picha ya pamoja na Balozi wa Tanzania Nchi Indonesia Mhe. Macocha Yembele, alipofika Ofisini kwake Vuga kwa ajili ya mazungumzo na kujitambulisha na kumuaga akielekea Kituo chake cha Kazi.

Na.Abdulrahim Khamis

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla amemuhakikisha mashirikiano ya kutosha Balozi  wa Tanzania Nchini Indonesia Mhe. Macocha Yembele. 

Ameyasema hayo katika mazungumzo yaliyofanyika Afisini kwake Vuga Jijini Zanzibar wakati Balozi huyo alipofika kujitambulisha na kumuaga baada ya kushika wadhifa huo.

 

Mhe. Hemed amempongeza Balozi Yembele kwa Imani aliyopewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuiwakilisha Tanzania Nchini Indonesia ambapo Serikali inategemea mafanikio katika kukuza Uchumi wa Tanzania kupitia mashirikiano yaliyopo baina ya Nchini hizo mbili.

 

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amemueleza Balozi huyo kuwa Zanzibar ina mahusiano makubwa hasa ya kibiashara na Indonesia katika Bidhaa ya karafuu ambapo amemtaka Balozi huyo kuongeza mashirikiano na wakulima wa zao hilo anapokuwa katika eneo lake la kazi ili kujua njia bora wanazotumia katika kuzalisha zao hilo kwa wingi.

 

Sambamba na hayo Mhe. Hemed amemuomba Balozi Yembele kuitangaza sera ya Zanzibar ya Uchumi wa Buluu hasa akizingatia kuwa Indonesia ina visiwa vingi mithili ya Zanzibar .

 

Aidha Mhe. Hemed amemtaka Balozi huyo kuweka Historia nzuri kwa kuwa Balozi wa kwanza tokea kuanzishwa kwa Balozi ya Tanzania Nchini Indonesia kwa kuacha athari nzuri nchini humo.

 

Mhe. Hemed ametumia fursa hiyo kumuasa Balozi huyo kuitangaza Tanzania kwa mazuri yake hasa Suala la Utalii na vivutio mbali mbali vilivyopo nchini ili kuikuza sekta ya Utalii Nchini.

 

Aidha amemuomba kueleza fursa za uwekezaji zilizopo Nchini na kuwakaribisha wawekezaji kutoka Nchini Indonesia kuja kuwekeza ili kuzidisha zaidi uhusiano na udugu uliopo baina ya Nchi hizo.

 

Nae Balozi wa Tanzania Nchini Indonesia Mhe. Macocha Yembele amemuhakikishia Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kuwa atasimamia maelekezo aliyopewa na viongozi wakuu katika kuiwakilisha Tanzania kwenye majukumu yake ikiwemo kuongeza Diplomasia pamoja na kuzitangaza fursa mbali mbali za kiuchumi zilizopo nchini.

 

Aidha Balozi Yembele ameeleza kuwa wapo Watanzania wengi Nchini Indonesia ambapo kwa ushirikiano wao wataweza kufikia malengo waliyokusudiwa na viongozi wakuu wanchi ya kuwaletea maendeleo wananchi wake kupitia ushirikiano  na nchi mbali mbali.

 

Afisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

06/07/2022.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.