Habari za Punde

Tanzania Kunufaika na Wenyeji wa Mkutano wa 65 wa UNWTO.

  • Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe.Pindi akizungumza na Waandishi wa habari ,jijini Arusha.

  • Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe.Pindi akizungumza Mkurugenzi wa Shirika la Utalii Duniani Kamisheni ya Afrika Bi. Marie Elicie mara baada ya kumaliza kuongea na Waandishi wa Habari.

    Tanzania inatarajia kunufaika na fursa mbalimbali zitakazotokana na  Mkutano wa 65 wa Shirika la Utalii Duniani UNWTO – CAF utakaofanyika jijini Arusha kuanzia  Oktoba 5 hadi 7, 2022.

    Hayo yamesemwa na Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana alipokua akizungumza na vyombo vya habari  jijini Arusha  kuhusu kufanyika kwa mkutano huo ambapo amesema Tanzania itanufaika  na ujio wa mkutano huo kwa kukuza na kuendeleza utalii, kuimarisha ushirikiano wa kimataifa pamoja na lengo litakalowekwa la haki ya msingi ya binadamu kutembelea maeneo mbalimbali ya vivutio vya Utalii bila vikwazo vyovyote.

    Kuhusu mkutano huo Mhe. Waziri Balozi Pindi  Chana amesema utahudhuriwa na watu mashuhuri wakiwemo Katibu Mkuu wa UNWTO, Mawaziri wa Utalii kutoka nchi Wanachama wa Shirika la Utalii Duniani – Kamisheni ya Afrika na wadau wa utalii kutoka ndani na nje ya Afrika na Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan ambaye anatarajiwa kuwa Mgeni Rasmi.

    “Mkutano huu utahusisha matukio mbalimbali ikiwemo Mkutano wa Mawaziri wa Utalii kutoka nchi wanachama, Jukwaa la Uwekezaji kwa ajili ya kutangaza fursa za uwekezaji zilizopo nchini na  mafunzo kwa wadau wa sekta ya Utalii yaani Marketing Symposium kwa lengo la kuwajengea uwezo wadau wa utalii kuhusu utangazaji Utalii”. Amefafanua  Waziri Chana

    Aidha, kwa kutambua umuhimu wa mkutano huo, Mhe Balozi Dkt. Pindi Chana ametoa rai kwa wadau wote wa utalii hususan wakazi wa Jiji la Arusha na maeneo ya jirani wanaotoa huduma za malazi, mawakala wa biashara za utalii, na waongoza watalii kuonesha ukarimu wa hali ya juu kwa washiriki wa Mkutano wa 65 wa UNWTO – CAF kwa kipindi chote watakachokuwa hapa nchini ili waitangaze vyema Tanzania.

    Akizungumza kwa niaba ya UNWTO, Mkurugenzi wa Shirika la Utalii Duniani Kamisheni ya Afrika Bi. Marie Elicie, amesema wameridhishwa na namna Tanzania  ilivyo jiandaa kwa  mkutano huo wa Kimataifa kuanzia viwanja vya ndege, hoteli na ukarimu kwa watoa huduma.


    No comments:

    Post a Comment

    ZanziNews Copyright © 2014

    Theme images by Bim. Powered by Blogger.