Habari za Punde

Sensa ya watu na makaazi ina mchango mkubwa kwa sekta ya uchumi wa Buluu - Dk Mwinyi

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akizungumza na Wanndishi wa habari wa vyombo mbalimbali vilioko Zanzibar baada ya kumaliza kuhesabiwa katika zoezi la Sensa ya Watu na Makaazi Tanzania lililofanyika  katika makazi yake Migombani Ikulu Ndogo leo 23-8-2022.                                     

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema Sensa ya Watu na Makaazi 2022 ina mchango mkubwa katika kuimarisha  shughuli mbali mbali za sekta ya uchumi wa Buluu hapa nchini.

Dk. Mwinyi amesema hayo nyumbani kwake Ikulu Migombani, Jijini Zanzibar, baada ya kukamilisha zoezi la kuhesabiwa katika Sensa ya Watu na makaazi 2022.

Amesema kupitia sensa, Serikali itaweza kutambua idadi ya watu na shughuli wanazofanya katika Sekta ya Uchumi wa Buluu hatua itakayosaidia mipango ya Serikali katika  uimarishaji wa sekta hizo.

Akiambatana  na mkewe Mama Mariamu Mwinyi , Rais Dk. Mwinyi alitoa wito kwa wananchi wote Unguja na Pemba kushiriki kikamilifu katika zoezi la kuhesabiwa, akibainisha faida kubwa itakayopatikana ya kuliwezesha Taifa kupanga mipango yake ya maendeleo.

Alisema takwimu zitakazopatikana kupitia sense hiyo zitaisaidia Serikali kupanga mipango ya  maendeleo kwa kipindi cha miaka kumi pamoja na kujua mahitaji katika sekta zote, ikiwemo huduma mbali mbali  za kijamii, kama vile maji, elimu, afya  na nyenginezo.

Akiongoza Kaya yake wakati wa kuhesabiwa Dk. Mwinyi aliwatoa khofu wananchi kwa kusema zoezi hilo ni rahisi na lisilotumia muda mwingi.

“Maswali yana lengo la kujua idadi ya watu na shughuli  zao, ni zoezi rahisi, halitumii muda mrefu, maswali yake rahisi, hakuna sababu ya kuwa na khofu”, alisema.

Mapema, Kamisaa wa Sensa na makaazi 2022 Zanzibar, Balozi Mohamed Hamza alisema ana matumaini makubwa kuwa zoezi hilo litakamilika vyema, huku akibainisha taarifa za awali za wananchi kulipokea vizuri zoezi hilo.

Aidha, Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Idrissa Kitwana Mustafa alieleza matarajio yake ya zoezi hilo kupata ufanisi kwa kuzingatia kuwa linafanyika katika mazingira ya amani na usalama pamoja na kuwapongeza watendaji  kwa maandalizi bora  na kuwa na mipango mizuri.

Nae, Mtakwimu Mkuu wa Serikali Salum Kassim Ali mchakato wa kuhesabu watu katika maeneo mbali mbali nchini, ikiwemo kwenye mahoteli, hospitalini,bandarini , maeneo ya visiwa na dago na maeneo mengine umefanyika kikamilifu kwa watendaji na makarani wa Sensa kufika na kufanikisha na kutekeleza kwa ufanisi majukumu yao.

Imetayarishwa na Idara ya Mawasiliano,

IKULU ZANZIBAR

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.