Habari za Punde

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Kassim Majaliwa Ashiriki Ibada ya Kumuaga Marehemu Augustine Lyatonga Mrema leo 24-8-2022

Waziri Mkuu, wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa akitoa heshima za mwisho kwa aliyekuwa Mwenyekiti wa Tanzania Labour Party (TLP) marehemu Augustine Lyatonga Mrema, kwenye Kanisa la Roman Catholic Salasala, jijini Dar es Salaam

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Kassim Majaliwa amesema Serikali itaendelea kumkumbuka Mhe. Augustino Lyatonga Mrema kutokana na mchango wake mkubwa wa kuendeleza mahusiano na vyama vya siasa.

 

“Mheshimiwa Mrema atakumbukwa kama kiongozi mkuu wa Chama cha TLP kwa muda mrefu sana. Na akiwa katika siasa, aliisaidia Serikali kupata mwelekeo mzuri wa vyama vya siasa," amesema Waziri Mkuu.

 

Ametoa kauli hiyo leo mchana (Jumatano, Agosti 24, 2022) wakati akizungumza na mamia ya waombolezaji kwenye ibada ya kumuaga marehemu Mrema katika Parokia ya Mt. Augustino Kilimahewa, Salasala, nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam.

 

Amesema salamu za Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ziliwasilishwa asubuhi na Makamu wa Rais, Mhe. Dkt. Philip Mpango.

 

"Sisi tuliopo hapa tuna mambo mawili makubwa ya kufanya ili kumuenzi ndugu yetu Mrema. Moja ni kuenzi yale yote aliyofanya kwa upande wa Serikali na upande wa siasa lakini pili, tuendelee kumuombea ili Mwenyezi Mungu aweze kuilaza roho yake mahali pema peponi," amesema.

 

Kuhusu mazishi yake yanayotarajiwa kufanyika kesho Alhamisi huko Kiraracha, Moshi, Waziri Mkuu amesema Serikali itawakilishwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu, Mhe. George Simbachawene pamoja na Waziri wa Mambo ya Ndani, Mhe. Hamad Masauni.

 

Akizungumza na niaba ya Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Mkuu wa Utawala wa Jeshi hilo, DCP Anthony Luta alisema Jeshi la Polisi litaendelea kumkumbuka Mhe. Mrema kwa mambo kadhaa ikiwemo hatua yake ya kuanzisha jeshi la ulinzi wa sungusungu, ujenzi wa vituo vidogo vya polisi na utetezi wa haki za wanawake ambapo kwa sasa wameanzisha madawati ya jinsia kwenye vituo vya polisi.

 

Naye Paroko wa kanisa hilo, Padre Peter Assenga alisema Mhe. Mrema alikuwa akijitolea kwa mambo mengi parokiani hapo na ataendelea kukumbukwa sana.

 

Kwa upande wake, Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mhashamu Henry Mchamungu alisema umati mkubwa uliokuwepo kanisani hapo ni ishara tosha ya jinsi Bw. Mrema alivyoishi vizuri na watu wakiwemo viongozi wa Serikali na vyama vya siasa.

 

Ibada hiyo iliongozwa na Askofu mmoja na mapadre sita. Baadhi ya viongozi waliohudhuria ni Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye, Hamad Rashid, Prof. Ibrahim Lipumba, John Cheyo, Steven Wassira, James Mbatia, Joseph Selasini na Mchungaji Dkt. Eliona Kimaro.


Waziri Mkuu ,wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Kassim Majaliwa akizungumza wakati alipohudhuria ibada ya kumuaga aliyekuwa Mwenyekiti wa Tanzania Labour Party (TLP) marehemu Augustine Lyatonga Mrema, iliyofanyika katika Kanisa la Roman Catholic Salasala, jijini Dar es Salaam
Wafiwa na Viongozi wa Siasa wakiwa katika ibada ya kumuaga aliyekuwa Mwenyekiti wa Tanzania Labour Party (TLP) marehemu Augustine Lyatonga Mrema, iliyofanyika katika Kanisa la Roman Catholic Salasala, jijini Dar es Salaam
Wafiwa na Viongozi wa Siasa wakiwa katika ibada ya kumuaga aliyekuwa Mwenyekiti wa Tanzania Labour Party (TLP) marehemu Augustine Lyatonga Mrema, iliyofanyika katika Kanisa la Roman Catholic Salasala, jijini Dar es Salaam.
Waziri Mkuu, wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa akitoa heshima za mwisho kwa aliyekuwa Mwenyekiti wa Tanzania Labour Party (TLP) marehemu Augustine Lyatonga Mrema, kwenye Kanisa la Roman Catholic Salasala, jijini Dar es Salaam.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Waziri Mkuu Mstaafu, Fredrick Sumaye, wakati alipohudhuria ibada ya kumuaga aliyekuwa Mwenyekiti wa Tanzania Labour Party (TLP) marehemu Augustine Lyatonga Mrema, iliyofanyika katika Kanisa la Roman Catholic Salasala, jijini Dar es Salaam, Agosti 24 2022.
 (Picha na Ofisi ya Wziri Mkuu)
 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.