RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema Serikali
itashirikiana kikamilifu na Bodi ya Tume
ya Nguvu za Atomic Tanzania (TAEC) ili kuweza kukamilisha vyema majukumu yake.
Dk. Mwinyi amesema hayo Ikulu Zanzibar alipokutana na ujumbe kutoka Bodi ya Tume ya Nguvu za Atomic Tanzania, uliofika kwa ajili ya kuelezea utekelezaji wa majukumu ya Tume hiyo.
Alisema Serikali kupitia Wizara ya Afya, itahakikisha Tume hiyo inatekeleza kikamilifu majukumu yake hapa Zanzibar na akatumia fursa hiyo kuipongeza kwa kazi kubwa na nzuri inayofanya.
Akigusia baadhi ya mafanikio na changamoto yanayoikabii TAEC katika utekelezaji wa majukumu yake, Dk. Mwinyi aliipongeza kwa kuwa na uharaka katika utoaji wa vibali, ikilinganishwa na taasisi nyingine za Muungano, huku akibainisha kuwepo kwa urasimu katika taasisi nyingi za Serikali.
Aidha, aliishukuru TAEC kwa udhibiti mzuri wa mionzi na kusema ni suala muhimu sana kwa Afya ya wananchi.
Katika hatua nyengine, Dk. Mwinyi alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itatoa msukumo kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili kuona masuala mbali mbali, ,ikiwemo ufinyu wa bajeti na upungufu wa wafanyakazi unaokabili taasisi hiyo hapa Zanzibar yanapatiwa ufumbuzi.
Alieleza kuwa Serikali itafuatilia kuhakikisha eneo la mradi wa ujenzi wa majengo ya TAEC katika eneo la Dunga Duze, Wilaya Kati Unguja linaongezwa ili kukidhi mahitaji ya taasisi hiyo.
Aidha, alisema Serikali kupitia Wizara ya Ardhi itaangalia uwezekano wa kupunguza gharama za tozo la ada ya kiwanja ya shilingi Milioni 2.5 kwa mwaka, pamoja na kuahidi kusaidia ujenzi wa barabara ya ndani yenye urefu wa kilomita 2.5 inayotoka barabara kuu hadi eneo la mradi, akibainisha hatua hiyo itabadili mazingira ya eneo hilo.
Nae, Waziri wa Afya Ahmeid Nassor Mazrui aliipongeza Bodi hiyo kwa utekelezaji mzuri wa majukumu yake hapa Zanzibar, hususan katika suala la uingizaji wa bidhaa kutoka Tanzania Bara, kwa kutambua kuwa Zanzibar ni sehemu ya Muungano, tofauti ilivyo kwa taasisi nyingie za Muungano.
Mapema, Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Tume ya Nguvu za Atomic Tanzania (TAEC) Pro. Lazaro Simon Petro alisema TAEC inaendelea na mradi mkubwa wa ujenzin wa majengo mbali mbali hapa Zanzibar katika eneo la Dunga Zuze, unatarajiwa kugharimu zaidi ya shilingi Bilioni 3.03.
Alisema ujenzi huo utakaohusisha maabara mbali mbali umefikia kiwango cha asilimia 35 hivi sasa, ukifanyia katika eneo la ardhi lenye ukubwa wa kilomita za mraba 7,314 na kuishukuru Serikali kwa kuipatia Bodi eneo hilo, ingawaje bado haitoshelezi mahitaji.
Alisema TAEC imepata mafanikio makubwa katika masuala mbali mbali hapa Zanzibar, ikiwemo utoaji wa vibali, ambapo kabla ilikuwa vikitolewa baada ya siku saba na hivi sasa hutolewa ndani ya siku moja.
Aidha, Mkurugenzi huyo akatumia fursa hiyo kuipongeza TAEC kwa kufanikiwa kutokomeza Mbung’o katika mradi uliofanyika hapa zanzibar mnamo mwaka 1995.
Alisema miongoni mwa changamoto inazoikabili TAEC ni uhaba wa wafanyakazi, ambapo kwa wastani wanahitajika wafanyakazi 20 na hivyo akatumia fursa hiyo kuiomba Serikali kibali cha kuajiri.
Imetayarishwa na Idara ya Mawasiliano
Ikulu Zanzibar.
No comments:
Post a Comment