Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Fedha na Mipango Zanzibar, Mhe. Dkt. Saada Salim Mkuya akizungumza wakati Mkutano wa Majadiliano ya Kimkakati kati ya Serikali na Washirika wa Maendeleo uliofanyika katika Hotel ya Seaclif, Zanzibar.
Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango na Mwenyekiti wa Mkutano wa Majadiliano ya Kimkakati kati ya Serikali na Washirika wa Maendeleo, Bw. Emmanuel Tutuba (Kulia) akiongoza mkutano huo uliofanyika katika Hotel ya Seaclif, Zanzibar, kushoto ni Mwenyekiti Mwenza wa Washirika wa Maendeleo nchini, Bw. Zlatan Milisic.
Meza kuu ikiongozwa na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Othman Masoud Othman wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya mabalozi na wawakilishi wa mabalozi wa nchi mbalimbali walioshiriki Mkutano wa Majadiliano ya Kimkakati kati ya Serikali na Washirika wa Maendeleo uliofanyika katika Hotel ya Seaclif, Zanzibar.
Na Farida Ramadhan -WFM, Zanzibar
Serikali imewahimiza washirika wa maendeleo kushiriki katika kuwezesha nchi kufufua fursa zote za kiuchumi zilizozuiwa na kuharibiwa na athari za Uviko- 19 pamoja na vita inayoendelea baina ya Urusi na Ukraini.
Wito huo umetolewa na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Othman Masoud Othman wakati akifungua Mkutano wa Majadiliano ya Kimkakati kati ya Serikali na Washirika wa Maendeleo uliofanyika katika Hotel ya Seaclif, Zanzibar.
Alisema Serikali inatambua michango mbalimbali iliyotolewa na washirika hao lakini bado inahitaji ushirikiano wao katika kuiwezesha nchi kufikia malengo yake.
“Wote tunajua uchumi wa Dunia kwa mwaka 2022, umetikiswa na vita baina ya Urusi na Ukraini, hii imetokea katika kipindi ambacho nchi nyingi duniani zilikua zimeanza kuimarika kutoka katika janga la korona, Tanzania Bara na Zanzibar pia ni miongoni mwa nchi zilizoathirika kwa kuwa inategemea wawekezaji na ushirikiano wa wadau wa maendeleo”, alisema Mhe. Othman Masoud Othman.
Kwa upande wake Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango Zanzibar, Mhe. Dkt. Saada Salim Mkuya alisema pamoja na mambo mengine mkutano huo utajadili namna ya kuiwezesha nchi kutumia rasilimali zilizopo kwa ajili ya kukuza uchumi.
Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango ambaye ni Mwenyekiti wa Mkutano huo, Bw. Emmanuel Tutuba aliwataka washirika wa maendeleo kuendelea kuunga mkono juhudi za Serikali katika kutekeleza sera mbalimbali za kiuchumi kwa maendeleo endelevu.
Alisema Serikali inatambua na kuthamini michango yao kwa kuwa anaamini mafanikio na maendeleo ya uchumi yanategemea michango yao na matokeo ya majadiliano hayo yataiwezesha nchi kufikia malengo yake ya ukuaji uchumi.
Alisema mada zinazojadiliwa katika mkutano huo wa siku mbili ni pamoja na uchumi wa taifa kwa ujumla na masuala ya mazingira kwa kuangalia changamoto ya kimazingira na tabia ya nchi.
Kwa upande wake Mwenyekiti Mwenza wa Washirika wa Maendeleo nchini, Bw. Zlatan Milisic alisema washirika wa maendeleo wataendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika majadiliano yanayo hamasisha uwazi na uawajibikaji kwa maendeleo ya Watanzania.
Aliipongeza Serikali kwa kufanikisha zoezi la Sensa ya Watu na Makazi ambalo matokeo yake yatatumika kwa maendeleo ya kiuchumi.
Alisema washirika wa maendeleo pia wanaipongeza Serikali kwa kuwa na uongozi bora unao zingatia haki za binadamu pamoja na jitihada mbalimbali izozichukua kuboresha maendele ya kiuchumi na kijamii.
No comments:
Post a Comment