Waziri wa Nchi Ofisi
ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo akiwasilisha Taarifa
ya hatua zilizofikiwa katika kuhuisha Sheria ya Hifadhi
ya Mazingira, Sura 191 kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira katika
ukumbi wa Ofisi za Bunge jijini Dodoma leo Septemba 07, 2022.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo amesema azma ya Serikali si ya kufungia viwanda badala yake imejikita katika kutoa elimu ili wawekezaji wafuate Sheria ya Mazingira.
Amesema hayo wakati akiwasilisha Taarifa ya hatua zilizofikiwa katika kuhuisha Sheria ya Hifadhi ya Mazingira, Sura 191 kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira katika ukumbi wa Ofisi za Bunge jijini Dodoma leo Septemba 07, 2022.
Miongoni mwa masuala muhimu yaliyobainishwa yanayohitaji maboresho katika utekelezaji wa Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ni pamoja na Baraza la Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kupewa hadhi ya Mamlaka.
Dkt. Jafo alisema ili nchi iendelee inahitaji wawekezaji hivyo kama kuna viwanda vinachafua mazingira Ofisi ya Makamu wa Rais inavielekeza kurekebisha changamoto hizo ili uzalishaji uendelee.
“Ni kweli tunabaini baadhi ya viwanda kuchafua mazingira kwa njia ya hewa au majitaka lakini sisi kama Serikali hatukimbilii kuvifungia viwanda lakini tunachukua hatia ya kutoa elimu kwani kufungia viwanda kunasababisha watu wakose ajira na Serikali kukosa mapato kutokana na kodi,” alisema.
Akijibu hoja za wajumbe wa kamati hiyo, Waziri Jafo alisema alisema katika kutekeleza kazi ya kuhuisha Sheria ya Hifadhi ya Mazingira, Sura 191 zipo kazi zilizofanyika ambazo ni kuifanyia uchambuzi Sera ya Taifa ya Mazingira ya Mwaka 2021 ili kubainisha masuala mapya yaliyojitokeza katika Sera mpya.
Alisema kuwa
masuala muhimu yaliyobainishwa yanayohitaji
maboresho katika utekelezaji wa Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ni pamoja na mabadiliko ya tabianchi kwa kuimarisha
ushiriki wa sekta binafsi, uhawilishaji wa teknolojia na upatikananaji wa
rasilimali fedha.
Pia alisema kuwa masuala mengine ni kuanzishwa kwa
Kituo cha Kuratibu Hewa Ukaa Nchini na udhibiti wa biashara ya hewa ukaa ambayo
mwongozo wake upo katika maandalizi.
Aidha, Waziri Jafo alisema uchafuzi wa mazingira umebainishwa
kwa usimamizi wa kemikali katika hatua zote (life-cycle) na hifadhi ya
mazingira katika shughuli za sekta ya gesi na mafuta.
Sheria ya Hifadhi ya Mazingira, Sura 191 ilitungwa Mwaka 2004 kufuatia Sera ya Taifa ya Mazingira ya mwaka 1997. Sheria hii imekuwa ikifanyiwa marekebisho mbalimbali ili kuendana na wakati na kwa kuzingatia kwamba masuala ya mazingira ni mtambuka na ambayo yamekuwa yakibalidilika kulingana na wakati.
Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na
Mazingira ndio inayosimamia Sheria hiyo na ndani ya Sheria hiyo Waziri wa Nchi
Ofisi ya Makamu wa Rais amepewa mamlaka ya kutunga kanuni kwa ajili ya
utekelezaji wa Sheria ya Hifadhi ya Mazingira, Sura 191.
Hivyo, kutokana na ukweli kwamba Sheria hiyo ni ya muda mrefu ipo haja ya kuihuisha ili iweze kuendana na wakati.
No comments:
Post a Comment