Habari za Punde

Maadhimisho ya Baraza la Maulid Zanzibar Lafanyika Ukumbi wa Hoteli ya Golden Tulip Uwanja wa Ndege Kiembesamaki Unguja Jijini Zanzibar.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Alhajj Hemed Suleiman Abdulla  akizungumza na wananchi kwa niaba ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa baraza la Mapinduzi Alhajj Dkt. Hussen Ali Mwinyi katika  Baraza la Maulid Zanzibar lililofanyika Ukumbi wa Hotel ya Golden Tulip Uwanja wa Ndege jijini Zanzibar leo. Tarehe 09.10.2022
Wananchi wa Zanzibar wakishiriki katika Baraza la Maulid Zanzibar lililofanyika katika ukumbi wa Hoteli ya Golden Tulip Uwanja wa Ndege Kiembesamaki Wilaya ya Magharibi "B" Unguja Jijini Zanzibar.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhajj Dkt. Hussein Ali Mwinyi amepongeza kuanzishwa kwa Baraza la Maulid Zanzibar na kueleza kuwa Baraza hilo litakuwa chachu Ya kurejesha Maadili Nchini.

Alhajj Dkt. Mwinyi ameeleza hayo katika Hotuba  iliyosomwa kwa Niaba yake na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Alhajj.Hemed Suleiman Abdulla  wakati akihutubia katika  Baraza la Maulid Zanzibar lililofanyika Ukumbi wa Hotel ya Golden Tulip Uwanja wa Ndege jijini Zanzibar.

Amesema Ofisi ya Mufti Mkuu wa Zanzibar kwa kushirikiana na Taasisi ya Zanzibar Relief and Development Foundation (ZARDEFO) imekuja na wazo la kuanzisha kwa Baraza hilo ambapo litakuwa na kazi ya kuchambua mwenendo wa Maisha ya Mtume Muhammad (S.A.W) kwa lengo la kuhakikisha  kizazi cha sasa na cha baadae kinaiga kuiga Mwenendo Mzima na Kiongozi huyo wa Umma huu.

Ameeleza kuwa Sherehe za Mazazi ya Mtume Muhammad (S.A.W) zimefanywa na wanazuoni waliopita katika Visiwa vya Zanzibar kwa kufundisha na kusimamia Maadili na Nidhamu ya Uislamu katika Hafla hizo.

Alhajj Dkt.Mwinyi ameeleza kusikitishwa kwake na baadhi ya Madrasa kutozingatia Maadili katka hafla zao na kueleza kuwa Baraza hilo litaweza kueleza namna bora ya usomaji wa Maulid ikiwemo Mavazi, upigaji wa Dufu na mengineyo.

Aidha ameeleza kuwa ili kurejesha maadili ya Maulid Zanzibar ni vyema baraza hilo kutoa maelekezo na  miongozo kwa kuwatumia wanazuoni wa ndani na nje ya Zanzibar.

Katika hatua nyengine Rais wa Zanzibar  ametumia Fursa hiyo kuwataka Waumini kupitia Baraza la Maulid Zanzibar kukemea matendo maovu yaliyokithiri katika jamii kama vile Ulevi, Wizi , Ubadhilifu wa Mali za Umma, Udhalilishaji  wa Wanawake na watoto Madawa ya kulevya na yale yote yanayofanana na hayo.

"Baraza hili la Maulid litasaidia sana sio tu kusimamia taratibu za Shughuli za Maulid hapa Zanzibar bali pia ni Fursa nyengine ya kushirikiana zaidi katika kukemea matendo yote maovu yaliyokothiri katika Jamii yetu kama vile ulevi, Wizi wa Mazao ubadhirifu wa Mali za Umma, udhalilishaji wanawake na watoto” amesema

Nae waziri wa Nchi Afisi ya Rais Katiba Sheria Utumishi na Utawala Bora Mhe. HAROUN ALI SULEIMAN ameitaka bodi ya Baraza la Maulid kusambaza taarifa kama hizi za kidini nchi nzima na kuishauri kulifanya baraza kama hili mwakani katika kisiwa cha Pemba ili kupata manufaa zaidi.

Aidha waziri Haroun ameipongeza kamati ya maandalizi kulisimamia jambo hili muhimu katika nchi yetu kwa lengo la kuyarejesha yale yote yaliofanywa na wanazuoni waliopita katika kuadhimisha mazazi ya mtume Muhammad (S.A.W) katika nchi yetu.

Pia amewapongeza viongozi wa ngazi za juu serikalini kuanzisha utamaduni wa kuwa na wananchi katika shuhuli mbali mbali za kijamii.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Tamasha la Maulid Zanzibar Sheikh.Hassan Othman Ngwali amesema lengo kuu la tamasha hili ni kuielimisha jamii katika mambo mema kwa maslahi ya taifa na kumridhisha Allah (S.W)

Sheikh.Ngwali amesema kuwa baraza litahakikisha linasimamia vya kutosha mambo yote ambayo hayaendani na matakwa Mwenyezi mungu hasa katika shuhuli za maulid ya kumsifu Mtume Muhammad ( S.A.W) na kuhakikisha yanarejea yale yote waliyoyafanya wanazuoni waliopita katika kuazimisha kuzaliwa kwa mtume na kufanya yote yanayomrizisha Allah (S.W) kwa maslahi ya vizazi vya sasa na vya baadae.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.