Habari za Punde

Sikitu wa Habari Hana Mpinzani SHIMIWI

 

Mashindano ya Michezo ya SHIMIWI ikiendelea Mkoani Tanga kwa michezo mbalimbali kwa washiriki ukiwemo mchezo wa Draft kama wanavyooneka washiriki wakiendelea kuoneshana ufundi wa mchezo huo. 

Na Mwandishi Wetu, Tanga

MCHEZAJI Niuka Chande almaarufu Sikitu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari  amedhihirisha hana mpinzani katika mchezo wa draft kwenye mashindano ya Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI) baada ya kutokufungwa mchezo wowote kuanzia hatua ya makundi hadi kutwaa ubingwa kwa upande wa wanawake uliofanyika katika ukumbi wa Bwalo la Maafisa wa Polisi jijini Tanga.

Huu ni ubingwa alioupata miaka miwili mfululizo, ambapo katika mchezo wa fainali Niuka alimfunga Mizowa Kiemena wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Ujenzi) kwa pointi 4-2, huku ushindi wa tatu umechukuliwa na Pulkeria Maimu wa Tume ya Utumishi wa Walimu aliyemfunga Sophia Mpema wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).

Kwa upande wa wanaume, mchezaji Jihadhari Said wa Ofisi ya Waziri Mkuu Sera amemgaragaza Masoud Simba wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na kutwaa ubingwa; naye Juma Mohamed wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo  kamshinda James King wa Wizara ya Kilimo na kutwaa ushindi wa tatu.

Wakati huo huo, timu ya netiboli ya Ofisi ya Rais Ikulu wamewafunga Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa magoli 59-32 katika mchezo wa nusu fainaili uliofanyika kwenye uwanja wa Bandari.

Katika mchezo mwingine uliokuwa wa kuvutia timu ya Wakala wa Hifadhi ya Taifa ya Chakula (NFRA) waliwafunga Ofisi ya Bunge kwa magoli 60-33.

Katika mchezo wa kuvuta Kamba wanawake timu ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Uchukuzi) wamewavuta Wizara ya Maji kwa mivuto 2-0 katika mchezo wa nusu fainali uliofanyika uwanja wa Shule ya Sekondari ya Usagara; wakati Idara ya Mahakama waliwashinda Ofisi ya Waziri Mkuu Sera kwa mivuto 2-0.

Kwa upande wa wanaume Ofisi ya Rais Ikulu imewavuta bila huruma Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa mivuto 2-0 na kuingia hatua ya fainali, ambapo wataungana na Idara ya Mahakama waliowavuta Wizara ya Mambo ya Ndani kwa mvuto 2-0.
No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.