Habari za Punde

Dk.Hussein Mwinyi Ameridhishwa na Hatua Zilizofikiwa Ujenzi wa Hospitali ya Mkoa wa Mjini Magharibi Lumumba

 

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akizungumza na Waandishi wa habari wa vyombo mbalimbali vilioko Unguja baada ya kumaliza ziara yake kutembelea na kukagua ujenzi wa jengo jipya la Hospitali ya Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja leo 19-11-2022, na (kulia kwa Rais) Waziri wa Afya Zanzibar Mhe.Nassor Ahmed Mazrui na Naibu Waziri wa Afya Zanzibar Mhe. Hassan Khamis Hafidh

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi   Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema ameridhishwa na hatua zilizofikiwa za ujenzi katika  Hospitali mpya ya Mkoa wa Mjini Magharibi, inayoendelea kujengwa katika eneo la  Lumumba.

Dk. Mwinyi amesema hayo leo katika ziara fupi alipotembelea Hospitali hiyo ili kuangalia maendeleo ya ujenzi wake.

Akizungumza na Viongozi, watendaji na wananchi walioshiriki katika  ziara hiyo Dk. Mwinyi alisema amefurahishwa na kasi ya Mkandarasi anaendeleza mradi huo, ambapo hadi sasa hatua za ujenzi zimefikia asilimia 69 ya kazi yote.

Alisema kuna kila sababu ya kujivunia kwa uwepo wa Hospitali hiyo ambayo ni ya  aina yake hapa Zanzibar.

Alisema  Serikali ina matarajio  makubwa kuwa Hospitali hiyo itakamilika ujenzi wake na kuanza kutumika ifikapo mwezi Aprili 2023 , na kuwa Hospitali mbadala katika kuendeleza tiba na kupisha ukarabati mkubwa unaotarajiwa kufanyika katika Hospitali ya Rufaa ya Mnazi Mmoja.

Aidha , alibainisha  azma ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya kuhakikisha kila Mkoa hapa nchini unakuwa na Hospitali  ya aina hiyo.

Wakati huo huo,  Dk. Mwinyi aliwatoa khofu wajasiriamali wanaojihusisha na kazi za kutengeneza vyombo vya moto ambao wamelazimika kusimamisha shughuli zao na kuhama eneo hilo ili kupisha ujenzi wa Hospitali hiyo.

Aliwathibitishia Wajasiriamali hao kuwa  tathmini kwa ajili ya  malipo yao tayari imefanyika na wanatarajiwa kulipwa katika kipindi kifupi kijacho.

Aidha, aliwawahikishia kuwekewa miundombinu muhimu katika sehemu yao mpya kazi  

Mapema, Waziri wa Afya Nassor Ahmed Mazrui alielezea  maendeleo ya Kazi za ujenzi wa Hospitali hiyo na kusema kabla Hospitali hiyo ilitarajiwa kukamilika ujenzi wake mnamo mwezi Januari 2023 , lakini kutokana na  changamoto ya kuibuka kwa Ugonjwa wa Covid – 19, baadhi ya vifaa vilivyotarajiwa kutumika  vilichelewa kufika nchini. Hata hivyo akabainisha kuwa tayari mahitaji mengi ya vifaa yameshakamilika.

 Imetayarishwa na Idaya ya Mawasiliano

Ikulu Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.