Habari za Punde

Serikali Yawasilisha Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka 2023/24

Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) akiwasilisha Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleowa Taifa kwa Mwaka 2023/24, bungeni jijini Dodoma.
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb) akiwasilisha hati ya Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleowa Taifa kwa Mwaka 2023/24, bungeni jijini Dodoma.
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) akiteta jambo na Waziri wa Madini, Mhe. Dotto Biteko, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Mhe. George Simbachawene pamoja na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mhe. Dkt. Eliezer Feleshi kabla ya kuwasilisha Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleowa Taifa kwa Mwaka 2023/24, bungeni jijini Dodoma.

Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba akiteta jambo na Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe. Antony Mavunde kabla ya kuwasilisha Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleowa Taifa kwa Mwaka 2023/24, bungeni jijini Dodoma.

Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Hamad Hassan Chande akisalimiana na baadhi ya wakuu wa Idara na Maafisa wa Wizara hiyo baada ya kuwasilisha Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleowa Taifa kwa Mwaka 2023/24, bungeni jijini Dodoma.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Mhe. George Simbachawene akiteta jambo na baadhi ya wakuu wa Idara na Maafisa wa Wizara hiyo baada ya kuwasilisha Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleowa Taifa kwa Mwaka 2023/24, bungeni jijini Dodoma.

(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini – WFM, DODOMA)

1.0       UTANGULIZI

1.          Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja kwamba, Bunge lako Tukufu likae kama Kamati ya Mipango ili kupokea na kujadili Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka 2023/24.

 2.    Mheshimiwa Spika, awali ya yote napenda kutumia fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuendelea kutujalia uhai na afya njema na kutuwezesha kukutana ili kuwasilisha na kujadili Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka 2023/24.

 3.          Mheshimiwa Spika, naomba nimpongeze kwa dhati Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,  ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, kwa uongozi wake mahiri katika kuendelea kuwatumikia watanzania kwa kusimamia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo na kuboresha huduma za jamii kama ilivyoainishwa katika Ilani ya CCM ya Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2020.  Aidha, napenda kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor Mpango, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa busara, hekima na weledi katika kazi zake za kumsaidia na kumshauri Mheshimiwa Rais kuongoza Taifa letu. Napenda pia kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Hussein Ally Mwinyi, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa uongozi wake Bora na utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi mzuri na dhamira ya dhati ya kuwaletea Wazanzibar maendeleo ya kweli. Vile vile, nampongeza Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa mbunge wa jimbo la Ruangwa - Lindi, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Kiongozi wa shughuli za Serikali Bungeni kwa uongozi wake hodari ndani ya Serikali na hapa Bungeni pamoja na  kumsaidia Mheshimiwa Rais kufuatilia kwa ukaribu utekelezaji wa Mpango na Bajeti na ahadi zilizomo katika Ilani ya CCM ya Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2020.

 4.          Mheshimiwa Spika, naomba nitumie fursa hii kukupongeza wewe Mheshimiwa Spika pamoja na Naibu Spika kwa kuendelea kuliongoza Bunge letu kwa weledi. Naomba nitumie fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Jaji Mkuu wa Makama ya Tanzania na mhimili mzima wa utoaji wa haki kwa kazi nzuri wanayoifanya na pongezi za pekee ziwaendee vyombo vya Ulinzi na Usalama vikiongozwa na Jenerali Jacob John Mkunda, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama kwa kuendelea kusimamia imara ulinzi na Usalama wa Nchi na kuwezesha shughuli zote za maendeleo hapa Nchini kufanyika. Aidha, nitumie fursa hii kuishukuru Kamati ya Kudumu ya ya Bunge ya Bajeti chini ya Mwenyekiti wake Mheshimiwa Sillo Daniel Baran, Mbunge wa Babati Vijijini (CCM) na  Makamu Mwenyekiti Mheshimiwa Omari Mohamed Kigua, Mbunge wa Kilindi (CCM) kwa maoni na ushauri wakati wa vikao vya kamati. Maoni na ushauri wa Kamati ulizingatiwa katika kuboresha Mapendekezo ya Mwongozo  wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka 2023/24 ninayowasilisha katika Bunge hili leo.

 5.          Mheshimiwa Spika, napenda kutoa shukrani zangu za dhati kwa Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mheshimiwa Hamad Hassan Chande (Mb), Mheshimiwa Jaji Dkt. Eliezer Feleshi Mwanasheria Mkuu wa Serikali na timu yake, watendaji wote wa Wizara ya Fedha na Mipango wakiongozwa na Katibu Mkuu, Bw. Emmanuel Mpawe Tutuba kwa ushirikiano walionipa katika maandalizi ya hotuba hii, vitabu vya Mapendekezo ya Mpango na Mwongozo pamoja na utekelezaji wa majukumu yangu. Aidha, ninawashukuru sana Wizara, Taasisi, Idara za Serikali, Sekta Binafsi na wadau mbalimbali waliotoa maoni na michango yao katika kukamilisha Mapendekezo ya Mpango na Mwongozo.

6.          Mheshimiwa Spika, Mapendekezo haya yanabainisha juhudi ambazo Serikali  ya Awamu ya Sita inachukua katika kuboresha maisha ya Watanzania kwa: kuimarisha huduma za jamii; kuboresha mazingira ya uwekezaji na biashara nchini ili kuchochea ukuaji wa sekta binafsi na fursa za ajira; kuimarisha uhusiano na ushirikiano wa kimataifa; kuimarisha sekta ya utalii na uwekezaji kwa kuendelea kutangaza vivutio vya utalii na uwekezaji kupitia Royal Tour; kuweka msukumo katika kuimarisha sekta za uzalishaji na zile zinazotoa ajira kwa vijana wengi kama utamaduni, sanaa na michezo na kuongeza kasi ya kufufua uchumi; na kuimarisha ulinzi na usalama ndani ya nchi na katika mipaka yote ya nchi. Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti yanayowasilishwa yameainisha masuala muhimu ya kuzingatiwa na Maafisa Masuuli wa Wizara, Idara Zinazojitegemea, Wakala wa Serikali, Sekretarieti za Mikoa, Mamlaka za Serikali za Mitaa, Taasisi na Mashirika ya Umma wakati wa kuandaa, kutekeleza, kufuatilia, kutathmini na kutoa taarifa za utekelezaji  wa Mipango na Bajeti za Mafungu yao ili kufikia malengo ya kiuchumi na kijamii yaliyobainishwa katika vipaumbele vya Taifa. Aidha, katika kitabu cha Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa, tunawasilisha mapendekezo ya vipaumbele vya Serikali katika mwaka 2023/24.

7.          Mheshimiwa Spika, Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka 2023/24 yameandaliwa kwa kuzingatia Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (2021/22 – 2025/26) na Ilani ya CCM ya Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2020. Aidha, Mapendekezo haya yamezingatia mafanikio na changamoto zilizojitokeza katika utekelezaji wa Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali pamoja na Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2021/22 na katika robo ya kwanza ya mwaka 2022/23.

8.          Mheshimiwa Spika, Mapendekezo haya yameainisha masuala mbalimbali ikiwemo: Mapitio ya utekelezaji wa Mpango na Bajeti kwa mwaka 2021/22 na robo ya kwanza ya mwaka 2022/23; mwenendo na mwelekeo wa hali ya uchumi; makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka 2023/24; maeneo ya vipaumbele vya Mpango na Bajeti kwa mwaka 2023/24; vihatarishi vya ukuaji wa uchumi na utekelezaji wa mpango na bajeti na mikakati ya kukabiliana navyo; na maelekezo yanayotakiwa kuzingatiwa na Maafisa Masuuli wakati wa uandaaji, utekelezaji, ufuatiliaji na tathmini ya mpango na bajeti kwa mwaka 2023/24.

2.0       MAPITIO YA UTEKELEZAJI WA MPANGO NA BAJETI

2.1      Mwenendo wa Viashiria vya Uchumi

9.          Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2021, Pato la Taifa lilikua kwa wastani wa asilimia 4.9 ikilinganishwa na asilimia 4.8 mwaka 2020. Aidha, katika kipindi cha nusu ya kwanza ya mwaka 2022 (Januari hadi Juni), uchumi ulikua kwa asilimia 5.2 ikilinganishwa na asilimia 4.4 katika kipindi kama hicho mwaka 2021. Kuimarika kwa kasi ya ukuaji wa uchumi kulitokana na: utekelezaji wa Ilani ya CCM ya Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2020 pamoja na uwekezaji uliofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa CCM Taifa, hususan katika miundombinu ya afya, elimu, nishati, maji, ujenzi, barabara za mijini na vijijini, sanaa, michezo na utamaduni, biashara ndogondogo na shughuli za kiuchumi zilizotokana na ongezeko la mikopo katika sekta binafsi; uchimbaji wa madini; na utawala bora unaozingatia misingi ya sheria.

10.       Mheshimiwa Spika, mwaka 2022, kiwango cha ukuaji wa uchumi wa dunia kinatarajiwa kupungua kufikia asilimia 3.2 kutoka ukuaji halisi wa asilimia 6.1 mwaka 2021. Hali hii inatokana na changamoto zinazoukumba uchumi wa dunia ikiwemo vita inayoendelea nchini Ukraine sambamba na mabadiliko ya tabianchi yaliyopelekea kuwepo kwa ukame na upungufu wa chakula. Pamoja na mwenendo mzuri wa uchumi wa Taifa katika nusu ya kwanza, hali inayoukumba uchumi wa dunia kwa sasa  itaathiri pia uchumi wa Tanzania katika nusu ya pili. Hivyo, kufuatia mwelekeo na mwingiliano wa uchumi wa dunia, kiwango cha jumla cha ukuaji wa uchumi wa Tanzania kinatarajiwa kupungua kufikia wastani wa asilimia 4.7 mwaka 2022 kutoka ukuaji halisi wa asilimia 4.9 mwaka 2021. Hata hivyo, makadirio haya ni zaidi ya wastani wa ukuaji wa nchi za Afrika zilizo Kusini mwa Jangwa la Sahara wa asilimia 3.8 mwaka 2022.

11.       Mheshimiwa Spika, Kwa mwaka 2023 ukuaji wa uchumi unatarajiwa kuanza kuongezeka kufikia makadirio ya asilimia 5.3. Maoteo ya ukuaji wa uchumi wa Tanzania yamezingatia hatua zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali ya Awamu ya Sita ya Chama cha Mapinduzi inayoongozwa na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kukabiliana na athari zitokanazo na vita inayoendelea nchini Ukraine ikiwemo: uimarishaji wa sekta za uzalishaji ambapo bajeti ya kilimo, mifugo na uvuvi zimeongezeka kwa kiasi kikubwa; uimarishaji wa miundombinu ya barabara mijini na vijijini pamoja na nishati na maji; uboreshaji wa huduma za jamii; utekelezaji wa miradi inayochachua shughuli za uchumi; na uboreshaji wa mazingira ya biashara na uwekezaji.   

12.       Mheshimiwa Spika, mfumuko wa bei uliongezeka katika nchi nyingi duniani kutokana na athari za vita nchini Ukraine. Kwa mujibu wa taarifa ya IMF ya mwezi Julai 2022, mfumuko wa bei wa dunia kwa mwaka 2021 uliongezeka na kufikia wastani wa asilimia 4.7, ikilinganishwa na asilimia 3.2 mwaka 2020.  Aidha, mfumuko wa bei duniani kwa mwaka 2022 unatarajiwa kuendelea kuwa juu kufikia wastani wa asilimia 8.3. Kwa upande wa hapa nchini mfumuko wa bei ulifikia wastani wa asilimia 4.0 katika mwaka ulioishia Juni, 2022 ambao upo ndani ya lengo la nchi la wastani wa asilimia 3.0 hadi 5.0. Mfumuko wa bei kwa kiasi kikubwa ulichangiwa na athari ya vita inavyoendelea nchini Ukraine ambayo imesababisha kuongezeka kwa bei na gharama za usafirishaji wa bidhaa na huduma kutoka nje, hususan bidhaa za petroli, mafuta ya kula, ngano na mbolea. Kutokana na mfumuko wa bei kumekuwepo na kupanda kwa gharama za maisha duniani kote kwa nchi zilizoendelea, zinazoendelea na nchi masikini.

13.        Mheshimiwa Spika, Hata hivyo katika kukabiliana na athari hizo, Serikali ya Awamu ya Sita ya Chama cha Mapinduzi inayoongozwa na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayowajali wananchi wake inaendelea kuchukua hatua mbalimbali zikiwemo: kutoa ruzuku ya bidhaa za mafuta (Fuel) ambapo takriban shilingi bilioni 100 kila mwezi zimekuwa zikitolewa kushusha bei ambapo bei za mafuta kwa Tanzania ziko chini ikilinganishwa na nchi nyingi za jirani, (Yaani Serikali ya Chama cha Mapinduzi inayoongozwa na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan inamlipia mwananchi takriban shilingi 500 kwenye kila lita ya mafuta yanayotumika katika shughuli mbalimbali); kutoa ruzuku kwenye  pembejeo za kilimo (mbolea, mbegu bora) ambapo takriban shilingi bilioni 150 zimetolewa kama ruzuku na kupunguza bei za mbolea kwa zaidi ya nusu ya bei iliyokuwepo (Yaani Serikali ya Chama cha Mapinduzi inayoongozwa na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan inamlipia nusu ya bei kila mwananchi anapotumia mbolea); kutoa  ruzuku kwa bidhaa muhimu kama mafuta ya kula na unga wa ngano kwa kufuta kodi na tozo kwenye bidhaa hizo(Yaani Serikali ya Chama cha Mapinduzi inayoongozwa na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan inamlipia kila mtumiaji wa mafuta ya kula na unga wa ngano  kwa kufuta kodi na tozo zote zilizotakiwa kulipiwa kwenye bidhaa hizo), lengo ni kushusha bei ya bidhaa hizo halikadhalika kwa bidhaa za mbolea zinazozalishwa nyumbani.

14.       Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka ulioishia Juni 2022, mikopo chechefu ilipungua kufikia asilimia 7.8 ya mikopo yote kutoka asilimia 9.3 kwa mwaka ulioishia Juni 2021; na mikopo kwa sekta binafsi ilikua kwa asilimia 19.4 ikilinganishwa na asilimia 3.6 katika kipindi kama hicho mwaka 2021. Kuongezeka kwa mikopo kwa sekta binafsi kulitokana na sera madhubuti za Serikali za kufungua uchumi na kuwezesha ushiriki wa sekta binafsi katika shughuli za biashara na uwekezaji. Hali hii pia ilisaidia wakopaji kuweza kurejesha mikopo yao na hivyo kuongeza utulivu wa sekta ya fedha.

15.        Mheshimiwa Spika, hadi Juni 2022, deni la Serikali lilikuwa shilingi bilioni 71,559.0 kufuatia kuendelea  kupokelewa kwa mikopo na riba za mikopo kwa ajili ya kugharamia miradi ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji, barabara, reli, viwanja vya ndege, umeme, elimu na afya na miradi mingine ya maendeleo. Tathmini ya uhimilivu wa deni (DSA) iliyofanyika Novemba 2021 ilionesha kuwa deni la Serikali limeendelea kuwa himilivu katika muda mfupi, wa kati na mrefu. Aidha, tarehe 7 Octoba 2022 Kampuni ya Moody’s Investors Service ambao ni wabobezi katika masuala ya kupima uhimilivu wa deni duniani walitoa taarifa inayoonesha kuwa mwelekeo wa hali ya uhimilivu wa deni la Tanzania umeimarika (Positive outlook). Kampuni hiyo ilifanya uchambuzi wa athari ya uwezo wa nchi kukopa na kulipa madeni yake kwa nchi mbalimbali duniani, (unsolicited credit rating). Matokeo haya yanatokana na kuwepo kwa viashiria  imara vya uchumi na kuwepo kwa utulivu wa kisiasa nchini na hatua mbalimbali zinazochukuliwa na Serikali ya Awamu ya Sita katika kufungua uchumi na kuvutia mitaji.

16.       Mheshimiwa Spika, akiba ya fedha za kigeni ilifikia dola za Marekani bilioni 5.11 Juni 2022, kiasi ambacho kinatosheleza uagizaji wa bidhaa na huduma nje ya nchi kwa kipindi cha miezi 4.6. Kiwango hiki ni zaidi ya viwango vya kimataifa vya kupima uwezo wa akiba ya fedha za kigeni wa nchi  kukidhi miezi 4.0 ya uagizaji wa bidhaa za nje na zaidi ya lengo la miezi 4.5 kwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.  Akiba ya fedha za kigeni  katika mataifa mengi zimeathiriwa na vita vinavyoendelea nchini Ukraine iliyosababisha kuongezeka kwa gharama za uagizaji wa bidhaa na huduma kutoka nje ya nchi. Sehemu kubwa ya bidhaa zilizoagizwa nje ya nchi zilikuwa za kukuza mitaji na malighafi za viwandani (capital and intermediate goods) kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo (barabara, reli, nishati, maji, afya).

17.       Mheshimiwa Spika, maelezo ya kina kuhusu mwenendo wa viashiria vya uchumi yanapatikana katika Sehemu ya Kwanza, Sura ya Kwanza ya kitabu cha Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2023/24 na Sura ya Kwanza ya Kitabu cha Mapendekezo ya Mpango.

2.2      Utekelezaji wa Mpango na Bajeti

2.2.1         Utekelezaji wa Bajeti ya Mwaka 2021/22

 18.       Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2021/22, Serikali ilikusanya jumla ya shilingi bilioni 36,924.8 kutoka vyanzo vyote, sawa na asilimia 97 ya bajeti iliyoidhinishwa ya shilingi bilioni 37,992.5. Ufanisi wa mapato kwa asilimia 97 ulitokana na jitihada za Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kufuatilia kwa karibu vyanzo vyote vya mapato vya kugharamia bajeti ya Serikali. Kiasi cha mapato yaliyokusanywa kinajumuisha shilingi bilioni 24,395.6 mapato ya ndani; shilingi bilioni 4,825.3 za misaada na mikopo nafuu kutoka kwa Washirika wa Maendeleo; na shilingi bilioni 7,703.9 za mikopo ya kibiashara ya ndani na nje ya nchi. Aidha, Serikali imetumia shilingi bilioni 37,215.8 kugharamia utekelezaji wa bajeti. Kati ya kiasi hicho, shilingi bilioni 22,561.5 ni matumizi ya kawaida na shilingi bilioni 14,654.3 ni matumizi ya maendeleo.

 2.2.2         Utekelezaji wa Bajeti kwa Robo ya Kwanza ya Mwaka 2022/23

19.       Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka 2022/23 mapato ya jumla ya shilingi bilioni 9,100.1 yalikusanywa kutoka vyanzo vyote vya ndani na nje. Kati ya mapato hayo, mapato ya ndani yalikuwa shilingi bilioni 6,211.3 sawa na asilimia 95.0 ya lengo la shilingi bilioni 6,537.1. Mapato ya ndani yalichangia asilimia 68 ya mapato yote yaliyopatikana katika kipindi cha rejea. Katika kipindi hicho, ridhaa ya matumizi ya shilingi bilioni 9,153.9 ilitolewa sawa na asilimia 90.6 ya lengo la shilingi bilioni 10,107.6. Kati ya kiasi hicho, shilingi bilioni 5,848.7 ni ridhaa ya matumizi ya kawaida na shilingi bilioni 3,305.1 kwa ajili ya matumizi ya maendeleo sawa na asilimia 36.1 ya matumizi yote kwa kipindi cha robo mwaka.

 20.       Mheshimiwa Spika, maelezo ya kina kuhusu Utekelezaji wa Mpango na Bajeti ya mwaka 2021/22 na robo ya kwanza ya mwaka 2022/23 yanapatikana katika Sehemu ya Kwanza, Sura ya Pili na Sura tatu mtawalia ya kitabu cha Mwongozo na Sura ya Pili ya Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2023/24.

 2.3      Utekelezaji wa Baadhi ya Miradi ya Maendeleo kwa Mwaka 2021/22 na Robo ya Kwanza ya Mwaka 2022/23

21.       Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2021/22 na robo ya kwanza ya mwaka 2022/23 Serikali iliendelea kutekeleza miradi ya kielelezo na shughuli nyingine katika maeneo ya kipaumbele yaliyobainishwa katika Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2021/22 - 2025/26. Hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wa baadhi ya miradi ni kama ifuatavyo:

(i)          Reli: Ujenzi wa Reli ya Kati kipande cha Dar es Salaam - Morogoro (km 300) umefikia asilimia 97.41 na kipande cha Morogoro - Makutupora (km 422) asilimia 89.07; na kipande cha Mwanza - Isaka (km 341) asilimia 12.53. Aidha, Kipande cha Makutopora - Tabora (km 371) na kipande cha Tabora -Isaka (km 163) tayari vimepata mkandarasi na ufadhili, na kipande cha Tabora - Kigoma (km 514) na Uvinza -Malagarasi kuelekea Msongati (Burundi) – Gitega - Kindu (DRC) viko katika hatua ya kupata makandarasi. Jumla ya shilingi trilioni 1.38 zimetumika katika mwaka 2021/22 na shilingi bilioni 255.42 katika  robo ya kwanza ya mwaka 2022/23;

(ii)         Uboreshaji wa Shirika la Ndege Tanzania (ATCL): Kukamilika kwa malipo ya awali ya ndege tano (5) ambapo ndege nne (4) ni za abiria na ndege moja (1) ni ya mizigo. Jumla ya shilingi bilioni 732.56 zimetumika katika mwaka 2021/22 na shilingi milioni 494.61 katika robo ya kwanza ya mwaka 2022/23. Aidha, mradi mkubwa wa ujenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Msalato unaojumuisha ujenzi wa njia ya kurukia ndege na majengo ya abiria unaendelea chini ya ufadhili wa Benki ya Maendeleo Afrika (AfDB) kwa gharama ya Shilingi Bilioni 360 na uwekaji wa jiwe la msingi umefanywa mwezi Novemba 2022. Ukamilishaji wa taratibu za fedha kwa ajili ya viwanja vya ndege Kigoma, Tabora, Shinyanga na Rukwa zinaendelea.

(iii)         Mradi wa Kufua Umeme wa Maji – Julius Nyerere MW 2,115: Kwa ujumla hadi kufikia Oktoba 2022 utekelezaji wa mradi umefikia asilimia 75. Jumla ya shilingi trilioni 1.273 zimetumika katika mwaka 2021/22 na shilingi bilioni 394.02 katika robo ya kwanza ya mwaka 2022/23;

(iv)       Miradi ya Umeme Vijijini: Kuendelea na usambazaji wa umeme vijijini ambapo vijiji 9,163 kati ya vijiji 12,345 vya Tanzania Bara vimeunganishiwa umeme. Jumla  ya shilingi bilioni 313.40 zimetumika katika mwaka 2021/22 na shilingi bilioni 84.90 katika robo ya kwanza ya mwaka 2022/23;

(v)         Mradi wa Ujenzi wa Bomba la Mafuta Ghafi kutoka Hoima (Uganda) hadi Chongoleani - Tanga (Tanzania) – EACOP: Kukamilika kwa malipo ya fidia katika maeneo 14 yatakayojengwa kambi za wafanyakazi, hifadhi za vifaa na karakana; kuendelea na ujenzi wa kiwanda cha kupaka rangi kwenye mabomba; na kutolewa kwa jumla ya shilingi bilioni 261.33 ikiwa ni sehemu ya malipo ya asilimia 15 ya umiliki wa Serikali katika mradi. Jumla ya shilingi bilioni 224.69 zimetumika katika mwaka 2021/22 na shilingi bilioni 36.63 katika robo ya kwanza ya mwaka 2022/23;

(vi)       Mradi wa Kuchakata na Kusindika Gesi Asilia (LNG) Lindi: Kuendelea na majadiliano ya Mkataba wa Nchi Hodhi (HGA) kati ya Serikali na Wawekezaji kwa kushirikiana na Mshauri Elekezi wa masuala ya sheria, fedha, biashara, uchumi na masoko. Jumla ya shilingi bilioni 3.69 zimetumika katika mwaka 2021/22 na shilingi milioni 963.0 katika robo ya kwanza ya mwaka 2022/23;

(vii)      Ujenzi wa Barabara na Madaraja chini ya Usimamizi wa TANROADS: Kuendelea kuboresha mtandao wa barabara nchini kwa kujenga barabara za mikoa na barabara zinazounganisha Tanzania na nchi jirani na barabara za mijini na vijijini; kukamilika kwa ujenzi wa madaraja ya Tanzanite (Dar es Salaam), Kiyegeya (Morogoro) na Ruhuhu (Ruvuma); na kuendelea na ujenzi wa daraja la Kigongo Busisi (Mwanza) pamoja na barabara unganishi zenye urefu wa km 1.66 ambapo ujenzi umefikia asilimia 47.32, Daraja la Wami (Pwani) na barabara unganishi (km 3.8) asilimia 83 na kuanza kutumika katika kipindi cha uangalizi, daraja la Kitengule (Kagera) na barabara unganishi (km 18) asilimia 95.15 na daraja la Sibiti (Singida) asilimia 95.15.  

Mheshimiwa Spika, kwa ujumla ya miradi 14 yenye urefu wa kilometa 883 imekamilika kati ya Aprili 2021 hadi sasa, yaani ndani ya kipindi cha Awamu ya Sita ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa jumla ya shilingi trilioni 1.37. Pamoja na hayo kuna jumla ya miradi 44 ya barabara yenye urefu wa kilometa 1,523 yenye gharama ya Shilingi Trilioni 3.8 ipo katika hatua mbalimbali za ujenzi nchi nzima.  Vilevile, Miradi 62 ya barabara iko katika hatua mbalimbali za manunuzi kwa ajili ya ujenzi kwa kiwango cha lami. Utekelezaji wa Miradi kwa kutumia utaratibu wa EPC + F mchakato wake umekwishaanza kwa Miradi 8 yenye urefu wa kilometa 2,533 na hatua za kimanunuzi zinaendelea. Aidha, jumla ya miradi 43 ya barabara yenye jumla ya urefu wa kilometa 2,021.04 ipo kwenye hatua mbalimbali za upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa gharama ya jumla ya shilingi bilioni 9.6.

(viii)     Ujenzi wa Barabara na Madaraja Chini ya usimamizi wa TARURA

Aidha, kwa upande wa barabara za vijijini na mijini zinazosimamiwa na Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini (TARURA), mafanikio yaliyopatikana ni pamoja na: kukamilika kwa ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami zenye urefu wa kilometa 275.85, changarawe kilometa 11,120.89, madaraja 596, makalavati na mifereji ya maji ya mvua yenye urefu wa kilometa 67.44; na kufanyika kwa matengenezo ya kawaida ya barabara zenye jumla ya kilometa 25,078.73.

 Mheshimiwa Spika, Jumla ya shilingi trilioni 2.36 zimetumika katika ujenzi wa barabara na madaraja kwa mwaka 2021/22 na shilingi bilioni 670.46 katika robo ya kwanza ya mwaka 2022/23. Kwa kupitia bajeti ya mwaka  2022/23 jumla ya zabuni 1,706 zenye thamani ya shilingi bilioni 621.66 zimetangazwa na Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini ambapo kati hizo Wakala imekwishaingia jumla ya Mikataba 1,246 na Wakandarasi kwa kazi mbalimbali kwa nchi nzima yenye thamani ya Shilingi bilioni 406.21. Kazi za Mikataba hiyo zimeshaanza na zinaendelea na zinahusisha ukarabati, ujenzi na matengenezo ya barabara na madaraja ikiwa ni pamoja na ujenzi wa madaraja makubwa matatu ya Berega (Kilosa) lenye urefu wa Mita 140, Msadya (Mpimbwe-Katavi) lenye urefu wa Mita 60, na Mkomazi (Korogwe) lenye urefu wa Mita 40. Madaraja haya yanaunganisha maeneo yenye uzalishaji mkubwa wa mazao ya kilimo. Zabuni 460 zilizobaki ziko kwenye hatua za mwisho za kuwapata Makandarasi na kufikia mwishoni mwa mwezi Novemba 2022 Mikataba itakuwa imesainiwa.

 (ix)       Uboreshaji wa Bandari za Dar es Salaam, Mtwara na Tanga: Kuendelea na uboreshaji wa bandari za Dar-es-Salaam, Mtwara na Tanga ambapo jumla ya shilingi bilioni 328.56 zimetumika katika mwaka 2021/22 na shilingi bilioni 19.95 zimetumika katika robo ya kwanza ya mwaka 2022/23.

(x)         Kilimo:

Ruzuku ya Mbolea, Korosho na Pamba: Kwa kutumia mfumo maalum wa utambuzi unaotumia QR Code Serikali imeratibu uuzaji wa mbolea ambapo kufikia tarehe 5 Novemba, 2022 tani 67,296 za mbolea zenye thamani ya ruzuku ya shilingi bilioni 74.47 zimenunuliwa na wakulima kwa kutumia mfumo maalum. Serikali inaendelea na zoezi la usajili wa wakulima kwa kutumia alama za vidole(biometric registration) ambapo kufikia tarehe 5 Novemba, 2022 wakulima 2,118,911 wamesajiliwa kwenye mfumo huu. Kutolewa kwa shilingi bilioni 29 kwa ajili ya ruzuku ya pembejeo za Korosho na kutolewa ruzuku ya mbegu na viatilifu vya pamba vyenye thamani ya shilingi bilioni 75. Uzalishaji mbegu (ASA): kuwezesha upatikanaji wa mbegu za alizeti tani 2,500; kupatikana kwa tani 1,700 za mbegu za ngano; tani 400 za mbegu za soya na kuzalishwa miche 7,998,784 ya mazao mbalimbali. Ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji kwenye mashamba ya uzalishaji mbegu hekta 800 ambapo wakandarasi wanaendelea na kazi. Pia jumla ya hekta 1,300 za mashamba mapya ya kuzalisha mbegu yanaendelea kusafishwa.

Mheshimiwa Spika, Utafiti (TARI): Kukamilika kwa tathmini ya wazabuni wa ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji katika mashamba ya uzalishaji mbegu yenye ukubwa wa hekta 854; kuanza ujenzi wa ghala 5 na ukarabati wa ghala 5 za kuhifadhi mbegu zenye uwezo wa kuhifadhi tani 300 kila moja; kupata mzabuni wa ununuzi wa vifaa na madawa kwa maabara ya Mikocheni; ununuzi wa vifaa na madawa kwa maabara ya udongo ya TARI Mlingano ili kupata ithibati ya kimataifa; Ujenzi wa maabara ya Tissue Culture – Kituo cha TARI Mlingano na ukarabati wa biotechnology Mikocheni; ujenzi wa uzio (fensi) wa mashamba ya TARI Uyole. kwa upande wa Kilimo cha Umwagiliaji: Hadi kufikia mwisho wa robo ya kwanza ya mwaka 2022/2023 Jumla ya Mikataba 21 ya ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji kwenye skimu za kijamii yenye thamani ya shilingi bilioni 182 imesainiwa na wakandarasi wako uwandani (site). Aidha, miradi 15 yenye thamani ya shilingi bilioni 199.7 ipo katika hatua mbalimbali za manunuzi na inategemewa kusainiwa ifikapo mwezi Desemba, 2022.

Mheshimiwa Spika, Kilimo cha Mashamba Makubwa ya Pamoja (Block farming): Wizara imeratibu upatikanaji wa jumla ya ekari 183,000 za mashamba makubwa ya pamoja (block farms). Lengo ni kutatua changamoto ya upatikanaji wa ardhi, mitaji, teknolojia za kisasa na masoko kwa vijana na kinamama. Kazi ya kupima ardhi na afya ya udongo imekamilika; kazi ya kusafisha Shamba lenye ukubwa wa ekari 11,000 katika kijiji cha ndogowe Halmashauri ya Chamwino Dodoma inaendelea; Ujenzi wa Bwawa lenye ujazo wa lita za ukubwa Milioni 12 litakolomwagilia shamba lenye ekari 8,000 katika kijiji cha Membe Chamwino mkandarasi yuko uwandani (site); na uwekaji wa miundombinu ya umwagiliaji kwenye shamba la ekari 600 la Chinangali II unandelea. Vile vile, ekari 75 katika Kituo cha mafunzo ya Kilimo Bihawana kitakachotumika kutoa mafunzo ya umahiri ya Kilimo kwa vijana kabla ya kupelekwa kwenye mashamba makubwa linasafishwa na ukarabati wa majengo ya kituo uko hatua za mwisho. Mradi huu katika awamu ya kwanza  unategemea kutoa ajira 32,000 na kutengeneza ajira Milioni 8 ifikapo 2030.

Mheshimiwa Spika, Huduma za Ugani: Uanzishwaji wa kituo cha huduma kwa wakulima (Call Center); Kukamilika kwa andiko la ukarabati wa vituo sita vya rasilimali za kilimo vya Kata; Utambuzi wa maafisa ugani na vikundi vya wakulima kwa uanzishwaji wa mashamba darasa;  kutolewa mafunzo kwa maafisa ugani na utambuzi wa maeneo ya kuanzisha mashamba ya mfano kwa mazao ya alizeti, ufuta, na soya katika Mikoa ya Mbeya, Ruvuma, Songwe, Rukwa na Dodoma. Jumla ya shilingi bilioni 84.85 zimetumika katika mwaka 2021/22 na shilingi bilioni 47.37 katika robo ya kwanza ya mwaka 2022/23. Usalama wa Chakula. Kuimarika kwa usalama wa chakula ambapo hali ya uzalishaji wa chakula katika msimu wa 2021/22 umefikia tani 17,403,880 sawa na asilimia 115 ya Utoshelevu wa chakula nchini (Self Sufficiency Ratio – SSR). Mapato ya mauzo nje. Kuongezeka mapato ya mauzo ya mazao ya chakula na yasiyo ya chakula nje ya nchi kutoka Dola za Kimarekani Bilioni 1.8 katika mwaka wa fedha 2021/2022 ambapo katika mwaka wa fedha 2022/2023 Wizara ya Kilimo inatarajia mapato hayo kufika Dola za Kimarekani Bilioni 2. Ongezeko hilo ni kutokana na ongezeko la uzalishaji wa mazao ya chakula na yasiyo ya chakula ikiwemo Pamba, Tumbaku na Korosho;

 (xi)       Mifugo: Kukamilika kwa ujenzi wa majosho 192 katika mamlaka za Serikali za Mitaa 85; kuzalishwa kwa jumla ya dozi 50,261 za mbegu za mifugo; kukamilika kwa ujenzi wa minada nane (8) na ukarabati wa minada tisa (9); kukamilika kwa ujenzi wa mabwawa ya Chamakweza (Pwani), Kimambi (Lindi) na Mhanga (Singida); na kuanzishwa kwa program ya vituo atamizi (SAUTI Program = Samia Ufugaji kwa Tija Program) katika vituo 8 na kila kituo kuwa na vijana 30. Jumla ya vijana 240 wamesharipoti kwenye vituo hivyo na kuanza kutengeneza miundombinu inayohitajika kwa ufugaji kwenye vituo hivyo. Mchakato wa manunuzi ya ng'ombe wa kunenepesha umekamilika na ng'ombe watanunuliwa mara fedha zitakapotolewa. Jumla ya shilingi bilioni 15.35 zimetumika katika mwaka 2021/22 na shilingi bilioni 2.42 katika robo ya kwanza ya mwaka 2022/23.

(xii)      Uvuvi: Kukamilika kwa ujenzi wa mialo mitatu (3) ya Kayenze, New Igombe - (Mwanza) na Ihale – Busega (Simiyu); kukamilika kwa ujenzi wa soko la samaki Mbambabay (Ruvuma); kusainiwa kwa mkataba wa ujenzi wa Bandari ya  Uvuvi Kilwa Masoko; na kukamilika kwa hatua za awali za ununuzi wa meli mbili (2) za uvuvi katika Bahari Kuu. Jumla ya shilingi bilioni 44.85 zimetumika katika mwaka 2021/22 na shilingi milioni 500.0 katika robo ya kwanza ya mwaka 2022/23; Tathmini ya mazingira kwa ajili ya ufugaji samaki kwa njia ya vizimba imekamilika na maeneo ya kuweka vizimba kutambuliwa ambapo Vizimba 873 vinatarajiwa kujengwa. Mpango wa ununuzi wa boti 160 kwa ajili ya wavuvi na mchakato wa manunuzi kwa ajili ya kumpata mkandarasi wa ujenzi wa boti hizo unaendelea. Serikali imeshaanza ujenzi wa bandari ya uvuvi katika eneo la Kilwa Masoko Mkoani Lindi. Mkataba wa ujenzi wa bandari hiyo ulishasainiwa na Mkandarasi China Harbour Engineering ameshaanza maandalizi ya awali ya ujenzi wa bandari hiyo.

 (xiii)     Madini: Kupitia Mradi wa usimamizi endelevu wa rasilimali madini (SMMRP), imetekeleza shughuli mbalimbali za maendeleo zikiwemo: Kujengwa kwa vituo vitatu (3) vya umahiri katika masuala ya madini vya Chunya, Songea na Mpanda; Kuanzishwa kwa masoko mapya mawili (2) na vituo vya ununuzi wa  madini vipya 17 hivyo kufanya jumla ya masoko ya madini kuwa 42 na vituo vya ununuzi wa madini 83; kukamilika kwa ujenzi wa kiwanda cha mfano cha kuzalisha vitofali vinavyotokana na makaa ya mawe kwa matumizi ya majumbani na viwandani (Dar es Salaam); kuendelea na ujenzi wa ofisi ya Tume ya Madini Dodoma; Ununuzi wa magari 40 kwa ajili ya kuwezesha utekelezaji wa shughuli za Tume ya Madini; kukamilisha ujenzi wa kiwanda na kuanza uzalishaji wa mkaa mbadala (Rafiki Briquettes); Ununuzi wa mitambo nane (8) ya uchorongaji, Lori moja (1), Wheel Loader, Excavator na magari manne (4) kwa ajili ya ofisi za STAMICO. Jumla ya shilingi bilioni 8.40 zimetumika katika mwaka 2021/22 na shilingi bilioni 2.89 katika robo ya kwanza  ya mwaka 2022/23;

Mheshimiwa Spika, Kukamilisha ununuzi wa vifaa vya mawasiliano, gari moja, pikipiki nne (4) na kujenga minara ya barabara na saa Mirerani; kukamilisha taarifa ya TEITI ya mwaka 2018/19 ya ulinganifu wa malipo ya kodi kutoka kampuni za madini, mafuta na gesi asilia; na Kuendelea Kuimarisha na kuboresha mifumo mbalimbali ya utoaji leseni kwa kufanya ujenzi wa mfumo mpya wa usimamizi na utoaji wa leseni za madini ambapo utekelezaji umefikia asilimia 52; na ununuzi wa vifaa vya utafiti wa jiosayansi, maabara na uchunguzi kwa taasisi ya GST. Wizara ya Madini imelenga kutekeleza maeneo ya kipaumbele kama ifuatavyo:  kuendeleza madini ya kimkakati; kuwaendeleza wachimbaji wadogo na kuwawezesha wananchi kushiriki katika uchumi wa madini; kuhamasisha shughuli za uongezaji thamani madini; kuhamasisha uwekezaji na biashara katika Sekta ya Madini; na kuzijengea uwezo taasisi zilizo chini ya Wizara ya Madini ili ziweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi zaidi.

 (xiv)     Afya: Kuendelea na ukamilishaji wa ujenzi na ukarabati wa hospitali za rufaa za mikoa 19; kuendelea na ujenzi wa Hospitali 135  za Halmashauri ambapo hospitali 70 zimeanza kutoa huduma kwa wagonjwa wa nje;vituo vya afya 335 na zahanati 668,kununuliwa na kusambazwa kwa chanjo mbalimbali; na kufungwa kwa mitambo 19 ya kuzalisha hewa tiba ya Oksijeni katika hospitali za rufaa za mikoa na mitambo 13 katika Hospitali za Wilaya Jumla ya shilingi bilioni 563.85 zimetumika katika mwaka 2021/22 na shilingi bilioni 75.32 katika robo  ya kwanza ya mwaka 2022/23;

(xv)      Miradi ya Maji:  Kuboresha upatikanaji wa huduma ya maji ambapo hadi Juni 2022 umefikia wastani wa asilimia 74.5 vijijini kutoka asilimia 72.3 Juni 2021 na mijini asilimia 86.5 kutoka asilimia 86 mwaka 2021; kukamilika kwa utekelezaji wa miradi 394 ambapo wananchi wapatao 1,336,856 waishio vijijini wamenufaika; na miradi 145 imetangazwa ili kupata wakandarasi wa ujenzi. Aidha, Miradi ya maji katika miji 28 imeanza utekelezaji baada ya kupatikana wakandarasi; mkandarasi kwa ajili ya ujenzi wa bwawa la Kidunda amepatikana; na mtaalam mshauri kwa ajili ya ujenzi wa bwawa la Farkwa amepatikana. Kupitia mradi wa UVIKO-19, seti 25 za mitambo ya uchimbaji visima zimenunuliwa, seti 5 za mitambo ya uchimbaji na ujenzi wa mabwawa zimenunuliwa, miradi 154 ya maji vijijini na 42 mijini imeanza kutoa huduma kwa wananchi na utekelezaji wa miradi 18 ya maji vijijini na minne (4) ya mijini unaendelea na umefikia wastani wa asilimia 97. Jumla ya shilingi bilioni 598.5 zimetumika katika mwaka 2021/22 na shilingi bilioni 74.35 katika robo ya kwanza ya mwaka 2022/23;

(xvi)     Elimu: Kuendelea na utekelezaji wa programu ya Elimumsingi Bila Ada ambapo jumla ya shilingi bilioni 296.46 zimetolewa; kuendelea na ujenzi wa vyumba vya madarasa 3,425 (sekondari 1,295 na msingi 2,130); kutolewa kwa mikopo yenye thamani ya shilingi bilioni 569.0  kwa wanafunzi 177,925 wa Elimu ya Juu; na kukamilika kwa ujenzi wa madarasa mapya 15,000 (madarasa 12,000 kwa ajili ya shule za sekondari na madarasa 3,000 kwa ajili ya shule za msingi) na mabweni 50 ya wanafunzi wenye mahitaji maalum na ujenzi na ukarabati wa vyuo vya ufundi stadi katika Wilaya 25 na vyuo vinne (4) vya watu wenye ulemavu kupitia mradi wa UVIKO-19. Ukamilishaji wa madarasa uliwezesha wanafunzi wote 907,802 waliofaulu darasa la saba kuingia kidato cha kwanza mwaka 2022 bila kuwepo kwa awamu za kusubiria.  Kwa mwaka huu tayari tumetoa shilingi bilioni 160 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa 8,000 ya kuanzia, bado tunatafuta fedha za madarasa mengine 8,000 ili kupata madarasa 16,000 ya kuweza kutosheleza matarajio ya watoto wengi zaidi kujiunga na mwaka mpya wa masomo ya Sekondari. Jumla ya shilingi bilioni 1,187.56 zimetumika katika mwaka 2021/22 na shilingi bilioni 274.39 katika robo ya kwanza ya mwaka 2022/23;

(xvii)   Sensa ya Watu na Makazi: Kukamilika kwa zoezi la sensa ya watu, makazi na majengo ambapo jumla ya shilingi bilioni 117.81 zimetumika katika mwaka 2021/22 na shilingi bilioni 302.59 katika robo ya kwanza ya mwaka 2022/23. Aidha, matokeo ya Sensa ya mwaka 2022 yaliyozinduliwa na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, tarehe 31 Oktoba 2022, yameainisha kuwa, idadi ya watu nchini imefikia watu 61,741,120 kutoka watu 44,928,923 mwaka 2012. Kati ya watu waliohesabiwa, watu 59,851,347, sawa na asilimia 96.9 ya watu wote ni Tanzania Bara na watu 1,889,773 ni Tanzania Zanzibar. Aidha, matokeo ya Sensa ya mwaka 2022 yatatumika katika maandalizi ya mipango jumuishi ili kuleta maendeleo endelevu ya nchi na kugawanya kwa uwazi rasilimali zilizopo kuendana na uwiano wa idadi ya watu katika ngazi zote za utawala. Vile vile, matokeo haya yatatumika na Serikali na wadau wengine katika kufuatilia na kutathmini utekelezaji wa mipango ya maendeleo ya kitaifa na kimataifa ikijumuisha Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025, Mpango wa Tatu wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2021/22 - 2025/26) na Dira ya Maendeleo ya Jumuiya ya Afrika Mashariki 2050. Ni dhahiri kuwa kutokana na ongezeko hilo la idadi ya watu, gharama za utoaji huduma za Serikali kwa wananchi (public goods) zitaongezeka na hivyo Serikali itajipanga ipasavyo.

 

(xviii)  Utawala Bora na Utawala wa Sheria: Kuendelea na Awamu ya Pili ya ujenzi wa majengo ya Wizara katika Mji wa Serikali Mtumba; kufikia asilimia 99 ya ujenzi wa barabara zenye urefu wa km 51.2 kwa kiwango cha lami katika Mji wa Serikali Mtumba; kuendelea na ujenzi wa majengo ya mahakama katika maeneo mbalimbali nchini na vituo sita (6) jumuishi vya utoaji haki; na ujenzi wa majengo ya kutolea huduma jumuishi kwa taasisi za serikali zinazotoa huduma za kisheria mahakamani na wadau mbalimbali (Government Legal Institutions integrated centers-GLIICs) kwa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, Wizara ya Katiba na Sheria na RITA, chini ya Uratibu wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Mafanikio mengine yaliyopatikana ni: kufanyika maboresho ya kusomana kwa mifumo ya TEHAMA inayotoa huduma za malalamiko, maombi ya kufungua kesi nje ya muda, usajili wa watoa huduma za msaada wa kisheria, pamoja na usuluhishi na upatanishi; kuendelea na urekebu wa Sheria 446 za nchi ili ziendane na mahitaji ya wakati ambapo kazi ya uhakiki wa Sheria hizo kwa ajili ya kutangazwa inaendelea; kutafsiriwa kwa jumla ya Sheria Kuu 300 kutoka Lugha ya Kingereza kwenda Kiswahili; kuajiriwa kwa waandishi wa sheria, maafisa wa TEHAMA, mawakili wa Serikali na mahakimu; na kuteuliwa kwa majaji wapya 22 wa Mahakama Kuu ya Tanzania. Jumla ya shilingi bilioni 245.73 zimetumika katika mwaka 2021/22 na shilingi bilioni 93.83 katika robo ya kwanza ya mwaka 2022/23.

 

Mheshimiwa Spika, Usimamizi wa fedha za umma, Katika mwaka 2022/23 Serikali imeanza kuchukua hatua za kimakusudi ikiwemo kupitia upya muundo wa Idara ya Mkaguzi wa Ndani Mkuu, kuimarisha uhuru wa Idara ya Mkaguzi wa ndani Mkuu wa Serikali na vitengo vya Ukaguzi wa ndani katika Taasisi za Umma, kuipatia fungu linalojitegemea, mafunzo ya ukaguzi wa mifumo na kuifanya kamati za Ukaguzi kuwa na wajumbe wa nje wa tatu (3). Kadhalika Serikali ya CCM inayoongozwa na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa CCM imeiongezea bajeti Ofisi ya CAG ili kuwajengea uwezo wakaguzi, kuajiri wakaguzi wapya na kuongeza uwazi katika matumizi ya Serikali ili kuwezesha ofisi hizi kufanya kwa wakati na kukagua thamani ya fedha kwenye miradi, yaani Real time Audit na Value for Money.  Katika taarifa za CAG za kati ya kipindi cha 2019 hadi 2022, TAKUKURU, ilifungua majalada 897, kati ya hayo majalada 594 yalitokana na taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali, za mwaka 2019 mpaka 2021, majalada 303 yamefunguliwa kutokana na taarifa ya CAG iliyokabidhiwa kwa Mhe. Rais mwezi Machi 2022.

 

Mheshimiwa Spika, Kati ya majalada 353 uchunguzi wake umekamilika na watuhumiwa wamefikishwa Mahakamani, Majalada 96 kesi zinaendelea ziko hatua nzuri, kati ya kesi 11 ambazo uamuzi umeshafanywa na Jamhuri imeshinda kesi 10, na majalada 32 watuhumiwa wake wamechukuliwa hatua za kinidhamu.  Tuliokulia vijijini mtakumbuka, kuna wakati kulikuwa na vingere vinavyoibaiba mazao, hatukuacha kulima tuliwadhibiti, kuna wakati vitanda tulivyokuwa tunalalia vilipata kunguni, hatukuchoma nyumba ili kuua kunguni, tuliwamwagia maji ya moto, kuna wakati chawa waliingia kichwani kwenye nywele, hatukukata kichwa na kukitoa, tulinyolewa upara tu. Tumeongeza uwazi katika matumizi, tumeziongezea nguvu ofisi za ukaguzi ili mali zauma ziheshimiwe. Kwa hiyo hakuna atakayefuja fedha za umma, fedha za walipakodi wa Tanzania na akabaki salama, tutaendelea kuwafikisha kwenye mkono wa sheria. Ukitaka kumwelezea mtu kwa maneno machache kuhusu Tanzania, mwambie "Nchi inasonga mbele, kwa Uongozi Sahihi, uelekeo sahihi na mwendokasi sahihi", kwa kujiamini kabisa, mwambie awaelezee na wengine.

 

(xix)     Maliasili na Utalii: Uzinduzi wa The Royal Tour iliyoasisiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kutangaza vivutio vya utalii na Uwekezaji. Kufuatia hatua zilizochukuliwa na Serikali kutangaza vivutio vya utalii ikiwemo Royal Tour, idadi ya watalii iliongezeka kutoka watalii 637,052 mwaka 2020/21 hadi watalii 1,123,130 mwaka 2021/22 na mapato yatokanayo na utalii yaliongezeka kutoka dola za Marekani milioni 834.1 hadi dola za Marekani milioni 1,790.5 sawa na ongezeko la asilimia 114.7 katika kipindi hicho. Ongezeko hili la idadi ya watalii na mapato lilisaidia kuongeza fursa za ajira na kuchachua shughuli za uchumi kwenye sekta ya utalii na uwekezaji. Aidha, mafanikio yaliyopatikana katika uhifadhi maliasili ni: kupungua kwa ujangili na uvunaji haramu wa maliasili ambapo idadi ya wanyamapori imeongezeka katika mifumo mbalimbali ya Ikolojia Nchini; na kuongezeka kwa upatikanaji wa malighafi ya mazao ya misitu katika mashamba ya miti ya Serikali kutoka wastani wa mita za ujazo 729,000 kwa mwaka 2020/21 hadi mita za ujazo 1,000,000 kwa mwaka 2021/22;

 

(xx)      Sanaa, Utamaduni na Michezo: Katika kipindi hiki, uamuzi wa Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wa kuanza kutenga fedha kugharamia timu za taifa na matukio ya kimkakati ikiwemo kutoa asilimia 5 ya mapato ya michezo ya kubashiri matokeo kwenda Mfuko wa Maendeleo ya Michezo, umeanza na unaendelea kuzaa matunda. Sekta hizi ambazo ziliongoza kwa ukuaji wa asilimia 19 mwaka uliopita zimeendelea kuchachua uchumi, kuwapatia vijana wengi ajira na zaidi kuitangaza nchi. Kwa kipindi hiki ninayo furaha kuwaarifu kuwa kwa mara ya kwanza Timu yetu ya Michuano ya Jumuiya ya Madola iliyofanyika Julai-Agosti kule Birmingham Uingereza ilirejea nchini na medali tatu ikiwa ni baada ya miaka mingi ya kurejea patupu ikiwemo medali ya fedha kutoka kwa mwanariadha Alphonce Simbu. Aidha, Mwezi Septemba na Oktoba Timu zetu zilizowekwa kambini na kugharamiwa na Serikali, Tembo Warriors na Serengeti Girls zilifanya maajabu ya kufika robo fainali ya makombe ya dunia Uturuki na India mtawalia. Chini ya uwekezaji huu Tanzania pia iliandaa kwa mafanikio Mashindano ya Urembo na Utanashati kwa Viziwi Duniani ambapo Mtanzania Hadija Kanyama aliibuka kuwa mshindi wa dunia kwa wanawake. Shindano hili limeitangaza Tanzania duniani. Serikali itaendelea kuwekeza katika sekta hizi zenye mchango chanya na mtambuka kwa uchumi wa nchi.

 

(xxi)     Ushiriki wa Sekta Binafsi: Ushiriki wa sekta binafsi umeendelea kuongezeka ambapo jumla ya miradi 329 (127 wageni, 111 Watanzania na 91 ubia kati ya wageni na Watanzania) ilisajiliwa yenye thamani ya dola za Marekani milioni 4,517 na inatarajiwa kutoa ajira kwa watanzania wapatao 53,632. Aidha, katika azma ya Serikali kuendelea kuishirikisha na kuiwezesha sekta binafsi katika shughuli za kiuchumi, miradi na huduma nyingi zilitolewa na sekta binafsi kupitia bajeti ya Serikali. Kutokana na kuendelea kujenga mazingira mazuri ya biashara na uwekezaji pamoja na ushirikiano na sekta binafsi, matokeo chanya yameanza kupatikana kwa kuongeza uzalishaji kwa baadhi ya viwanda hapa nchini na hivyo kuleta athari chanya kwenye sekta ya kilimo na ajira. Katika robo ya kwanza ya mwaka 2022/23, kiwanda cha sukari cha Bagamoyo kimeanza uzalishaji kwa wastani wa tani 25,000 kwa mwaka. Vilevile, viwanda vya sukari vya Kagera, Kilombero, Mtibwa na TPC Moshi vimeendelea na upanuzi kwa ajili ya kuongeza uzalishaji wa sukari hapa nchini. Mategemeo yetu ni kwamba viwanda hivi vitakapoanza kuzalisha sukari katika uwezo wake wa juu (maximum capacity) changamoto ya pengo la sukari hapa nchini itakuwa imepungua kwa kiasi kikubwa ifikapo mwaka 2024/25.

 

 

 

Aidha, kiwanda cha tumbaku cha Mkwawa kimefufuliwa kwa upatikanaji wa mwekezaji mahiri ambapo kwa takwimu za mwaka huu kiwanda kimezalisha ajira za moja kwa moja zaidi ya 800 na kimewezesha kununuliwa kwa tumbaku zote za wakulima na kuleta bei shindani kwenye zao hili. Haya yote ni matokeo ya ushirikiano mzuri wa Serikali na Sekta Binafsi chini ya uongozi makini wa Serikali ya Awamu ya sita inayoongozwa na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.  

 

22.       Mheshimiwa Spika, maelezo ya kina kuhusu utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa mwaka 2021/22 na robo ya kwanza ya mwaka 2022/23 yameainishwa katika kitabu cha Mapendekezo ya Mpango (Sura ya Pili).

 

2.4      Changamoto za Utekelezaji wa Mpango na Bajeti na Hatua na Kukabiliana nazo

23.       Mheshimiwa Spika, Utekelezaji wa Mwongozo wa mwaka 2021/22 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2021/22 ulikabiliwa na changamoto mbalimbali zikiwemo:

(i)          Vita inayoendelea nchini Ukraine ambayo imedhoofisha matarajio ya kurejea kwa shughuli za kiuchumi zilizokuwa zimeathiriwa na UVIKO-19. Hivyo, kasi ya ukuaji wa uchumi inatarajiwa kupungua kufikia asilimia 4.7 mwaka 2022 ikilinganishwa na matarajio ya awali ya asilimia 5.2;

(ii)         Kuongezeka kwa bei na gharama za usafirishaji wa bidhaa na huduma kutoka nje, hususan bidhaa za petroli, mafuta ya kula, mbolea kutokana na athari za vita inayoendelea nchini Ukraine;

(iii)        Kukosekana kwa mazingira wezeshi ya matumizi ya teknolojia kwa baadhi ya Wizara, Taasisi za Umma na Mamlaka za Serikali za Mitaa katika ukusanyaji wa mapato ya Serikali. Mfano ulipaji wa kodi ya ardhi, leseni za biashara; na

(iv)        Kuendelea kuwepo kwa baadhi ya wafanyabiashara wanaokwepa kodi hususan kupitia njia za magendo, uhamishaji wa faida kwa kampuni zenye mtandao wa kimataifa na kutokutoa stakabadhi za kielektroniki wakati mauzo yanapofanyika hivyo kuathiri ukusanyaji wa mapato yatokanayo na kodi.

 

 

 

 

24.       Mheshimiwa Spika, katika kukabiliana na changamoto za utekelezaji wa Mpango na Bajeti, Serikali imeendelea kuchukua hatua zifuatazo:

(i)          Kuendelea kuongeza tija katika sekta za uzalishaji ikiwemo kilimo, mifugo, uvuvi na nishati ambazo zina fursa nyingi zisizotumika ipasavyo;

(ii)         Kuendelea kutoa ruzuku katika bidhaa za petroli kwa lengo la kupunguza gharama za maisha kwa wananchi;

(iii)        Kuendelea kutekeleza miradi ya kimkakati ya kuongeza mapato ya ndani, kubuni vyanzo vipya vya mapato na kutafuta masoko ya bidhaa nje ili kuongeza uwezo wa Serikali kugharamia Mpango na Bajeti;

(iv)        Kuendelea kufuatilia kwa karibu mwenendo wa biashara duniani ili kuchangamkia fursa zitokanazo na athari za UVIKO-19 na vita kati ya Urusi na Ukraine, hususan uzalishaji wa mazao ya biashara na chakula pamoja na kuchukua hatua za kisera na kiutawala kurejesha biashara zilizoathirika;

(v)         Kuendelea kuimarisha mifumo ya usimamizi na ukusanyaji wa mapato ili kudhibiti ukwepaji kodi pamoja na kuhamasisha umma juu ya umuhimu wa kulipa kodi, matumizi ya stakabadhi za kielektroniki na kuhimiza malipo ya Serikali kwa kutumia namba ya kumbukumbu ya malipo (Control Number); na

(vi)        Kuimarisha usimamizi wa mapato yasiyo ya kodi katika Wizara na Idara Zinazojitegemea ili kuhakikisha mikakati iliyopangwa ya kuongeza mapato inatekelezwa ipasavyo ili kuongeza ufanisi.


3.0       MWONGOZO WA MAANDALIZI YA MPANGO NA BAJETI YA SERIKALI KWA MWAKA 2023/24

 

25.       Mheshimiwa Spika, misingi itakayozingatiwa kufikia shabaha za uchumi jumla ni: kuongezeka kwa ushiriki wa sekta binafsi kwenye shughuli za uwekezaji na biashara; kuendelea kuhimili athari za majanga ya asili na yasiyo ya asili; kuendelea kuhimili athari zitokanazo na kushuka kwa uchumi wa dunia na kuongezeka kwa bei za bidhaa na huduma katika soko la dunia; kuendelea kuimarika kwa utoshelevu wa chakula nchini; na uwepo wa amani, usalama, umoja na utulivu wa ndani na nchi jirani.

 

26.       Mheshimiwa Spika, shabaha na malengo ya uchumi jumla yatakayozingatiwa katika muda wa kati ni pamoja na:

(i)          Pato la Taifa linakadiriwa kukua kwa asilimia 4.7 mwaka 2022 kutoka asilimia 4.9 mwaka 2021 na kuendelea kukua hadi asilimia 5.3 mwaka 2023;

(ii)         Kuendelea kudhibiti kasi ya mfumuko wa bei na kuhakikisha kuwa unabaki kwenye wigo wa tarakimu moja ya wastani wa asilimia kati ya 3.0 hadi 5.0 katika muda wa kati;

(iii)        Mapato ya kodi kufikia asilimia 12.0 ya Pato la Taifa mwaka 2023/24 kutoka matarajio ya asilimia 11.7 mwaka 2022/23;

(iv)       Nakisi ya bajeti (ikijumuisha misaada) kuwa chini ya asilimia 3.0 ya Pato la Taifa; na

(v)         Kuwa na akiba ya fedha za kigeni kwa kiwango cha kukidhi mahitaji ya uagizaji wa bidhaa na huduma kutoka nje kwa kipindi kisichopungua miezi minne (4).

 

3.1      Mfumo wa Awali wa Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka 2023/24

27.       Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2023/24, Serikali inatarajia kukusanya na kutumia jumla ya shilingi bilioni 43,294.6 ikilinganishwa na makadirio ya shilingi bilioni 41,480.6 mwaka 2022/23. Kiasi kilichoongezeka ni sawa na asilimia 4.4. Ongezeko hili limezingatia mwenendo halisi wa ukusanyaji wa mapato ya ndani na jitahada zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali za kuongeza mapato. Aidha, ongezeko hilo limezingatia mahitaji yasiyoepukika (first charge expenditure) kama vile mikataba ya  kugharamia miradi mbalimbali, deni la Serikali na mishahara ya watumishi wa umma. Mwaka 2023/24, mapato ya ndani yanakadiriwa kuwa shilingi bilioni 31,034.6 sawa na asilimia 71.7 ya bajeti yote. Aidha, Washirika wa Maendeleo wanatarajiwa kuchangia shilingi bilioni 4,511.0 sawa na asilimia 10.9 ya bajeti. Serikali inatarajia kukopa shilingi bilioni 5,638.5 kutoka soko la ndani ambazo zinajumuisha shilingi bilioni 3,542.1 kwa ajili ya kulipia hatifungani na dhamana za Serikali zinazoiva na shilingi bilioni 2,096.4 kwa ajili ya kugharamia miradi ya maendeleo. Vile vile, mikopo ya masharti ya kibiashara kutoka nje inatarajiwa kuwa shilingi bilioni 2,110.6.

 

28.       Mheshimiwa Spika, baadhi ya mikakati itakayotumika katika kufikia lengo la makusanyo ya mapato ya ndani ni pamoja na kuendelea: kuwatengea wafanyabiashara na watoa huduma wadogo maeneo maalum kwa lengo la kukuza biashara zao; kutambua na kusajili kampuni za kimataifa zinazoendesha biashara za kidigitali nchini kwa kutumia mfumo wa usajili uliorahisishwa (simplified registration regime); kuwekeza kwenye matumizi ya teknolojia ili kuhakikisha mifumo ya Serikali inabadilishana taarifa; kusimamia mikakati ya kuongeza ufanisi katika ukusanyaji wa mapato ya Wizara na Idara Zinazojitegemea; na kuimarisha hatua za kiutawala za usimamizi na ukusanyaji wa kodi.

 

29.       Mheshimiwa Spika, matumizi ya Serikali yanakadiriwa kuwa shilingi bilioni 43,294.6, ambapo shilingi bilioni 28,266.6 ni matumizi ya kawaida na shilingi bilioni 15,028.0 ni matumizi ya maendeleo, sawa na asilimia 34.7 ya bajeti. Hii imetokana na kuongezeka kwa mahitaji ya uendeshaji katika matumizi ya kawaida ikiwemo deni la Serikali; mishahara ya watumishi wa umma; uendeshaji wa miradi iliyokamilika ikijumuisha miundombinu ya kutolea huduma za afya na elimu; maandalizi ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa mwaka 2024; na maandalizi ya Dira Mpya ya Taifa ya Maendeleo mwaka 2050. Aidha, kufuatia matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022, ni dhahiri kuwa gharama za utoaji huduma za jamii zitaongezeka kutokana na ongezeko la idadi ya watu nchini kutoka watu 44,928,923 mwaka 2012 hadi watu 61,741,120 mwaka 2022.

 

30.       Mheshimiwa Spika, mfumo wa awali wa mapato na matumizi ya Serikali kwa mwaka 2023/24 umeainishwa katika Jedwali Na. 4.3 na 4.4 katika Sehemu ya Kwanza, Sura ya Nne ya Kitabu cha Mwongozo.

 

 

 

3.2      Maelekezo Mahsusi ya Mwongozo

31.       Mheshimiwa Spika, Mwongozo wa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2023/24 umeainisha maelekezo mbalimbali ambayo Maafisa Masuuli watatakiwa kuyazingatia wakati wa uandaaji, utekelezaji, ufuatiliaji, tathmini na utoaji wa taarifa. Hivyo, Maafisa Masuuli wanaelekezwa kuzingatia kikamilifu maelekezo yote yaliyopo kwenye Mwongozo wakati wa uandaaji, utekelezaji, na ufuatiliaji na tathmini ya mpango na bajeti. Miongoni mwa maelekezo hayo ni kama ifuatavyo:

 

3.2.1 Uandaaji

(i)          Kuandaa bajeti ya miradi ya maendeleo kwa kuzingatia vipaumbele vya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2023/24 na kwa kuwa Dira ya Taifa ya Maendeleo inakamilika mwaka 2025, hivyo kipaumbele cha bajeti kiwe ni ukamilishaji wa miradi ya maendeleo inayoendelea kabla ya kuanzisha miradi mipya;

 

(ii)         Kutenga bajeti ya kuandaa miradi inayoweza kutekelezwa kwa utaratibu wa ubia baina ya sekta ya umma na binafsi (PPP). Miradi ya PPP ipewe msisitizo zaidi ili kupunguza utegemezi wa bajeti ya Serikali katika kutekeleza miradi ya maendeleo. Serikali inaendelea kukamilisha taratibu za mapitio ya Sheria ya PPP ili kuifanya wezeshi katika utekelezaji wa miradi kwa njia ya PPP.

 

(iii)        Kuzingatia Waraka wa Mkuu wa Utumishi wa Umma Na.2 wa mwaka 2021 kuhusu utaratibu wa kutumia magari, aina na stahili za magari kwa viongozi katika utumishi wa umma na hii ijitokeze kwenye bajeti ya mafungu husika. Watumishi waliofikia stahiki ya kuendeshwa kwa magari ya Serikali wakopeshwe magari na siyo kununuliwa na Serikali;

 

(iv)       Kutenga bajeti na kulipa gharama za uendeshaji wa ofisi ikiwemo umeme, maji, simu, mtandao, pango, ulinzi, usafi, mafuta na matengenezo ya magari. Aidha, madeni yatakayozalishwa katika kasma hizi yatalipwa kwa kutumia fedha za matumizi mengineyo za Fungu husika;

(v)         Halmashauri zenye mapato yasiyolindwa chini ya shilingi bilioni mbili (Kundi C), zinaelekezwa kutenga kiasi kisichopungua asilimia 20 kwa ajili ya miradi ya maendeleo ikijumuisha asilimia 10 ya Mikopo ya Wanawake, Vijana na Watu Wenye Ulemavu; na

(vi)       Kupata idhini kutoka kwa Waziri mwenye dhamana ya masuala ya Fedha kabla ya kupokea mikopo, misaada na dhamana kwa mujibu wa Sheria ya Mikopo, Dhamana na Misaada, Sura 134, Kifungu cha 15(1).

 

3.2.2 Utekelezaji

(i)          Kutoingia mikataba bila kuwa na bajeti na kukamilisha maandalizi ya awali ikiwemo kufanya upembuzi yakinifu na kulipa fidia kwa wananchi watakaopisha maeneo ya miradi ili kuepuka malimbikizo ya madai na malipo ya riba na gharama za mitambo zinazotokana na kutoendelea kutekelezwa kwa mradi (idle charges);

(ii)         Kuhakikisha mapato yote katika Wizara na Taasisi za Umma yanaendelea kukusanywa kupitia Mfumo wa GePG na yanaingizwa katika Mfuko Mkuu wa Hazina ya Serikali isipokuwa pale ilipoelekezwa vinginevyo kwa mujibu wa Sheria husika;

(iii)        Kuzingatia Sheria za Kodi ikiwa ni pamoja na kukata kodi ya zuio (withholding tax) na kudai risiti za kielektroniki kwa malipo yote yanayofanywa kwa wazabuni na wakandarasi;

(iv)       Kuzingatia maelekezo ya Waraka wa Hazina Na. 2 wa Mwaka 2019 unaohusu utaratibu wa kuomba, kuhamisha, kupokea, kutumia, kuhasibu na kutoa taarifa za utekelezaji wa miradi ya D-Fund na matumizi ya Mfumo wa Usimamizi wa Fedha Zinazopelekwa Moja kwa Moja kwenye miradi;

(v)         Kuimarisha uwajibikaji na udhibiti katika usimamizi wa malipo ya mishahara ili kuhakikisha kuwa watumishi wanaolipwa mishahara ni wale wanaostahili na kwa viwango wanavyostahiki;

(vi)       Kusimamia upelekaji kwa wakati wa ruzuku za Wakala na Taasisi za Serikali zilizo katika Mafungu wanayosimamia;

(vii)      Kuhakikisha ununuzi wa umma unafanyika kwa kuzingatia Sheria ya Ununuzi wa Umma, Sura 410 na Kanuni zake kwa kufanya ununuzi wa pamoja na kutumia Mwongozo wa Matumizi ya Force Account wa Mei 2020 ili kupata thamani halisi ya fedha;

(viii)     Kutumia kikamilifu rasilimali za maji zilizopo nchini ili kupanua wigo wa fursa zilizopo kwenye uchumi wa buluu;

(ix)       Kuendelea kugharamia uhamisho wa watumishi, utekelezaji wa ujenzi wa ofisi na miundombinu ya Serikali Dodoma; na

(x)         Kuendelea kutekeleza Blueprint kwa kuboresha sheria mbalimbali ikiwa ni pamoja na kufanya tathmini ili kuweka misingi mizuri ya kusimamia mazingira bora ya kufanya biashara na uwekezaji nchini. Aidha, matokeo ya tathmini hiyo yataisaidia Serikali katika kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji.

 

3.2.3 Ufuatiliaji na Tathmini

(i)          Kuzingatia Waraka wa Hazina Na. 5 wa mwaka 2021/22 na Mfumo wa Kitaifa wa Kusimamia Miradi ya Maendeleo (NPMIS);

(ii)         Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kwa kushirikiana na Mamlaka ya Serikali Mtandao kusimamia uhuishaji wa mifumo ya ukusanyaji wa mapato ili kuwezesha mapato yote kukusanywa sehemu moja na kuhakikisha kuwa mifumo yote inafanyiwa ukaguzi maalum kila baada ya nusu mwaka;

(iii)        Kusimamia uimarishaji wa vikao vya Kamati ya Bajeti kwa ajili ya kupitia na kujadili taarifa za ufuatiliaji, tathmini na utekelezaji kila robo mwaka ili kuleta uwazi na uwajibikaji;

(iv)       Kuandaa taarifa za utekelezaji kwa kuzingatia muundo ulioainishwa katika Sehemu ya Pili, Sura ya Pili ya Mwongozo. Taarifa za utekelezaji za kila robo ya mwaka ziwasilishwe ndani ya siku 30 baada ya kukamilika kwa robo ya mwaka husika. Vilevile, taarifa za utekelezaji za mwaka ziwasilishwe kabla ya tarehe 15 Oktoba ya mwaka unaofuata;

(v)         Kuimarisha Vitengo vya Ukaguzi wa Ndani kwa kuvipatia vitendea kazi na kuwajengea uwezo watumishi ili kuongeza mawanda ya ukaguzi; na

(vi)       Kuendelea kutumia taarifa za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali katika kuboresha mifumo ya ufuatiliaji na tathmini ya utekelezaji wa mpango na bajeti.

 

32.       Mheshimiwa Spika, maelezo ya kina kuhusu maelekezo mahsusi ya Mwongozo yanapatikana katika Sehemu ya Pili, Sura ya Kwanza ya Kitabu cha Mwongozo.


4.0       MAPENDEKEZO YA MPANGO WA MAENDELEO WA TAIFA WA MWAKA 2023/24

 

33.       Mheshimiwa Spika, Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2023/24 yatajielekeza katika kukamilisha utekelezaji wa miradi na programu za maendeleo zilizoainishwa katika maeneo matano ya kipaumbele ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (2021/22-2025/26). Maeneo hayo ni:

 

(i)          Kuchochea Uchumi Shindani na Shirikishi: Eneo hili litajikita katika kuimarisha utulivu wa uchumi jumla; kuboresha uzalishaji na kuimarisha miundombinu ya usafiri na usafirishaji, umeme na TEHAMA;

(ii)         Kuimarisha Uwezo wa Uzalishaji Viwandani na Utoaji Huduma: Eneo hili litajikita katika kuwezesha ujenzi wa viwanda vinavyotumia malighafi na rasilimali zinazopatikana nchini; na kuendelea kuboresha miundombinu ya umwagiliaji, uhifadhi wa mazao, masoko, mifugo na uvuvi; ikiwemo kuwezesha wananchi kushiriki katika uzalishaji na kuongeza thamani ya bidhaa hasa zile za kilimo kupitia viwanda vidogo vidogo.

(iii)        Kukuza Biashara na Uwekezaji: Eneo hili litajikita katika kusimamia utekelezaji wa Mpango Kazi wa Kuboresha Mazingira ya Biashara na mifumo ya uratibu na usimamizi wa masuala ya uwekezaji, biashara na masoko;

(iv)       Kuchochea Maendeleo ya Watu: Eneo hili litajikita katika kuimarisha utoaji wa huduma za jamii ikiwemo afya, maji, elimu, utambuzi, upangaji, upimaji na urasimishaji wa ardhi nchini; na kuimarisha huduma za maendeleo ya jamii na makundi maalumu; na

(v)         Kuendeleza Rasilimali Watu: Eneo hili litajikita katika kukuza ujuzi kwa vijana, kurasimisha ujuzi uliopatikana nje ya mfumo rasmi wa mafunzo; na kutoa mafunzo kwa vitendo mahali pa kazi kwa wahitimu wa elimu ya juu.

 

34.       Mheshimiwa Spika, Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2023/24 yataendelea na ukamilishaji wa miradi ya kielelezo yenye matokeo makubwa katika ukuaji wa uchumi inayojumuisha: Ujenzi wa Reli ya Kati kwa Kiwango cha Kimataifa (SGR); Mradi wa Kufua Umeme wa Maji wa Julius Nyerere – MW 2,115; Kuboresha Shirika la Ndege Tanzania (ATCL); Ujenzi wa Bomba la Mafuta Ghafi kutoka Hoima (Uganda) hadi Tanga (Tanzania); Mradi wa Kuchakata na Kusindika Gesi Asilia kuwa Kimiminika (LNG) – Lindi; na Ujenzi wa Madaraja Makubwa na Barabara za Juu mfano Daraja la Kigongo - Busisi (Mwanza).

 

35.       Mheshimiwa Spika, katika Kujenga Uchumi Shindani na Viwanda kwa Maendeleo ya Watu, Taifa linahitaji ushiriki wa sekta binafsi yenye uwezo wa kuchangia katika utekelezaji wa Mpango. Kwa msingi huo, Serikali itaendelea kuweka mazingira wezeshi ya uwekezaji kwa sekta binafsi kwa kufanyia kazi maoni na ushauri wa kukabiliana na changamoto za sekta binafsi katika utekelezaji wa Mpango na miradi ya maendeleo. Aidha, katika mwaka wa fedha 2023/24 miradi ya Makaa ya Mawe - Mchuchuma na Chuma - Liganga pamoja na Bandari ya Bagamoyo inatarajiwa kutelekezwa kwa kushirikisha sekta binafsi.

 

 

36.       Mheshimiwa Spika,  maelezo ya kina kuhusu Maeneo ya Kipaumbele kwa mwaka 2023/24 yapo katika Kitabu cha Mapendekezo ya Mpango (Sura ya Tatu).

 

5.0       HITIMISHO

 

37.       Mheshimiwa Spika, Mapendekezo ya Mwongozo na Mpango yatawezesha kukamilika kwa maandalizi ya Bajeti za Mafungu kwa wakati; kuimarika kwa usimamizi wa matumizi ya fedha za umma; kuimarika kwa utawala bora unaozingatia misingi ya sheria; na kuongezeka kwa uwajibikaji na ushiriki wa wadau mbalimbali katika uandaaji, utekelezaji na ufuatiliaji na tathmini ya Mpango na Bajeti. Hivyo, Maafisa Masuuli wa Wizara, Idara Zinazojitegemea, Wakala za Serikali, Sekretarieti za Mikoa, Mamlaka za Serikali za Mitaa, Taasisi na Mashirika ya Umma wanaelekezwa kuzingatia kikamilifu maelekezo yote yaliyopo kwenye Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali na Mapendekezo ya  Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka 2023/24. Aidha, wanaelekezwa kuzingatia kikamilifu Sheria ya Bajeti, Sura 439 na Kanuni zake.

 

38.       Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo hayo naomba sasa Bunge lako Tukufu lipokee na kujadili Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka 2023/24.

 

39.       Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.

 

 

Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba Madelu (Mb)

WFM

07 Novemba, 2022


 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.