Habari za Punde

ZATO yaandaa chakula cha usiku kwa kwa Mabalozi wa Tanzania Hoteli ya Park Hyatt

Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale Mhe. Simai Mohamed Said akizungumza katika Hafla ya Chakula cha Usiku kilichoandaliwa na Taasisi inayosimamia Makampuni yanayoandaa Misafara ya Watalii Zanzibar (ZATO) kwa Mabalozi wa Tanzania akimuwakilisha Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla iliyofanyika Hotel ya Park Hyyat Shangani Zanzibar.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Stegomena Lawrence Tax akizungumza na mabalozi na wageni mbali mbali waliohudhuria katika hafla ya chakula cha usiku kwa mabalozi wa Tanzania iliyofanyika hotel ya Park Hyyat Shangani Zanzibar.

 

Baadhi ya wageni waliohudhuria katika hafla ya chakula cha usiku kwa mabalozi wa Tanzania iliyofanyika hotel ya Park Hyyat Shangani Zanzibar.


Na Abdulrahim Khamis, OMPR
Kufanyika kwa Mkutano wa Mabalozi wanaoiwakilisha Tanzania katika Nchi mbali mbali hapa Zanzibar kutasaidia kutangaza Fursa zilizopo pamoja na kukuza Uchumi wake.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla ameyasema hayo katika Hafla ya Chakula cha Usiku ilichoandaliwa na Taasisi inayosimamia Makampuni yanayaondaa Misafara ya Watalii Zanzibar (ZATO) kwa Mabalozi wa Tanzania Hafla hiyo iliyofanyika Ukumbi wa Park Hyyat Shangani Jijini Zanzibar.

Mhe. Hemed akiwakilishwa na Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale Mhe. Simai Mohamed Said ameeleza kuwa ni Fursa ya kipekee kwa Mabalozi hao kutembelea Maeneo mbali mbali ya Zanzibar hatua ambayo itawasaidia kuweza kuitangaza Zanzibar katika nyanja tofauti.

Ameeleza kuwa Serikali ya Awamu ya Nane inayoongozwa na Rais Dkt. Hussein Ali Mwinyi imeamua kujielekeza katika Dhana ya Uchumi wa Buluu kwa lengo la kukuza  Uchumi wake kwa kutumia Bahari.

Aidha Mhe. Hemed amesema ana Imani Mabalozi hao wataitangaza Tanzania kwa Mazuri yake na Fursa zilizopo ili Wawekezaji kuja kuwekeza na hatimae Pato la Taifa liongezeke katika Pande zote mbili za Muungano.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ameongeza kuwa Imani waliopewa Mabalozi hao kuiwakilisha Tanzania ni muhimu kwao ambapo Taifa linawategemea katika uwakilishi wao kwa Maslahi ya Wote pamoja na kuitangaza Tanzania Duniani kote.

Sambamba na hayo Mhe. Hemed  ameipongeza Taasisi inayosimamia Makampuni yanayaondaa Misafara ya Watalii Zanzibar (ZATO) kwa kuandaa Chakula hicho na kuwataka Mabalozi hao kuwa karibu na Taasisi hiyo ikiwa ni Taasisi muhimu  katika kujenga Utalii endelevu kwa manufaa ya Tanzania.

Nae Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Stergomena Lawrence Tax ameeleza kuwa kuwepo kwa Mkutano uliwakutanisha Mabalozi wanaoiwakilisha Tanzania katika Mataifa mbali mbali kumetoa Fursa ya Mabalozi hao kufahamu mengi zaidi katika kuboresha utendaji wao wa Kazi.

Aidha Mhe. Tax ameipongeza ZATO kwa kuandaa Chakula hicho cha Usiku na kueleza kufarishwa na maamuzi hayo na kuahidi kuendelea kuwa karibu nao ili kukuza Sekta ya  Utalii Tanzania.

Mapema Mwenyekiti wa Taasisi inayosimamia Makampuni yanayaondaa Misafara ya Watalii Zanzibar Ndugu Hassan Ali Mzee ameeleza kuwa Mabalozi hao ni sehemu ya kutangaza Utalii wa Tanzania ambapo uwepo wao katika Nchi wanazofanya kazi itasaidia kurahisisha huduma bora kwa Watalii wanaokuja Nchini Tanzania.

Ameeleza kuwa bado Zanzibar inakumbwa na wasambaza watalii wasio rasmi na kuwataka Mabalozi hao kuhamasisha Watalii wanaokuja Zanzibar kutumia Makampuni yaliyosajiliwa kisheria ili kupata Huduma bora kipindi chote wanapokuwa  Zanzibar.

 

 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.