Habari za Punde

Mhe Hemed ameitaka jamii kujenga upendo na kuwa wamoja


 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Alhajj Hemed Suleiman Abdulla amejumuika na Waumini wa Msikiti wa Ijumaa wa Forodhani katika Ibada ya Sala Ijumaa.

Akiwasalimia Waumini hao Alhajj Hemed ameitaka Jamii kuendelea kuwa wamoja na wenye upendo kama Uislamu ulivyoelekeza ili kuweza kupata jamii yenye umoja na mshikamano baina yao.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ameendelea kuwaasa waumini na wananchi kwa ujumla kuendeleza matendo mema ikiwemo kusaidiana na kuhurumiana jambo ambalo linaongeza mapenzi na huruma baina ya Wananchi.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amesema ni jukumu la kila mmoja kuwasaidia  watu wenye mahitaji maalum wakiwemo watu wenye ulemavu, Mayatima, wajane na Maskini ili kuendeleza utamaduni uliokuwepo miaka iliyopita katika visiwa vya Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.

Aidha Mhe. Hemed ameeleza kuwa miongoni mwa mila na tamaduni za kizanzibari ni kukaa vyema na majirani ambapo amewataka waumini hao kuendeleza utamaduni huo kwa kuwahurumia majirani wanaohitaji ili kupata fadhila mbele ya Allaah.

Pamoja na hayo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amesema Uislamu umeelekeza Suala la kuendeleza Amani na utulivu huku akiwataka  wazanzibari kuitumia neema hio, jambo ambalo kila mmoja ana wajibu wa kulisimamia kwa nafasi yake ili kuleta chachu ya maendeleo nchini.

Sambamba na hayo Alhajj Hemed ameikumbusha jamii hiyo kuendelea kuwaombea Dua wagonjwa na waliotangulia mbele ya haki na kusisitiza kila mmoja kutenga muda wa kutembelea wagonjwa ili kuwafariji pamoja kupata ukumbusho uliokuwemo ndani yake.

Mapema katika Khutba ya Ijumaa Sheikh Thani Miraji ameikumbusha jamii ya wazanzibar kuwatunza wazee na kuwahurumia hasa wanapofikia umri wa utu uzima kama uislamu ulivyoamrisha.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.