Habari za Punde

SMZ Itaendelea Kutatua Changamoto Zinazowakabili Wananchi wake na Kuwafikishia Maendeleo ya Haraka

 

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk.Hussein Ali Mwinyi (kulia) alipokuwa akisisitiza jambo wakati akizungumza na Waumini wa dini ya Kiislamu  mara baada kujumuika katika Swala ya Ijumaa katika  Masjid Al Swafaa uliopo  Gongoni  Wilaya ya Mjini, Mkoa Mjini Magharibi

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Al hajj Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema Serikali ya Zanzibar itaendelea kutatua changamoto zinazowakabili wananchi wake na kuwafikishia maendeleo ya haraka kwa kadri ya hali inavyorusu katika kufanikisha malengo iliyojiwekea.

Al hajj Dk.  Mwinyi aliyasema hayo wakati akizungumza na wananchi na waumini aliojumuika nao pamoja wakati wa sala ya Ijumaa huko Masjid Al – Swafaa, Kikwajuni - Gongoni, Shehia ya Kisima majongoo, Wilaya ya mjini Unguja. Leo Disemba 30,2022.

Alisema tatizo la mtaro linalowakabili wananchi wa eneo hilo ambalo limekuwa kero kubwa kwao, Serikali italitatua kwa haraka ili kuwapa wepesi wananchi wake wa kuendelea na masuala ya msingi ya ujenzi wa nchi na maendeleo kwa ujumla.

Sambamba na hilo Dk. Mwinyi alitumia fursa hiyo kuwanasihi wazazi, walezi, wazee,  masheikh pamoja na viongozi wa eneo hilo, kujenga jamii yenye maadili na iliyoshiba imaani na hofu ya kumuogopa Mwenyezi Mungu, ili kupata jamii bora na yenye heshima na mapenzi kwa taifa lao.

“Jamii kujengwa kimaadili ndio ufumbuzi mkubwa zaidi ili kupata vijana nwenye imani, uweledi na nidhamu ya uzalendo kwa taifa lao” Dk. Mwinyi akiinasihi jamii ya Gongoni, Mjini Unguja.

Al hajj Dk.  Mwinyi pia aliwanasihi vijana na waumini kwenye msikiti huo kusameheana kwa waliokoseana kwa namna yoyote ya maisha yao, aidha, aliwataka kutubia na kurejesha kwa walivyowachukuliwa wenzao ili kujenga jamii yenye maadili na imani ya vitendo.

“Vijana watambue kwamba kudhulumu ni jambo baya sana, yako mambo tutamkosea Mwenyezi Mungu moja kwa moja tutubieni, lakini yale tunayowakosea, binaadamu wenzetu, tuwatake msamaha, kama kuna chao tumechukua turudishe, kisha tutubie” Alinasihi Dk. Mwinyi.

Katika hatua nyingine Al hajj Dk.  Mwinyi aliwahakikishia wananchi hao kwamba serikali yao bado inapambana na kukabilina na wanaofanya dhulma kuwadhulumu wenzao na kwamba serikali itawachukulia hatua na kuwawajibisha.

Hivyo, aliwataka wananchi hao kupunguza matatizo katika jamii yanayotokana na masuala ya dhulma.

 “Huku kwengine tuachieni tutaendelea kupambana, kupambana kwa maana ya wale wanaofanya dhulma tukigundua tunawachukulia hatua, lakini dhulma zishakuwa nyingi na nyngine za muda mrefu, yapo masuala ya nyumba, migogoro ya viwanja, serikali inayatambua hayo”. Alitahadharisha Dk. Mwinyi

Naye, Katibu Mtendaji kutoka Ofisi ya Mufti Zanzibar, Khalid Ali Mfaume  aliwanasihi waumini wa dini ya kiislamu na kuwashauri kwa kutofungamana na haki za watu, badala yake kurejesha dhulma wanazodhulumiana na kudumu kwenye istighfari ili kumcha Mwenyezi Mungu kikweli.

Aidha, aliwataka waumini hao kuwa na mipaka katika kuchukua haki za watu, sambamba na kuwataka wajitathmini kwa matendo waliyofanya mwaka 2022 kwa kuukaribisha vyema mwaka 2023 kwa kumcha Allah (S.W) kwa dhati ya nafsi zao.

Omar Abdi Abdalla, Khatib wa msikiti wa Masjid Al Swafaa wa Gongoni, alisema dini ya Kiislaam imeweka mwongozo mzuri kwa waumini wake kufanya toba ili kutubia makosa waliomkosea Mwenyezi Mungu.l

Akizungumza kwa niaba ya uongozi wa Msikiti wa Masid Al – Swafaa uliopo Gongoni, Kikwajuni, Ali Salum Mkweche alisema Wananchi wa eneo hilo wanaungamkono jitihada zinazofanywa na serikali ya awamu ya nane na kwamba maendeleo anayofanya Rais Dk. Mwinyi ni makubwa na yakupigiwa mfano kwani kipindi kifupi cha uongozi wake wameshuhudia maendeleo makuwa katika sekta zote za Elimu, Afya na Maji safi na salama.

Imetayarishwa na Idara ya Mawasiliano

Ikulu Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.