Habari za Punde

Mhe Hemed afungua majengo ya kikosi cha Valantia kambi ya Muyuni


Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla akikata utepe kufungua  mradi wa nyumba, mahanga na ofisi za Kikosi cha Valantia Zanzibar (KVZ) kambi ya Muyuni Mkoa wa Kusini Unguja ikiwa ni katika maadhimisho ya kutimia miaka 59 ya Mapinduzi ya Zanzibar 
 Mhe. Hemed Suleiman Abdulla  akikuhutubia katika hafla ya ufunguzi wa mradi wa Nyumba, Mahanga na Ofisi za Kikosi cha Valantia Zanzibar (KVZ) kambi ya Muyuni Mkoa wa Kusini Unguja ikiwa ni shamrashamra za kuadhimisha miaka 59 ya mapinduzi ya Zanzibar .
Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Idara Maalum za SMZ Ndugu Issa Mahfoudh akitoa taarifa ya kitaalamu kuhusu mradi wa Nyumba, Mahanga na Ofisi za Kikosi cha Valantia katika hafla ya ufunguzi wa Majengo hayo yaliyopo kambi ya Muyuni Mkoa wa Kusini Unguja.
Mkuu wa Kikosi cha Valantia Zanzibar (KVZ) Meja Said Ali Juma Shamhuna akisoma risala ya Kikosi hicho wakati wa ufunguzi wa mradi wa Nyumba, Mahanga na Ofisi za Kikosi cha Valantia Zanzibar (KVZ) kambi ya Muyuni Mkoa wa Kusini Unguja ikiwa ni shamrashamra za kuadhimisha miaka 59 ya mapinduzi ya Zanzibar 

muonekano wa Majengo ya makazi ya Askari wa Kikosi cha Valantia Zanzibar (KVZ) yaliyopo Muyuni Mkoa wa Kusini Unguja yaliyozinduliwa rasmi na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla ikiwa ni shamrashamra za maadhimisho ya miaka 59 ya Mapinduzi ya Zanzibar.

 

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kuwawekea mazingira mazuri Maafisa na wapiganaji wa Idara Maalum za SMZ ili waendelee na majukumu yao ya kulinda Amani na utulivu Nchini.

 

Mhe. Hemed ameyasema hayo wakati wa ufunguzi wa mradi wa Nyumba, Mahanga na Ofisi za Kikosi cha Valantia Zanzibar (KVZ) kambi ya Muyuni Mkoa wa Kusini Unguja ikiwa ni shamrashamra za kuadhimisha miaka 59 ya mapinduzi ya Zanzibar .

 

Amesema dhamira ya Mapinduzi matukufu ya Januari 1964 ni kumkomboa mwananchi mnyonge ambapo Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya Awamu ya Nane inaendeleza dhana hiyo kwa kuwawekea mazingira mazuri kwa kuwapatia miradi ya maendeleo pamoja na nyumba za makazi ya maafisa na wapiganaji.

 

Sambamba na hayo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ameridhishwa na matumizi mazuri ya fedha zilizotumika katika mradi huo hatua ambayo inaonesha uimara na uzalendo wa kikosi hicho katika kusimamia fedha za Serikali.

                 

Amesema ni hatua ya kuridhisha kuona Kikosi hicho kinaendeleza dhamira ya Mapinduzi kwa kubuni mradi wa kituo cha Mafuta (Petrol Station), maduka ya kibiashara na mradi wa ufugaji wa kuku wa kisasa katika kambi hiyo ikiwa ni sehemu ya vyanzo vya mapato.

 

Amesema mpango huo unaenda sambamba na jitihada za Serikali ya mapinduzi ya Zanzibar kuzitaka Taasisi zote za Serikali kubuni vyanzo vya mapato kwa lengo la kuweza kujiendesha na kutatua changamoto ndogo ndogo zinazojitokeza katika uendeshaji wa Taasisi.

 

Aidha ameeleza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaendelea na ujenzi wa miradi mbali mbali ya maendeleo kwa kasi ya kuridhisha miradi ambayo tumeshuhudia kukamilika kwa muda mfupi na ikiwa na viwango vya hali ya juu.

 

Hata hivyo, Mhe. Hemed amewaomba maafisa na wapiganaji wa Kikosi cha Valantia  Zanzibar (KVZ) kuthamini juhudi za Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi kwa kuendelea kuwajibika kwa kufanyakazi kwa bidii na maarifa ili kuendelea kuiweka Zanzibar katika hali ya amani na utulivu.

 

Nae Waziri wa Nchi Afisi ya Rais Tawala za Mikoa na Idara Maalum za SMZ Mhe. Masoud Ali Muhamed amempongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa kuendelea kuijenga Zanzibar kimaendeleo na kutenga Fedha kwa ajili ya ujenzi wa miradi katika Kambi mbali mbali za Idara Maalum za SMZ.

 

Aidha ameeleza kuwa Afisi ya Rais Tawala za Mikoa na Idara Maalum SMZ itaendelea kupokea maelekezo kutoka kwa viongozi wakuu wa Nchi yenye lengo la kuimarisha na kukuza Idara hizo ili zitekeleze majukumu yao kwa ukamilifu.

Akitoa taarifa ya kitaalamu ya mradi huo katibu mkuu afisi ya rais, tawala za mikoa na idara maalum za SMZ Issa Mahfoudh ameeleza utekelezaji wa mradi huo kwa Zanzibar ni wa miaka mitano 2018-2019 hadi 2022-2023 ambao utagharimu jumla ya shilingi Bilioni nne na milioni mia moja na sabiini.

Kwa upande wake Mkuu wa Kikosi cha Valantia Zanzibar (KVZ) Meja Said Ali Juma Shamhuna ameeleza kuwa Majengo hayo yamejengwa katika Kambi mbali mbali nchini ikiwemo Muyuni, Kikungwi, Mwanyanya na Mto wa Maji kwa lengo la kuwawekea mazingira mazuri wapiganaji hao pamoja na kuwaweka wananchi katika hali ya usalama.

 

………….

Abdulrahim Khamis

Afisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.