Habari za Punde

SMZ Imejipanga Vizuri Kuiletea Mabadiliko Makubwa Sekta ya Elimu Zanzibar

 

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akihutubia wakati wa kukabidhi zawadi za Komputa (Laptop) alizowaahidi Wanafunzi wa Kidatu cha Sita na Cha Nne waliofanya vizuri mitihani yao ya Taifa mwaka 2022 na kupata Daraja la Kwanza, hafla hiyo iliyofanyika katika viwanja vya Ikulu Jijini Zanzibar leo 11-1-2023.

SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema imejipanga vizuri kuiletea mabadiliko makubwa sekta ya Elimu visiwani ili kuongeza ufaulu kwa wanafuzi wengi.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi ameyasema hayo Ikulu mjini Unguja alipowakabidhi kompyuta wanafunzi 1142 waliofanya vizuri kwenye mitihani ya kidato cha nne na sita ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa ahadi yake kwao.

Alisema bila ya elimu hakuna taifa linalofanikiwa kwa maendeleo na kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali imejipanga kufanya mageuzi makubwa kuondosha changamoto zinazoikabili wizara hiyo na kuongeza kuwa Elimu ni kipaumbale chake cha kwanza.

“Huwezi kupata maendeleo yoyote uliyoyakusudia kuyafanya kama  huna wataalamu, kwa hiyo elimu itaendelea kuwa kitaombele cha kwanza cha Serikali” alieleza Dk. Mwinyi.

Alieleza Serikali ilivyojipanga kuboresha miundombinu kwa kuelendelea kujenga skuli mpya za ghorofa zenye komputa, maktaba na maabara kwa msingi na sekondari pamoja na kuondosha mikondo kwenye skuli zote za serikali ili wanafunzi wasome mara moja tuu kwa awamu.

Dk. Mwinyi aliongeza kwamba mwaka huu wa 2023 serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imedhamiria kujenga madarasa mapya mengine yasiyopungua 2000 ambayo yatasheheni vitendea kazi vikiwemo madawati, vifaa vya maabara na vitabu pamoja na kuongeza wataalamu wakiwemo walimu wa Sayasi na hesabati”

“Tuna uhaba wa walimu katika fani mbalimbali hususan walimu wa sayansi na hesabati, kwa hiyo lazima tuongeze walimu wa sayansi, lazima tuongeze walimu wa hesabati, lazima tuongeze mafunzo kwa waalimu ili watoe watalamu wengi wa sayansi...” alieleza Dk. Mwinyi.

 Aidha, aliwataka watendaji wa Wizara ya Elimu kurejesha utamaduni wa ukaguzi kwa skuli ya serikali pamoja na kuangalia upya suala la lugha kwa wanafunzi wa madarasa ya msingi ili kuondosha changamoto ya kutojua lugha kwa wanafunzi kwenye skuli za serikali.

Hata hivyo, Dk. Mwinyi aliwaomba wadau wote wa Elimu Zanzibar kuendelea kuiungamkono serikali katika kufanikisha adhma ya Mapinduzi ya kuimarisha elimu visiwani inaongezaka na kueleza kuwa serikali pekee haiwezi kufanya kila kitu badalayake ushirikiano wao utaleta tija kuongeza maendeleo kwenye sekta hiyo.

Mapema akizungumza kwenye ghafla hiyo, Waziri wa Elimu, Sayansi na teknolojia wa Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Prf. Adolf Mkenda alieleza hatua ya Dk. Mwinyi kuwazawadia wanafunzi wanaofanya vizuri kwenye mitihani yao ya taifa itachochea juhudi za kuongeza ufaulu visiwani na kueleza wanafunzi hao mbali na kunufaika kupitia Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar lakini pia wananufaika kupitia udhamini wa Samia Suluhu Hassan ambao unatoa udhamini wa masomo ya elimu ya juu wa asilimia mia moja kwa wanafunzo wote wanaofanya vizuri kwenye masomo ya sayansi.

Prf. Mkenda alisema Zanzibar ilitoa skuli 10 kwa wanafunzi waliofanya vizuri kwenye masomo ya sayansi na kunufaika na udhamini huo ikiwemo skuli ya sekondari ya Lumumba.

Naye Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Lela Muhamed Mussa alimshukru DK.Mwinyi kwa ugawaji wa kompya hizo na vishkwambi kwa walimu wa skuli zote za serikali za Unguja na Pemba na kueleza kuwa vifaa hivyo vitaongeza nguvu kwenye mradi mkubwa kwa wa e.WEMA Wizarani hapo na kueleza kuwa mradi huo utaunganisha Wizara na taasisi zake zote, wanafunzi na walimu wa skuli zote za msingi na sekondari na kila mtendaji wa Wizara na Idara zake.

Aidha, Waziri Lela alisema mradi huo utaisaidia Wizara, Idara na taassisi zake kupata taarifa wanazozihitaji kitaaluma kwa usahihi na wakati bila ya kutumia mtandao na kueleza kwamba mradi huo upo chini ya Idara ya Tehama kutoka Wizara ya Elimu, Zanzibar inashirikiana na Seririkali ya Ausrtia ambao pia utahusisha ofisi zote za elimu za Mikoa, Wilaya na vituo vya elimu.

Jumla ya wanafunzi 1142 waliofaulu daraja la kwanza walikabidhiwa kompya mpakato na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Mwinyi, Ikulu Zanzibar ambapo wanafunzi 449  kati ya hao kutoka kidato cha nne na wanafunzi 693 wa kitato cha sita kwa skuli za Serikali na binafsi kwa upande wa Unguja.

Kwa upande wa Pemba jumla ya wanafunzi 288 walipata daraja la kwanza kati ya hao137 kidato cha nne na 151 kidato cha sita. Aidha, jumla ya Vishkwambi 6600 kutoka Wizara ya Elimu, sayansi na Teknolojia ya serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania ambavyo ni sehemu ya vishikwambi vilivyotumika kwenye sensa ya watu na makaazi Tanzania ya mwaka 2022, Dk. Mwinyi alivikabidhi kwa walimu wa Skuli za serikali za Unguja na Pemba chini ya usimamizi wa walimu wakuu wa skuli hizo.

IDARA YAMAWASILIANO,

IKULU

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.