Habari za Punde

JAFO: Takriban Shs.Trilion Moja Kupatikana kwa Biashara ya Kaboni

 

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo amesema huenda zaidi ya sh. trilioni moja zikapatikana kwa mwaka kutokana na biashara ya kaboni.

Pia ametoa wito kwa wabunge kuhamasisha wananchi katika maeneo yao kushiriki katika biashara hiyo kwa kupanda miti kwa wingi hatua itakayosaidia katika kupambana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Ametoa kauli hiyo Februari wakati akichangia Taarifa ya utekelezaji wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira iliyowasilishwa bungeni jijini Dodoma Februari 01, 2023.

Amesema Wakala wa Huduma za Mistu Tanzania (TFS) sasa waongeze nguvu katika kuhakikisha misitu yote inayotunzwa, badala ya kukatwa kwa ajili ya kuni, mkaa au matumizi mengine sasa itatumika katika biashara ya kaboni 

Dkt. Jafo amesema miongoni mwa maeneo ambayo yameanza kunufaika na biashara ya kaboni ni pamoja na Halmashauri ya Tanganyika mkoani Katavi ambayo kwa wastani kwa mwaka inapata takriban sh. bilioni 2 hadi 3 hivyo ametoa hamasa kwa wilaya zingine kuhakikisha wanatunza misitu kwa ajili ya biashara hiyo.

“Niwaombe ndugu zangu wabunge tupitie kanuni na mwongozo wa kusimamia biashara ya kaboni hii itasaidia sana hasa jatika kuhakikisha maeneo yetu na kuona jinsi gani tunayaelekeza hasa katika suala zima la kuvuna hewa ukaa,” amesisitiza.

Aidha, amesema Waziri Jafo amesema biashara ya kaboni itagusa TFS ambao wana dhamana ya kuhifadhi misitu na kilimo (agro-forest) kwa wakulima wanaojihusisha na kilimo cha mikorosho, miparachichi na kahawa.

Katika hatua nyingine Dkt. Jafo amewapongeza wananchi kwa kuiunga mkono Serikali kwa kuchukulia ajenda ya kuhifadhi mazingira katika umuhimu wake kwa kuhakikisha wanapanda miti na kuitunza.

Awali akichangia katika taarifa hiyo Mbunge wa Kuteuliwa Mhe. Liberata Mulamula ametoa wito kwa Serikali kuchangamkia fursa ya kupata fedha za mabadliko ya tabianchi zinazotolewa na nchi zilizoendelea kwa nchi zinazoendelea.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.