RAIS wa Zanzibar
na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Al hajj Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema Serikali
inajitahidi kufanya kila linalowezekana kuwapunguzia wananchi changamoto ya ugumu
wa maisha uliochangiwa na athari za kupanda kwa gharama za bidhaa nchini.
Al hajj Dk. Mwinyi aliyasema hayo wakati akizungumza
na wananchi na waumini wa kiislamu waliohudhuria ibada ya sala ya Ijuma huko
Msikiti wa Forodhani, Wilaya ya Mjini, Mkoa wa Mjini Magharibi - Unguja.
Alisema kupanda kwa ghamara za bidhaa kumechangiwa
na athari mbalimbali nje ya Zanzibar na kueleza kwamba wananchi wa visiwa vya
Unguja na Pemba mbali ya kutegemea bidhaa za chakula kutoka nje ya nchi lakini
kwa baadhi ya vyakula hutoka Tanzania bara ambako nako bidhaa zimepanda bei
kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo ukame ulioathiri baadhi ya Mikoa
inayozalisha sana chakula kushindwa kupata mavuno mazuri yenye kutosheleza
mahitaji ya watu wote.
Alisema hali hiyo, imechangia Zanzibar bidhaa
kupanda bei maradufu na kueleza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inajitahidi
kukabiliana na hali hiyo ili kuleta nafuu kwa wananchi hasa kipindi hiki
wananchi na waumini wa dini ya kiislam wakielekea kwenye Mwezi Mtukufu wa
Ramadhani.
Al hajj Rais Mwinyi alisema, Serikali pia imechukua
hatua kadhaa za kukabiliana na hali hiyo ikiwemo kutoa ruzuku kwa baadhi ya
bidhaa hususan mafuta ambayo yameathiri zaidi sekta ya usafirishaji nchini inayobeba
dhima nzima ya uchumi na kugusa maisha ya wananchi.
Akizungumzia bidhaa za chakula, Al haj Rais
Mwinyi alisema kuelekea mwenzi mtukufu wa Ramadhani, Serikali imehakikisha
kwamba bei za vyakula inapungua nchini.
Aidha, aliwasihi waumini wa dini ya kiislam na Watanzania
kwa ujumla kuendeleza ibada kwa kufanya mema yanayompendeza Mwenyezi Mungu na
kuachana na yanayomchukiza hasa kwenye miezi hii Mitukufu ya Rajabu, Shaabani
na Ramadhani kwa kuongeza ibada na kuendelea kumuomba kuifungulia neema nchini
ili bidhaa zishuke bei.
“Tunamuomba Mwenyezi Mungu atufungulie neema ya mvua
nzuri ili mazao yastawi vizuri bidhaa zipatikane kwa wingi na zishuke bei”
alieleza Al hajj Mwinyi.
Hata hiyo, aliwasihi waumini wanaosali msikitini
hapo kuendelea kuutunza na kuukarabati kwa sehemu zinazohitaji matengenezo ili
msikiti udumu.
“Waliotangulia waliitunza misikiti hii, ndio
maana na sisi tumeikuta, hivyo
tunawajibu wa kwa hali na mali kukarabati na kuitunza misiki yote” alinasihi Al
hajj Dk. Mwinyi.
Alhaj Dk. Mwinyi alitoa ahadi ya kuchangia
shilingi milioni tano ikiwa ni sehemu ya mchango wake msikitini hapo.
Akizungumza kwenye ibada ya sala hiyo, Katibu Mtendaji kutoka Ofisi ya Mufti Zanzibar, Khalid
Ali Mfaume aliwataka waumini hao kutakiana mema na kuacha kuhusudiana kutokana
na neema alizowaruzuku Mungu.
Alisema Mwenyezi Mungu amewaumba binaadamu na kuwatofautisha kupitia neema
zake, hivyo aliwasihi kuendelea kutendeana mazuri badala ya kuhusudiana.
IDARA YAMAWASILIANO – IKULU, ZANZIBAR
No comments:
Post a Comment