Na Khadija Khamis – Maelezo .14/02/2023.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kamisheni ya Kukabiliana na Maafa Zanzibar, Makame Khatibu Makame amewataka wafugaji kuhakikisha wanawapatia chanjo wanyama wao ili kuepukana na madhara yanayoweza kujitokeza ikiwemo maradhi ya kichaa cha mbwa.
Kauli hiyo ameeleza jana huko katika Ukumbi wa Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais,Vuga wakati alipokutana na Wakurugenzi na Maafisa wa sekta mbali mbali kujadili jinsi ya kukabiliana na maradhi ya kichaa cha mbwa ambayo yanaonekana kuzuka hivi siku za karibuni katika maeneo mbali mbali ya Wilaya za Unguja.
Amesema hivi karibuni kumezuka maradhi hayo,hivyo wafugaji wa mbwa pamoja na paka wa hakikishe kuwa wanawapatiwa chanjo wanyama wao ambazo zinatolewa bure katika Idara ya maendeleo ya Mifugo maruhubi ili kuyathibiti madhara hayo.
Alieleza kuwa suala hilo lifanywe haraka kuwapeleka wanyama hao ili kudhibiti maradhi hayo na kuepusha madhara yanayo weza kutokea kwa wanyama wengine na jamii kwa ujumla.
Nae Daktari Mkuu wa mifugo Ali Zahran Mohamed amesema wamekuwa wakipokea baadhi ya kesi za kutafunwa kwa watu katika maeneo mbali mbali kama vile Wilaya ya Kati,Wilaya ya Magharibi A’,na Wilaya ya Magharibi B’ pamoja na Wilaya za Kaskazini Unguja.
Amesema Idara ya mifugo inaendelea kuchukuwa jitihada na tahadhari ya kuhakikisha tatizo hilo linakabiliwa kupitia mpango wa chanjo inayofanyika kila Mwaka katika Wilaya zote 11 za Unguja na Pemba.
Alifahamisha kuwa ugonjwa wa kichaa cha mbwa unasababishwa na virusi ambavyo huathiri mfumo wa fahamu wa binaadamu mara tu anapo tafunwa na mnyama alioathirika na maradhi hayo,mtu hupelea kuwa na dalili mbaya ya homa kali na hatimae akichelewa kutibiwa huweza kupoteza maisha.
Aidha alisema Idara ya Maendeleo na mifungo inaendelea na zoezi la chanjo ili kuthibiti hali hiyo hadi sasa wameshachanja mbwa 4118 na paka 305 kwa unguja na kuwataka wamiliki wa mbwa na jamii kutoa mashirikiano.
Akitoa tathmini daktari huyo alisema wamekuwa wakipima sampuli mbali mbali kwa kila mwaka katika mwaka 2022 wameweza kupima sampuli 36 kati ya hizo nane zilikutwa zimeathirika na maradhi hayo na kuanzia Januari 2023 hali leo febuari 13 wameweza kupima sampuli kumi kati ya hizo nne zilikutwa zina virusi vya maradhi hayo.
Akizungumzia taarifa ya maradhi hayo kwa upande wa Kisiwa cha Pemba alisema tokea mwaka 2018 hadi sasa hakujaripotiwa kesi yoyote ya maradhi hayo au kutafunwa mtu kutokana na kufanikiwa kwa zoezi la chanjo
No comments:
Post a Comment