NAIBU Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) Zanzibar, Dkt.Mohammed Said Mohammed (Dimwa), akitoa mkono wa pole kwa familia ya aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar marehemu Hassan Mussa Takrima, aliyefariki juzi nyumbani kwake Fuoni Zanzibar.
NA IS-HAKA OMAR,ZANZIBAR.
NAIBU Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) Zanzibar, Dkt.Mohammed Said Mohammed (Dimwa), ametoa mkono wa pole kwa familia ya aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Ndg.Hassan Mussa Takrima aliyefariki juzi nyumbani kwake Fuoni baada ya kuumwa kwa muda mrefu.
Dkt.Dimwa, akizungumza na familia hiyo amesema Chama Cha Mapinduzi kimepokea kwa masikitiko makubwa taarifa kifo cha Mwanasiasa na kada huyo.
Amesema Chama na Serikali wamepoteza mtu muhimu aliyekuwa ni kiongozi na mwalimu aliyebobea katika masuala ya sisasa na uongozi.
Katika maelezo yake Dkt.Dimwa, amesema marehemu Takrima alikuwa ni kiongozi muadilifu na mchapakazi aliyefanya kazi kwa ufanisi ndani ya Chama na Serikalini.
“Natoa pole kwa familia ya marehemu, tulipata taarifa za kifo chake wakati mimi nikiwa katika ziara ya kujitambulisha Kisiwani Pemba na niliporudi tu nikaona nije kuwapa pole kwa niaba ya Chama Cha Mapinduzi.
Kama mnavyojua kuwa Mzee wetu Takrima alikuwa ni mtu muhimu sana kutokana na uhodari wake wa kiutndaji ametufundisha mambo mengi katika uwanja wa siasa pamoja na utendaji serikalini.”, alisema Dkt.Dimwa.
Pamoja na hayo aliwasihi wanafamilia hao kuendelea kuwa na subra na uvumilivu katika kipindi chote cha kuombeleza msiba huo.
Marehemu Takrima, alizaliwa mwaka 1943 katika kijiji Mwaleni ya Makunduchi, Mkoa wa Kusini Unguja na alipa elimu ya msingi na Sekondari katika skuli ya Makunduchi na mafunzo ya Ualimu katika Chuo cha Nkurumah na Nchini Uingereza.
Aidha marehemu Takrima, enzi za uhai wake amewahi kushika nyadhifa mbalimbali zikiwemo Mkuu wa Wilaya ya Ngara,Mkuu wa Wilaya ya Kusini Pemba,Mkuu wa Mkoa Kusini Pemba na Mkuu wa Wilaya ya Magharibi “B”.
Kwa upande wa Chama amewahi kuwa mjumbe wa NEC na mwaka 1998-2000 alishika nyadhifa ya Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar na Mkuu wa Idara Makao Makuu Dodoma.
Dkt.Dimwa, alifuatana na Viongozi mbalimbali wakiwemo Katibu wa Kamati Maalum ya NEC,Idara ya Itikadi na Uenezi CCM Zanzibar Khamis Mbeto Khamis, Katibu wa Kamati Maalum ya NEC, Idara ya mambo ya Siasa na Uhusiano wa Kimataifa CCM Zanzibar Khadija Salum Ali, Katibu wa Kamati Maalum ya NEC,Idara ya Organazesheni CCM Zanzibar Omar Ibrahim Kilupi na Makamu Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi wa CCM Taifa Dogo Idd Mabrouk.
Akizungumza kwa niaba ya familia ya marehemu Omar Saleh, alimshukru Naibu Katibu Mkuu Dkt.Dimwa kwa kuwafariji.
No comments:
Post a Comment